Uislamu ni dini ya Amani na Usalama

  • | Sunday, 30 June, 2019
Uislamu ni dini ya Amani na Usalama

     Uislamu – kimsingi - ni dini ya amani. Jina lake linatokana na neno la kiarabu “Silm” ambalo lina maana mbili: Ya kwanza ni “kujisalimisha kwa Allah”. ya pili ni “amani”.

Wakati wowote Waislamu wanapokutana, wanatumia maamkizi ya amani “As-Salaam Alaykum – Amani iwe juu yako” na huyo mtu mwingine anajibu kwa kusema “Waalaykum As-Salaam – juu yako iwe amani.”

Vile vile Swala za kila siku zinaanza kwa kumsifu Allah, na zinaishia kwa salam za amani kwa wote.

Dini ya Uislamu ina mitazamo inayofanana na dini nyingine za mbinguni kuhusu suala hili la amani na usalama. Neno hilo la amani limetajwa mara nyingi katika aya za Qur'ani tukufu. Mwenyezi Mungu Anasema: (Enyi mlioamini! Ingieni katika usalama nyote. Wala msifuate nyayo za She'tani; hakika yeye kwenu ni adui aliye wazi)

Ili amani ipatakane, Uislamu umeweka awamu tatu tofauti:

Ya kwanza: ni amani na usalama ndani ya nafsi, Watu wote wanatakiwa kutakasa nafsi zao na kuzipamba kwa uchamungu.

Ya pili: amani na usalama wa jamii, mtu baada ya kuisafisha nafsi yake, huwa ametengeneza mazingira mazuri kwa ajili ya muungano mpana zaidi wa kijamii na wanadamu wenzake.

Ya tatu: amani na usalama kwa wasio Waislamu, miongoni mwa misingi inayotawala jamii ya Kiislamu ni kuishi kwa amani na usalama na wasio Waislamu. Suala la kuishi kwa amani na usalama na wasio Waislamu limesisitizwa sana katika aya za Qur'ani Tukufu na Sunnah  ya Mtume (S.A.W)

La kusikitika sana katika siku hizi kuwa - licha ya juhudi kubwa zinazofanywa kwa ajili ya kulinda amani na usalama - kunashuhudiwa ongezeko la vita na machafuko katika pembe mbalimbali za dunia.

Hivyo suala la kujenga na kuimarisha amani na usalama na kuishi pamoja na wanadamu wote bila ya kujali dini, rangi, na tofauti zao nyingine ndio lengo la mwisho la Uislamu na wafuasi halisi wa dini hiyo.

Bila shaka yo yote kufuata mafundisho ya dini ya Uislamu kuhusu jamo hilo la amani kunaweza kuwaondoa wanadamu wote wa ulimwengu katika mapigano na migogoro ya dunia ya hivi sasa, kwani Uislamu ni dini ya amani na usalama.

Print
Categories: Makala
Tags:
Rate this article:
4.3

Please login or register to post comments.