Mchango wa Malezi Bora katika Kupambana na Fikra Kali

  • | Sunday, 18 July, 2021
Mchango wa Malezi Bora katika Kupambana na Fikra Kali


    Bkila shaka jamii yoyote inahitaji kuwa na misingi ya kuijenga na kuipa nguvu ya kuendelea duniani na kupambana na majanga na matatizo yanayoikumba. Misingi hiyo ni kama vile; malezi, mshikamano, umoja, uadilifu n.k., ingawa misingi hiyo yenyewe ni muhimu na ya lazima, lakini ipo misingi ambayo isingekuwepo na kuwa imara jamii yote yanaathirika vibaya bali huweza kuporomoka na kuharibika.
Malezi bora ni miongoni mwa misingi muhimu ya kuijenga jamii na kuikinga dhidi ya maovu ya kisasa, ambapo malezi ni: zoezi la kuunda mwenendo na tabia ya mtu kuanzia utotoni kwa mujibu wa vidhibiti na vyanzo maalumu kidini, kijamii, kiuchumi na kifikra.
Kupitia malezi, mtu anazoeleshwa mambo na kufahamishwa namna ya kupambanua lilio sahihi na lililo kosa, lililo heri na lililo shari. Kwa hiyo, wataalamu wa malezi wanazingatia kuwa malezi ni: kumwezesha mtu aishi katika mazingira yake kwa kumpa uwezo wa kuendana na yaliopo katika jamii yake.
Hivyo, tunaweza kusema kuwa malezi ni njia ya kuunda mtu mwenye uwezo wa kuingiliana na jamii yake na kuanza safari ya maisha yake, kuathiri na kuathiriwa, kuhakikisha mafanikio na kufeli wakati mwingine. Kwa maneno ya Aflaton: "Malezi ni jaribio la kuongeza sifa na vigezo kwa mwanadamu (kimwili na kiroho) mapambo na uzuri unaowezekana".
Pia, malezi kwa mtazamo wa Rifaa Al-Twahtawy ni: "lile zoezi la kujenga na kuunda tabia ya mtoto kutokana na hali ilivyo katika mazingira ya jamii iliyo bora na kukuza sifa na tabia njema ambazo zinamkinga kutoka kwa maovu na kumwezesha kujielezea na kujitambulisha".
Wengine wanaona kuwa malezi ni kumlea mtu mwenye mwili mzuri, tabia njema, fikra sahihi, mpenda nchi yake, anawajibikia majukumu yake na anayo maelezo na maarifa ya kutosha ya kuendesha maisha yake.

Mtazamo wa wataalamu wa kisasa kwa dhana ya malezi hauko mbali na dhana zilizoelezwa na wataalamu na wanavyuoni wa zamani, ambapo wengi wa wataalamu wa kisasa wameainisha malezi kwa kusema kuwa ni: "zoezi la kuingiliana na kufungamana kwa mtu na mazingira anakoishi" wengine wametoa maoni yao kuwa malezi ni: "kazi inayopangwa na kukusudiwa kwa ajili ya kumpa mtu maarifa, ujuzi na sifa za kumwezesha aende sambamba na jamii, pamoja na kumsaidia akabiliane na mabadiliko ya enzi na changamoto zake katika nyanja mbalimbali za maisha".
Kwa kweli, tukitaka kutaja dhana ya malezi kutokana na mitazamo mbalimbali tutatumia mistari bali kurasa kadhaa, kwa kuwa kutaja na kueleza dhana ya malezi si lengo kuu la makala hii, ila ni kianzio cha makala tu.
Kwa upande wa mtazamo wa Uislamu kwa malezi, kwa hakika dini ya kiislamu imetilia mkazo sana malezi na kuyafanya msingi muhimu wa kujenga familiya ambayo ni kiini cha jamii na nguzo yaken kuu.
Kwa mujibu wa sheria ya kiislamu malezi ya mtu yanakuwepo hata kabla yeye hajazaliwa kwani kuchagua mke na mume ni sehemu ya malezi na kwamba wanandoa wanatakiwa kushirikiana katika kuwalea watoto wao hata kabla hawajaoa.
Isitoshe, bali Qurani Tukufu na Sunna za Mtume (S.A.W.) zilikusanya maelekezo mengi kuhusu umuhimu wa malezi katika kujenga jamii imara yenye amani na utulivu na kusisitiza umuhimu wa kuwajibika kwa familiya kwa majukumu yake katika jamii kwa pande zote kidini na dunia. Kwa hiyo Qurani Takatifu imesisitiza umuhimu wa familia na malezi mema ikayafanya sababu ya kujiokoa kutoka madhara na maovu duniani na Akhera, Mwenyezi Mungu Amesema: {Enyi mlio amini! Jilindeni nafsi zenu na ahali zenu na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe. Wanausimamia Malaika wakali, wenye nguvu, hawamuasi Mwenyezi Mungu kwa anayo waamrisha, na wanatenda wanayoamrishwa} [66/6].
Pia, kwa mujibu wa sheria ya kiislamu familia inatakiwa kuelewa na kutambua namna bora inayofaa katika kuwalea watoto wake, maana kwa kuchunguza jambo hilo imeonekana kuwa kuna aina tatu za miamala ya familia na mifumo ya malezi ambazo ni pamoja na:
Mfumo wa kwanza: Miamala kali ambapo wazazi wanafuata mfumo wa kuwatishia watoto wao na kuwahofisha na pengine kuwapiga jambo linalosababisha watoto hawa wakosa imani na utulivu, ilhali wazazi wanadhani kuwa wanawatunza wanao ipasavyo huwa wanawafanyia uzembe mkubwa kwa kutowasikia na kuwanyima haki ya kujielezea kwa sababu ya miamala kali hii, hivyo watoto hawa wanapokua huwa hatari juu ya jamii nzima na huwa lengo rahisi kwa kushawishiwa kwa fikra kali na upotofu wa fikra.
Mfumo wa pili: Miamala laini mpaka kumpa mtoto kila analolitaka bila ya kujali linafaa au halifai, mfumo huu ambao ni mfumo wa "Mtoto wa Mama" unapelekea matatizo mengi kwa kupata kijana asiyeweza kutambua majukumu yake wala hawajibiki kwa wajibu yoyote kwani ameshazoea uzembe na kufanyiwa kila analolitaka bila ya kufanya juhudi hata kidogo.
Mfumo wa tatu: Miamala ya wastani ambayo iko kati kati bila ya kuwahofisha watoto wala kuwapa kila kitu bure, kwa mujibu wa mfumo huu familia inasifika kwa uwastani katika mambo yake yote, kwa hiyo inakuwa familia yenye michango mikubwa katika jamii yake na umma wake, na inasaidia sana katika kuzuia kuenea kwa fikra isiyo sawa na kupambana na misimamo mikali.
Kutokana na hayo tuliyoyataja, familia katika Uislamu inawajibika kutekeleza majukumu yake yaliyo muhimu sana kwa mfumo ulio sawa sawa bila ya upungufu wala ziada, hasa kuhusiana na malezi ya watoto ambao wanatarajiwa kuwa vijana wa kesho na viongozi wa baadaye kwa kutaka heri na mafanikio kwa jamii, nchi na umma wote kwa jumla.
Kwa kuangalia nafasi ya malezi katika Uislamu tunatambua kuwa malezi yana mchango mkubwa sana katika kupambana na fikra kali na kuwakinga vizazi wajao kutokana na fikra hizo, kwa kuwa malezi huwa kama kinga na ukuta wa kuzuia fikra hizo zisimfike mtoto au kijana na kumwezesha apambanue anayoyasikia na kuyagawa kwa fikra zinazokubalika na zile zisizofaa kwa mujibu wa misingi ya dini na mafundisho yake.
Kwa upande wake, Al-Azhar Al-Shareif kupitia taasisi zake mbalimbali zikiwemo shule, vyuo vya elimu, machapisho, mitandao na hata mawaidha ya moja kwa moja imefanya juhudi kubwa mno kwa ajili ya kuhakikisha kuzuia kuenea fikra kali katika viwango mbalimbali.

Miongoni mwa nyanja za kuzingatiwa katika jitihada za Al-Azhar Al-Shareif za kupambana na fikra kali ni kutoa na kuandaa mipango ya kuwakinga watoto kutokana na fikra kali kupitia mitalaa ya elimu inayofundishwa katika mashule na vyuo vya Al-Azhar Al-Shareif ambayo imechukua hatua kadhaa kwa lengo la kutoa mwangaza juu ya vyanzo vya fikra kali na namna ya kupambana nazo.
Juhudi hizo zimejumuisha kuanzisha Kituo cha Al-Azhar cha kupambana na fikra kali ambacho kinashughulikia kuchunguza mikakati ya makundi ya kigaidi na machimbuko ya fikra zao na kutoa majibu kuhusu upotofu wa fikra na madai hayo yakiwemo madai yanayowahusu watoto na kupinga kikali majaribio ya makundi ya kigaidi ya kuwalazimisha watoto na wanawake kujiunga nayo.
Pia, Al-Azhar Al-Shareif kupitia Kituo cha Kupambana na Fikra kali imeanzisha kampeni kadhaa za kupinga mipango ya makundi ya kigaidi kuhusu mafunzo au mafundisho wanayoyatoa magaidi kwa watoto na dhana potofu wanazozitoa kama vile; Mfumo wa utawala katika Uislamu (Hakimiyya), Walaa na Baraa, Jihad n.k. ambapo makongamano ya Al-Azhar ya kupambana na ugaidi na fikra kali pamoja na hotuba za Imamu Mkuu na wanavyuoni wa Al-Azhar kuhusu suala hilo ziko nyingi.
Kwa ufupi, ugaidi hutumia silaha nyingine nyingi mbali na mabunduki na mabomo na kwamba kuwalea vizazi wa magaidi wapya ni lengo kubwa la makundi ya kigaidi, jambo ambalo linatubidi kufanya juhudi kubwa zaidi katika uwanja wa malezi na elimu kwa ajili ya kuwakinga watoto na vijana wetu kutokana na hatari hiyo na majaribio haya machafu ya kuanzisha jeshi la wapiganaji waliojazwa kwa fikra potofu.
Kwa hakika mapambano dhidi ya ugaidi na fikra kali huanzia nyumbani, shuleni, msikitini kabla ya kugeuka yawe mapambano katika viwanja vya mapigano kwa kutumia silaha na majeshi.  
 

Print
Categories: Makala
Tags:
Rate this article:
3.3

Please login or register to post comments.