Afrikaans (Suid-Afrika)

منبرٌ كبيرٌ لنشر وسطية الأزهر الشريف بكل لغات العالم

 

Hotuba ya Imamu Mkuu  Prof. Ahmad Al-Tayyib  Sheikh Mkuu wa Al-Azhar  kwenye  Kikao cha Kimataifa cha Undugu wa Kibinadamu
Anonym

Hotuba ya Imamu Mkuu Prof. Ahmad Al-Tayyib Sheikh Mkuu wa Al-Azhar kwenye Kikao cha Kimataifa cha Undugu wa Kibinadamu

 

 

Hotuba ya Imamu Mkuu

Prof. Ahmad Al-Tayyib

Sheikh Mkuu wa Al-Azhar

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Kiislamu

 

kwenye

 

Kikao cha Kimataifa cha Undugu wa Kibinadamu

Abu-Dhabi - Umoja wa Falme za Kiarabu

 

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

Ndugu yangu na rafiki yangu kipenzi/ Mtakatifu Papa Francis – Papa wa Kanisa Katoliki Duniani.

Ndugu yangu kipenzi/ Sheikh Muhammad bin Zayed na ndugu yake Sheikh Muhammad bin Rashid pamoja na ndugu zake viongozi wa nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu.

Amani iwe kwenu na rehema za Mwenyezi Mungu na Baraka zake

Ama baada ya hayo

Ninaanzaa hotuba yangu kwa kutoa shukurani kwa nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu: Kuanzia viongozi wa nchi pamoja na wananchi wake kwa kupokea tukio hili la kihistoria ambalo linakutanisha viongozi wa Dini, wanachuoni wake, viongozi wa Makanisa, wana siasa, wanafikra, wanafasihi na wanahabari… jopo hili la kimataifa linakutana leo kwenye ardhi ya “Abu-Dhabi” ili kushuhudia pamoja na ulimwengu kwa ujumla kuanza kwa “Waraka wa Undugu wa Kibinadamu” pamoja na yale yanayokusanya waraka huu ikiwa ni wito wa kueneza utamaduni wa amani, kuheshimiana pamoja na kufikia ustawi wa wanadamu wote badala ya utamaduni wa chuki, dhuluma, utumiaji nguvu na umwagaji damu, na kuwataka viongozi wa ulimwengu, wanasiasa na wale wanaosimamia mustakabali wa wananchi na nguvu za kijeshi na kiuchumi - kuingilia kati haraka ili kusimamisha umwagaji damu na kuua watu wasio na hatia, pamoja na kuweka kikomo cha mwisho cha yale yanayoshuhudiwa ikiwa ni pamoja na mivutano, fitina, vita vinavyorudisha nyuma ustaarabu na kukaribia kuibua vita vya tatu vya dunia.

Ndugu waalikwa

Mimi ni katika kizazi kinachoweza kuitwa kizazi cha vita, kwa maana zote za neno hili kuanzia hali ya hofu, wasiwasi na matatizo mbalimbali, bali ninakumbuka maneno ya watu - baada ya vita vya pili vya dunia -  kuhusu hali ya vita na yale yaliyotokea ikiwa ni pamoja na umwagikaji wa damu pamoja na uharibifu mkubwa uliotokea, nilikuwa nakaribia umri wa miaka kumi wakati huo mpaka pale tulipovamiwa na vita vya uaduia vya pande tatu mnamo mwezi Oktoba 1956, na niliona kwa jicho langu shambulizi la kijeshi kwa kutumia ndege za kivita zikishambulia uwanja wa ndege wa mji wangu wa Luxor na namna tulivyoishi kwenye kiza kinene pasi na kufumba hata ukope wa jicho usiku mzima mpaka mapambazuko ya asubuhi, na namna tulivyokuwa tumestushwa na mashambulizi ya anga na kukimbilia ghoba, bado akili imeendelea kuhifadhi kumbukumbu hii chungu na kupelekea kujifungia ndani kama kwamba bado haijapita miaka sitini… vita hivi havikupita miaka kumi mwishowe vikaibuka vita vyengine ndani ya mwaka 1967, na vilikuwa ni vita vikali mno kuliko vilivyotangulia, tumeviishi vita hivi na machungu yake yote, tuliishi baada ya vita hivi kwa miaka sita katika hali iliyotambulika kwa jina la vita vya kiuchumi, hatukuweza kupumua tukiwa wenye furaha isipokuwa mwaka 1973 katika vita vya ukumbozi wa eneo la Sinai ambavyo vilirudisha heshima ya Waarabu wote, na kuwaletea nguvu, kuwa na sauti, uwezo wa kuondoa dhuluma kwa watu wao na kuvunja mwiba wa uadui na maadui…. Na tulidhania wakati huo kuwa tumemaliza zama za vita na tumeanza zama za amani, usalama na uzalishaji.

Lakini hata hivyo kwa haraka kabisa mambo yalibadilika baada ya hapo pale tulipokumbwa na wimbi jipya la vita mbaya inayoitwa “Ugaidi” ulioanza miaka ya tisini, kisha ukachukua kasi baada ya hapo mpaka leo hii umekuwa unashughulisha utulivu wa dunia Mashariki na Magharibi.

Matumaini yalikuwa ni kuendelea kwa miongo mitatu na kuondoka kabisa mawimbi ya utumiaji nguvu, ugadi, uuaji wa watu wasio na hatia wakiwemo wanaume, wanawake na watoto wadogo, lakini mara moja matumaini hayo yakapotea kwa mara ya tatu pale tuliposhtukizwa na tukio la mlipuko wa majengo ya biashara huko New York nchini Marekani mnamo tarehe kumi na moja mwezi wa tisa mwanzoni mwa karne ya ishirini na moja, tukio ambalo Uislamu na Waislamu ndio waliolipa thamani yake kubwa sana, na kuwachukua kiasi cha bilioni moja na nusu ya Waislamu kwa sababu ya uharifu wa wachache wasiozidi idadi ya vidole vya mikononi, tukio hili lilitumika vibaya mno katika mwelekeo wa vyombo vya habari vya dunia kwa kuuonesha Uislamu kuwa ni Dini yenye kiu kubwa ya kumwaga damu, na kuwaonesha Waislamu ni watu waovu na wa hatari sana wenye kuvamia staarabu za jamii zilizoendelea, vyombo hivi vya habari vilifanikiwa kueneza hisia za chuki na hofu kwa watu wa Magharibi kuhofia Uislamu na Waislamu, na kuzingira hali kubwa ya wasiwasi siyo kwa magaidi tu bali ni kwa kila yule ambaye ni Mwislamu..

Mabibi na Mabwana

Hakika “Waraka wa Undugu” ambao leo tunaadhimisha kuanzisha kwake ndani ya ardhi hii nzuri umezaliwa kwenye meza tukufu nami nilikuwa mwalikwa nikialikwa na ndugu yangu rafiki yangu kipenzi Francis nyumbani kwake wakati alipohotubia mmoja wa vijana waliohudhuria kwenye meza hii iliyobarikiwa, hotuba iliyopata kukubalika sana na Mtakatifu Papa pamoja na kupata kuungwa mkono na mimi, hii ni baada ya mazungumzo mengi tuliyozingatia ndani yake hali ya ulimwengu na mazingira yake pamoja na matatizo ya waliouawa, masikini, wajane, mayatima, wenye kudhulumiwa, wenye hali ya hofu, wenye kukimbia makazi yao, nchi zao na familia zao, na kuangalia yale yanayowezekana kufanywa na Dini za mbinguni kama njia za kurahisisha kuokoa hawa wenye matatizo, jambo lililonishangaza sana mimi ni kuwa yanayomhuzunisha na kumshughulisha Papa ni yale yale yanayonihuzunisha mimi na kunishughulisha yamekuwa ni yenye kuendana na kukubaliana, kila mmoja kati yetu alihisi uzito wa majukumu ambayo Mwenyezi Mungu Atatuuliza kwayo Siku ya Mwisho, rafiki yangu alikuwa ni mpole na kuumia sana na matatizo ya watu wote, pasi na kutofautisha wala kubagua.

Miongoni mwa tuliyokubaliana kwa pamoja ni kuwa:

Hakika Dini za mbinguni hazihusiki na zipo mbali kabisa na harakati pamoja na makundi yenye kubeba silaha ambayo hivi sasa yanaitwa ni makundi ya “Ugaidi” vyovyote itakavyokuwa Dini zao, Imami zao na Fikra zao, au wahanga wao au ardhi ambayo wanayoitumia kuendeshea uhalifu wao.. hawa ni wauaji na wamwagaji damu, ni wenye kumfanyia ubaya Mwenyezi Mungu na Ujumbe wake… viongozi wa Mashariki na Magharibi wanabeba majukumu na wanapaswa kusimama kwenye wajibu wao katika kuwafuatilia hawa wenye kufanya uadui na kupambana nao kwa nguvu zote, kulinda roho za watu, imani zao na ibada zao kutokana na uhalifu wao.

 Kama tulivyokubaliana kuwa Dini zimekubaliana juu ya uharamu wa kumwaga damu, na Mwenyezi Mungu kupitia Ujumbe wake wote Ameharamisha kuua nafsi: Alitangaza hilo Nabii Musa Amani iwe kwake katika wasia kumi aliyotoa kwenye Mlima wa Hurib eneo la Sinai na akasema: “Usiue! usizini! usiibe!”([1]), kisha akayasema Nabii Isa Amani iwe kwake juu ya Mlima katika Milima Mitakatifu karibu sana na eneo la Kafr Nahoum nchini Palestina “Katika hazina yake ya maadili matakatifu” ambayo hufahamika kama Mawaidha ya Mlima, alisisitiza sana Nabii Isa yale aliyokuja nayo Nabii Musa na akaongeza kwa kusema: “Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa: Usiue, na mtu akiua, itampasa hukumu, bali mimi nawaambieni: kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jahanamu”([2]), mwisho akaja Nabii Muhammad na kutangaza kwa watu akiwa juu ya Mlima wa Arafa kwenye hotuba yake ya mwisho ambayo inaitwa hotuba ya kuaga, alitangaza yale waliyotangaza ndugu zake Mitume waliomtangulia kisha akaongeza kwa kusema: “Enyi watu! Naapa kwa Mwenyezi Mungu sifahamu kama nitakutana tena nanyi baada ya siku hii ya leo, katika sehemu yangu hii, Mwenyezi Mungu Amemrehemu mtu aliyesikia maneno yangu ya leo na kuyaweka akilini…. Enyi watu! Hakika damu yenu, mali zenu, heshima zenu kwenu ni vitukufu kama vile utukufu wa siku yenu hii, ndani ya mji wenu huu, mtakutana na Mola wenu, na Atakuulizeni kuhusu matendo yenu.. Aliyopo hapa ayafikishe haya kwa asiyekuwepo”. Na alikuwa anasema mwenye kutenganisha kati ya mzazi wa kike na mwanawe basi Mwenyezi Mungu Atamtenganisha na watu wake wa karibu Siku ya Kiyama… na mwenye kumuashiria ndugu yake kwa kipande cha chuma, basi Malaika huwa wanamlaani, akiwa huyo ndugu yake ni kwa upande wa baba yake na mama yake.

Haya pamoja na makumi ya Aya za Qurani ambazo zinaharamisha kuua nafsi, na kutangaza kuwa mwenye kuua nafsi ya mtu mmoja ni sawa na aliyeua watu wote, na yule mwenye kunusuru nafsi moja basi ni sawa na amewanusuru watu wote..

Waheshimiwa mtaona hapa umoja wa maneno ya Mwenyezi Mungu na umoja wa maana zake, bali umoja wa majukwaa ambayo walitolea hotuba Manabii hawa Watukufu, nayo ni Mlima wa Tur eneo la Sinai nchini Misri, Mlima katika milima ya Palestina, na Mlima wa Arafa katika Mji wa Makka ndani ya Ghuba ya Kiarabu..

Kutokana na haya kuna uwazi mkubwa kuwa si sahihi yale yanayosemwa kuwa Dini ndiyo inayobeba ujumbe wa vita na ndiyo sababu kuu, na historia ni shahidi juu ya hilo ikiwa ni dalili ya wazi ya mapinduzi ya ustaarabu wa hivi sasa juu ya Dini na maadili yake, na kuiweka mbali na mambo ya jamii, baada ya uongo kwenda haraka - haraka ya moto kwenye kuunguza kuni - katika kujenga uelewa kwa watu na vijana, hasa nchi za Magharibi, uongo huo uliosimama nyuma ya kuenea miito ya kupinga Mungu, falsafa ya vitu vya kuonekana, madhehebu ya fujo na uhuru usio na mipaka, na kuipa nafasi elimu ya vitendo sehemu ya “Dini” na kulisimika hilo, baada ya kupita zaidi ya karne tatu za mapinduzi dhidi ya Mwenyezi Mungu na Dini za mbinguni ndipo likaja janga kubwa ambalo ni msiba kwa mwanadamu wa sasa hakuna anayeupinga isipokuwa ni yule anayejitukuza..

Ukweli ambao lazima kuueleza kwenye uongo huu ni kuwa, sababu ya kwanza ya matatizo ya ulimwengu wa hivi sasa ni kutokana na kukosekana kwa dhamira ya kibinadamu na kupotea kwa maadili ya Kidini, pamoja na mivutano kuchukua nafasi, kupenda mali, kupinga Mungu na falsafa tasa ambazo zimemwaminisha mwanadamu na kumdharau Mwenyezi Mungu na wale wenye kumwamini… na kucheza shere misingi mikuu mitakatifu ambayo ndiyo mdhibiti pekee wa kumtisha na kumnyenyekesha mwanadamu na kumwandaa utiifu mbwa mwitu anayeishi ndani yake..

Ama vita ambavyo vilipigwa kwa jina la “Dini” na kuuawa watu wengi chini ya bango hilo, hakuna Dini hazihusiki na hili, lakini wahusika ni aina hii ya siasa zisizo na mwelekeo ambazo zimetumia baadhi ya watu wa Dini na kuwaingiza kwenye malengo yasiyojulikana na Dini wala kuheshimiwa, sisi tunakubali kuwa kuna watu wa Dini wenye kuleta ufafanuzi wa maandiko matakatifu, ufafanunuzi wenye uharibifu, lakini sisi hatukubali kabisa kwamba kusoma Dini kwa kisomo kilicho safi hakiwezi kabisa kwa hawa waliopotea wenye kupotosha kunasibishwa kuwa wapo katika upande ulio sahihi kwenye Dini yoyote ile ya Mwenyezi Mungu, au kuwasamehe kwa hiana yao katika ufikishaji wao kwa watu kama vile Alivyoteremsha Mwenyezi Mungu.

Ukiukaji huu unaofanya kazi katika uelewa na ufahamu wa maandiko hauhusiki na maandiko ya Dini tu na kuyatumia kwa uadui dhidi ya watu, bali mara nyingi hutokea mfano wake katika nyanja ya kisiasa, pale yanaposomwa maandiko ya makubaliano ya kimataifa yenye jukumu la kulinda amani ya dunia usomaji maalumu unaohalalisha vita dhidi ya nchi zenye amani, na kuziharibu mbele ya wananchi wake, hakuna kizuizi baada ya siasa hizi kutekeleza matakwa yake ya uadui mbaya… hakuna kinachozuia kuomba radhi ya mayatima na wajane kwa kudai tu makadirio vimekosewa. Mfano wa hayo upo wazi kama uwazi wa jua la majira ya saa kumi jioni.

Kwa sababu hiyo tumetoa wito kwenye waraka huu “Kusimamisha matumizi ya Dini na madhehebu kuibua hali za chuki, matumizi ya nguvu, ubaguzi usio na macho, na kuzuia kutumia jina la Mwenyezi Mungu ili kuruhusu matendo ya mauaji, kusababisha watu kukimbia makazi yao na ugaidi, pia kuukumbusha ulimwengu wote kuwa Mwenyezi Mungu hakuumba watu ili kuja kuuawa au kuadhibiwa au kubanwa katika uhai wao na maisha yao.. Mwenyezi Mungu ni mwenye kujitosheleza kwa yule mwenye kulingania kuondoa roho za watu au kutishia wengine kwa jina lake Mola”.

Wageni Waalikwa

 Mimi nina hakika kuwa pendekezo hili muhimu na harakati nzuri zinazochukuliwa kuelekea kufikia undugu wa ubinadamu katika eneo letu la Kiarabu huenda litaleta matunda yake, kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu limeshaanza nchini Misri kwa nguvu kubwa ambapo ndani ya masiku machache yaliyopita umefunguliwa Msikiti Mkubwa na Kanisa kubwa yakiwa yapo jirani ndani ya Mji Mkuu mpya wa kiidara, ni hatua ya kihistoria kuelekea kuimarisha usamehevu na kusimika undugu kati ya Dini, kwa pendekezo la Mheshimiwa Rais Abdulfattah El-Sisi Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri.

Limebakia kwangu neno moja ninalielekeza kwa ndugu zangu Waislamu katika eneo la Mashariki, nalo ni kuwataka kuendelea kuwa nao ndugu zenu wananchi wenzenu Wakristo sehemu zote za nchi zenu, wao ni washiriki wenzetu ndani ya nchi, ni ndugu zetu ambao Qurani yetu Tukufu inatukumbusha kuwa wao ndio watu wenye upendo sana kwetu, na Qurani inaelezea sababu ya upendo huu kwa kauli yake: (Hayo ni kwa sababu wapo miongoni mwao makasisi na wamonaki, na kwa sababu wao hawafanyi kiburi){Maidah: 82}. Wakristo - Wakristo wote - nyoyo zao zimejaa heri, upole na huruma, Mwenyezi Mungu ndiye Aliyewafanyiwa mambo haya mazuri kwenye nyoyo zao.. haya yanaelezewa na Qurani kwenye kauli ya Mola Mtukufu ndani ya Surat Al-Hadid: (Na Tukamfuatisha Isa bin Mariamu, na Tukampa Injili. Na Tukajaalia katika nyoyo za waliomfuata upole na rehema){Al-Hadid: 27}.

Ni wajibu wetu sisi Waislamu kutosahau kuwa Ukristo uliubeba Uislamu pale Uislamu ulipokuwa mwanzoni kabisa, na kuupa nguvu kutokana na upotofu wa ibada za masanamu na shirki, ambayo ilikuwa inalenga kuuteka Uislamu mwanzoni mwake, pale Mtume alipotoa amri kwa Masahaba wake wanyonge ambao walikuwa ndio wengi pindi adhabu na kero za Makuraishi zilipozidi kwao na kuwaambia: “Ondokeni na nendeni Habasha kwa sababu huko kuna Mfalme asiyedhulumu mtu yeyote aliye pembezoni mwake”. Mfalme huyu Mkristo aliwapokea Waislamu ndani ya nchi yake ya Kikristo na kuwakirimu pamoja na kuwalinda kutokana na kero na maudhi ya Makuraishi, kisha akawarejesha mji wa Madina baada ya kuenea kwa Uislamu na kuimarika.

Neno lengine kwa ndugu zangu Wakristo eneo la Mashariki: Nyinyi ni sehemu ndani ya umma huu na nyinyi ni wananchi na wala sio walio wachache, ni mategemeo yangu mtaachana na utamaduni wa msamiati huu unaochukiza wa “walio wachache”, nyinyi ni wananchi wenye haki kamili na wajibu, na fahamuni kuwa umoja wetu ndio mwamba pekee ambao njama zote za kumtenganisha kati ya Mkristo na Mwislamu zinagonga hapo ambapo umefika wakati sasa wa kufanya juhudi zaidi kwani muda wa kuchuma matunda pamoja umefikia.  

Neno lango kwa wananchi Waislamu eneo la Magharibi ni kujichanganya katika jamii yenu mchanganyiko chanya, mkiwa wenye kulinda Dini yenu kama vile mnavyopaswa kulinda na kuheshimu sheria za jamii, fahamuni kuwa usalama wa jamii hii ni jukumu la kisharia, na amani ya kidini mtakayokuja ulizwa mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, ikiwa itakuja sheria inayowataka kwenda kinyume na Sharia yenu basi elekeeni kwenye mikondo ya sheria kwani sheria ndiyo yenye dhamana ya kurejesha haki kwenu na kulinda uhuru wenu.

Kama ninavyosema kuwaambia vijana wa Magharibi na Mashariki: Hakika mustakabali unaonekana kwenu, ni juu yenu kujipamba na maadili mema, elimu na maarifa, ni juu yenu kuufanya huu waraka ni katiba ya msingi wa maisha yenu, ufanyeni waraka huu kuwa ndiyo dhamana ya mustakabali usiokuwa na mvutano na machungu, ufanyeni waraka ni wenye kujenga mazuri na wenye kubomoa shari, ufanyeni waraka huu kuwa ndio mwisho wa chuki… wafundisheni watoto wenu waraka huu kwani wenyewe ni mwendelezo wa waraka wa Madina Al-Munawwarah, Mawaidha ya Mlima, wenyewe unatoa shime kubwa ya ushirika wa kibanadamu na misingi ya kimaadili.. nitafanya kazi na ndugu yangu Mtakatifu Papa, ndani ya kipindi chote kilichobakia cha umri, pamoja na kufanya kazi na watu wa Dini lengo ni kulinda jamii na utulivu wake, hapa ni lazima kupongeza Kongamano la Muungano wa Dini kwa Usalama wa Jamii, kongamano ambalo lilifanyika hapa Abu-Dhabi ndani ya mwezi wa Novemba iliyopita na kupata uungwaji mkono mkubwa na Al-Azhar Al-Sharif pamoja na Vatican, kongamano lililohudhuriwa na viongozi wengi wa Dini ili kusimamia majukumu yao kwa lengo la kulinda heshima ya mtoto.

Mwisho kabisa: Natoa shukurani nyingi kwa ndugu yangu Sheikh Muhammad bin Zayed kwa uwenyeji wake wa kikao hiki cha kihistoria na usimamizi wake wa “Waraka wa Undugu wa Kibinadamu” ambao tunategemea hapo baadaye kuwa na mchango mkubwa wa amani kwa wananchi wa nchi mbalimbali, na kuamsha hisia za upendo na kuheshimiana kati ya pande za Magharibi na Mashariki na pande za Kasikazini na Kusini.

Kama vile natanguliza shukrani kwa Sheikh Abdallah bin Zayed, na vijana wote ambao wamekesha katika kuratibu na kuandaa kazi za kikao hiki ili kifanyike kwa sura yenye heshima kubwa.

Kwa kuifanyia kazi kauli ya Mola Mtukufu: (Wala msiwapunje watu vitu vyao){Al-A’araf: 85}. Natanguliza shukrani zangu kwa askari wawili wasiofahamika ambao walikuwa nyuma ya maandalizi ya “Waraka wa Undugu wa Kibinadamu” tokea mwanzo wake mpaka kufikia ukamilifu wake hii leo katika tukio hili la kilimwengu, nao ni kipenzi wa Hakimu/ Muhammad Abdulsalaam – Mwanasheria wa zamani wa Sheikh Mkuu wa Al-Azhar, na baba wa Yoan Lahzy sekretari maalumu wa Mtakatifu Papa Francis, kwao na kwa kila aliyechangia kufanikisha kikao hiki natoa shukrani za dhati kwao.

 

Nawashukuru kwa usikivu mwema

 

Amani iwe kwenu na rehema za Mwenyezi Mungu na Baraka zake

 

Imamu Mkuu

Prof. Ahmad Al-Tayyib

Sheikh wa Al-Azhar

 

([1])  Kitabu cha Kutoka, Mlango wa 20: 13 - 15.

([2])  Mathayo 5: 21 – 22.

Print
10708 Rate this article:
1.0

Please login or register to post comments.

أقسم بالله العظيم أن أكون مخلصًا لديني ولمصر وللأزهر الشريف, وأن أراقب الله في أداء مهمتى بالمركز, مسخرًا علمي وخبرتى لنشر الدعوة الإسلامية, وأن أكون ملازمًا لوسطية الأزهر الشريف, ومحافظًا على قيمه وتقاليده, وأن أؤدي عملي بالأمانة والإخلاص, وأن ألتزم بما ورد في ميثاق العمل بالمركز, والله على ما أقول شهيد.