Dhana ya Hijra kati ya mtazamo wa sheria ya kiislamu na uelewa wa makundi ya kigaidi

  • | Sunday, 15 August, 2021
Dhana ya Hijra kati ya mtazamo wa sheria ya kiislamu na uelewa wa makundi ya kigaidi

 

 

Miongoni mwa dhana zinazotumika kinyume na ukweli wake na kuchafuliwa na makundi ya kigaidi dhana ya "Hijra" ambayo ina nafasi kubwa katika Uislamu, ambapo inaashiria tukio la kihistoria la kutangaza mageuzi makubwa kabisa katika dini ya kiislamu na kuanza awamu mpya katika historia ya kiislamu.

Hijra ya Mtume Mohammed (S.A.W.) ni tukio la kihistoria lililotenga enzi ya kujificha na kuwalingania watu kisiri siri na kufanyiwa matusi ya kila aina na kuanza enzi ya kutangaza dini na kuanzisha dola imara yenye nguzo za kujivunia na kuwa na nguvu ya kujitetea, pamoja na kupanua eneo la dola hili na kuwavuta umma mkubwa kujiunga na dini hiyo mpaka dini yenyewe ikawa na nguvu na imara.

 

  • Hijra katika sheria na historia ya kiislamu..tukio na dhana

Kwa hakika Hijra ya Mtume (S.A.W.) ni tukio la kihistoria lililo muhimu kabisa si kwa waislamu tu, bali kwa ulimwengu mzima. Tukio hilo limeleta mabadiliko makubwa makubwa na likapelekea maendeleo mengi kwa jamii ya kwanza ya kiislamu na hata jamii ya kimataifa nzima. Waislamu watakiwa kutafakuri sana mafunzo ya tukio hilo na kuangalia kwa makini taratibu alizozichukua Mtume (S.A.W) na msimamo wa maswahaba wake watukufu (R.A.) kumwunga mkono na kumsaidia kwa ajili ya kufanikisha Hijra kwa mujibu wa maamrisho ya Mwenyezi Mungu (S.W).

Lile tukio la Hijra limekusanya mafunzo mengi sana ambayo makala moja wala zaidi hazitoshi kuyaelezea. Lakini tunayoyataka kubainisha hapa ni baadhi tu kati ya mafunzo na mawaidha hizo. La kusikitisha mno kuwakuta waislamu wa siku hizi wakiwa mbali na mafunzo haya wakijiacha kwa dunia na shughuli zake nyingi na masuala ya kimada badala ya kuzingatia masuala ya kiroho ya kujielemisha.

Kijumla, Hijra ya Mtume (S.A.W.) japokuwa ilitukia tangu miaka 1440, lakini atakayetia maanani na kukumbuka yale mazingira ya tukio hilo na taratibu zake hatapata shida kutambua kuwa tukio kama hilo haliwezekani kupangwa na watu wa kawaida, bali watu waumini wenye nyoyo safi na roho zinazoelekea Mwenyezi Mungu na kumtii kabisa bila ya kumhofia yeyote isipokuwa Mola Mlezi peke yake.

Kwa kuangalia matukio yaliyojiri kupitia miaka 1440 hiyo, tunaweza kupata fikra kuu kuhusu historia ya kiislamu na kutambua kwamba historia hiyo ilishuhudia hali na viwango tofauti, ambapo historia hiyo ndefu kuanzia kuanzishwa kwa dola la kiislamu lililojengewa misingi ya amani, usawa, uadilifu na ushirikiano mwema na watu wote waislamu na wasio waislamu, ile historia imejaa mafunzo na mawaidha mengi mno ambayo tunatakiwa kujifunza na kuyaelewa sana.

Mafunzo tunayoyapata kutokana na historia ya kiislamu hatuna budi kuyafuata na kuyatekeleza tukitaka kufanikiwa maishani mwetu ya hapa duniani na ya baadaye Akhera. Lakini kwa bahati mbaya wengi wa waislamu wa siku hizi wakawa wanatafuta maadili na mafunzo mbali na historia hiyo takatifu wakishawishwa na maadui wa umma wanaodai kuwa matukio, mafunzo na maadili ya historia hayafai kutekelezwa na kufuatwa katika zama hiyo.

Ilhali, mwislamu akiangalia na kuchambua historia hiyo hupata ufumbuzi na masuluhisho kwa matatizo yake na changamoto zake zote. Kwa mfano; tukitaka kutatua tatizo la kufeli kufika malengo yetu inatutosha kutafakuri katika tukio la Hijra na namna Mtume (S.A.W.) alivyopanga mambo yake haya akimtegemea Mwenyezi Mungu (S.W.) akifanya juhudi zake zote kwa ajili ya kufika na kufanikiwa katika malengo aliyoyataka.

Kwa hiyo, tunaona kwamba kupanga na kujiandaa vizuri wakati wa kumtegemea Mwenyezi Mungu (S.W.) na kumtii ndiyo msingi muhimu wa kumsaidia mtu kufika malengo yake. Hilo ndilo funzo la kwanza kabisa tunalolipata kuelewa; kujiandaa vizuri na kuainisha malengo na kuweka mkakati unaofaa kutuwezesha kufika malengo hayo. Inatajwa hapa kuwa kumtegemea Mwenyezi Mungu na kutii maamrisho yake haipingi kujiandaa na kupanga, kwa kuwa tumeamrishwa kumtegemea Mwenyezi Mungu tukiwa na mipango na juhudi zinazotusaidia kufika malengo na matamanio yetu.

Na hiyo ndiyo aliyoisisitiza Mtume (S.A.W.) aliposema katika hadithi iliyopokelewa na Tirmidhiy kutoka Anas Bin Malik (R.A.) kwamba Mtume (S.A.W.) alijiwa siku moja na mtu akiwa na ngamia wake akasema: "Ewe Mtume! Ni nini vizuri zaidi?! Nimfunge yule ngamia wangu kisha niende nikimtegemea Mwenyezi Mungu Amlinda? au Nimwache bila ya kumfunga nikimtegemea Mwenyezi Mungu Amlinda? Basi Mtume akamwambia: "Umfunge ukimtegemea Mwenyezi Mungu kumlinda".  

Tukiangalia maana ya hadithi hii tunapata kufahamu hekima muhimu kabisa ndiyo ni kwamba mwislamu japokuwa anatakiwa kumtegemea na kumtii Mwenyezi Mungu (S.W.) lakini wakati huo huo anatakiwa kutafakuri na kujipanga vizuri ili apate mafanikio.

Hilo ndilo funzo la kwanza kabisa ambalo tunaweza kulipata kutokana na tukio la Hijra ya Mtume (S.A.W.) basi hatutakiwi kukaa bure tukisubiri mafanikio na maendeleo yashuke kutoka mbingu, bali tunatakiwa kujitahidi sana na kujiandaa na kuweka mkakati na mipango ya kutosha, ambapo kazi yoyote ikikosa kupangwa ikawa ghasia na ovyo tupu haitarajiwi kumalizika ipasavyo wala kuhakikisha malengo yoyote kabisa.

Kwa kweli tukitaka kuzungumzia mafunzo na maadili ya Hijra ya Mtume (S.A.W.) tutahitaji makumi ya makala. Ambapo mafunzo ya tukio la Hijra yapo mengi ambayo ni pamoja na kujiandaa ili kufikia malengo, kushirikiana vizuri, kuwa na mkakati, kumtii kiongozi, kumtegemea Mwenyezi Mungu, kutowatendea watu vibaya wala kutowafanyia khiyana hata wakiwa maadui, kushikamana vizuri, kumwamini kiongozi, kuchagua marafiki na wasaidizi, umuhimu wa mwanamke na roli yake kuendeleza umma, …. n.k.

 Lakini hapa tunatupa mwangaza tu baadhi ya mafunzo haya kwa lengo la kutoa fikra kwa kifupi tu kuhusu tukio hilo takatifu katika historia ya umma wa kiislamu. Kwa hakika waislamu wa siku hizi wana haja kubwa kutafakuri na kutambua yale mafunzo yatokanayo kutokana na historia yetu ndefu.

Kwa kulinganisha baina ya hali ya umma wa kiislamu hapo zamani na hali yake katika zama hizi inabainika kuwa kuna dharura kubwa kabisa kwa waislamu wote duniani nzima warejelea mafunzo ya historia na kupuuza madai mapotofu yenye kuituhumu historia ya kiislamu kwa tuhuma isiyohusiana na ukweli hata kidogo. Waislamu wanatakiwa kutambua sababu za kufanikiwa na kutukuka kwa umma wao wakiwa na hisia ya fahari kwa historia hiyo.

Pia, Hijra inatukumbusha umuhimu wa kuhifadhi umoja wetu na kwamba umma huu lazima uwe na mshikamano mzuri na kuachana na kutofautiana na kugombana, ambapo tukio hilo limesisitiza kuwa huu ndio umma mmoja haukubaliki kugawanyika wala kusambaratika kwa mataifa, madhehebu, makundi, Mwenyezi Mungu (S.W.) Amesema: {Kwa hakika huu umma wenu ni umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu Mlezi. Kwa hivyo niabuduni Mimi} Al-Anbiyaa: 92. Kweli huu ndio umma mmoja japokuwa kutofautiana kwa upande wa lugha, rangi, kabila, eneo na hata madhehebu, ambapo utambulisho wetu sote ni Uislamu.

Miongoni mwa ishara na dalili za umoja wa umma wetu hiyo historia na ile kalenda ya kiislamu ambayo tunaianza siku hizi, ile kalenda ambayo Khalifa Omar Bin Al-Khattab (R.A.) aliianza akaungwa mkono na maswahaba waheshimiwa, akaifungamanisha na tukio muhimu zaidi kuliko katika historia ya kiislamu ambalo ni tukio la Hijra ya Mtume (S.A.W.) wala hakuifungamanisha na tukio lolote jingine kama kuzaliwa kwake Mtume wala kifo chake wala kuanza wahyi kwa kuwa Hijra ndiyo tukio lililotangaza kuanzishwa dola la Uislamu na kuenea kwake na kuimarika kwa dini hiyo takatifu ardhini.

Kwa kweli, tukio la Hijra inawakumbusha waislamu ulimwenguni kote kuwa wakitaka mafanikio duniani na Akhera basi, hawana budi ila kushikamana na mafundisho ya dini kama walivyokuwa wahenga wema na waislamu wa mwanzo, na kwamba kushikamana na dini hiyo na kutoa mbali mizozo, mapigano, migongano ndilo suluhisho la pekee lenye kuleta ushindi na mafanikio na kinga dhidi ya maangamizi na madhara ambayo maadui wa umma wanajitahidi sana kuyasababisha kwa umma huu. Kwa hakika kugombana na kutofautiana ndiyo sababu ya kimsingi ya kusambaratika kwa umma na kupatwa na maangamizi mabaya tunayoyashuhudia siku hizi.

Tukumbuke na kutafakuri sana wasia wa Mwenyezi Mungu Aliposema: {Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msizozane mkaingiwa woga, na zikapotea nguvu zenu. Nasubirini. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanao subiri} Al-Anfal: 46, na kauli yake: {Kabla yenu zimepita nyendo nyingi; basi tembeeni katika ulimwengu muangalie vipi ulikuwa mwisho wa wanaokanusha} Al-Imran: 136.

Na Kauli yake Mwenyezi Mungu (S.W.) Akizungumzia tukio hilo la Hijra ya Mtume: {Ikiwa nyinyi hamtamnusuru Mtume, basi Mwenyezi Mungu alikwishamnusuru walipomtoa waliokufuru, naye ni wa pili katika wawili walipo kuwa katika pango, naye akamwambia sahibu yake: Usihuzunike! Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi. Mwenyezi Mungu akamteremshia utulivu wake, na akamuunga mkono kwa majeshi msiyoyaona, na akalifanya neno la waliokufuru kuwa chini, na Neno la Mwenyezi Mungu kuwa ndilo juu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye nguvu Mwenye hikima} Al-Tawbah: 40,

Kuhusu tukio hilo hilo na hali ya maswahaba wakati huo Mwenyezi Mungu (S.W.) Amesema: {Wale ambao wametolewa majumbani mwao pasipo haki, ila kwa kuwa wanasema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu! Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hawakingi watu kwa watu, basi hapana shaka zingali vunjwa nyumba za wat'awa, na makanisa, na masinagogi, na misikiti, ambamo ndani yake jina la Mwenyezi Mungu linatajwa kwa wingi. Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu humsaidia yule anayemsaidia Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mtukufu} Al-Hajj: 40

Na kuhusu adhabu inayowasubiri wale makafiri wa Makkah waliowalazimisha Mtume (S.A.W.) na maswahaba wake (R.A.) watoke wakiacha jamaa, makazi na mali zao, Mwenyezi Mungu (S.W.) Amesema: {Na miji mingapi iliyokuwa na nguvu zaidi kuliko mji wako huu uliokutoa; nao tuliwateketeza na wala hawakuwa wa kuwanusuru}

 

  • Wanayoyasema magaidi kuhusu Hijra:

Kama kawaida yao, makundi ya kigaidi yamezoea kubadilisha dhana na kupotosha maana na kugeuza ukweli kuwa batili na lililo sahihi liwe kosa na kinyume, kwa kutumia mbinu mbalimbali zinazokusudia kudanganya vijana na kuzishawishi akili zao.

Kuhusu dhana ya "Hijra" makundi ya kigaidi yanadai kuwa Hijra ni wajibu na faradhi juu ya kila mwislamu na kwamba Hijra hiyo huwa kwa nchi ya kiislamu ambayo kwa mtazamo wao ni ile nchi inayodhibitiwa nao wakishikilia kauli yake Mtume (S.A.W.): "Hakika Hijra haitakatika endapo makafiri wanapiganiwa" na kauli yake (S.A.W.) iliyopokelewa na Mua'wiya amesema: "Hakika Hijra haitakatika mpaka tawaba ikatike na tawaba haitakatika mpaka jua ikuche kutoka upande wa magharibi; yaani siku ya Qiyama".

Pia, wenye fikra hizo wanatumia Qurani kwa kuunga mkono mtazamo wao huu, ambapo wanadhani kuwa agizo la Mwenyezi Mungu (S.W.) kwa waja wake kuhama ni kwa ujumla na linajumuisha hali zote kwa mujibu wa kauli ya Mwenyezi Mungu (S.W.): {Hakika Malaika watawaambia wale ambao wamewafisha nao wamejidhulumu nafsi zao: Mlikuwa vipi? Watasema: Tulikuwa tunaonewa. Watawaambia: Kwani ardhi ya Mwenyezi Mungu haikuwa na wasaa wa kuhamia humo? Basi hao makaazi  yao ni Jahannamu, nayo ni marejeo mabaya kabisa} [Al-Nisaa: 97].

Aya nyingine ambayo inatumiwa na makundi ya kigaidi kwa ajili ya kuthibitisha uwajibu wa Hijra ni kauli yake Mwenyezi Mungu (S.W.): {Na mwenye kuhama katika Njia ya Mwenyezi Mungu atapata pengi duniani pa kukimbilia, na atapata wasaa. Na anaye toka nyumbani kwake kuhama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kisha yakamfika mauti njiani basi umethibiti ujira wake kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye maghufira na Mwenye kurehemu} [Al-Nisaa: 100].

Baada ya kutaja wanayoyadai makundi ya kigaidi khusu uwajibu wa Hijra na uelewa wao kwa dhana hiyo, inafaa sasa kutoa mwangaza na ufafanuzi kuhusu ukweli wa dhana hii na kubainisha upotoshaji unaokusudiwa na makundi hayo.

Kwa mujibu wa waliyoyataja wataalamu wa Al-Azhar Al-Shareif wakiongozwa na Imamu Mkuu Profesa Ahmed Al-Tayyib, uelewa wa makundi ya kigaidi kwa dhana hii ya Hijra ina dosari kubwa na huonyesha kuwa makundi haya hayana msingi imara wala hawana uelewa wa kutosha wa kutoa fatwa bila ya kuwa na dalili za kuthibitisha ukweli wa fatwa hii.

Vile vile, dalili wanazozitumia magaidi hao zinagongana na muktadha wa mada yenyewe na kuweka matini katika mazingira yasiyofanana na mada, ambapo Mwenyezi Mungu (S.W.) Ameruhusu Hijra kwa wale wanaoteseka katika makazi yao wakawa wanaogopea dini, heshima na mali zao kwa lengo la kufanikisha jamii iwe na amani ya kutosha kwa kutekeleza maagizo ya Mwenyezi Mungu yanayoongozwa na ibada.

Pasipo na amani na utulivu, mwanadamu hawezi kutekeleza wajibu zake wala hatakuwa na uwezo wa kutimiza haki za Mola wake kwa ibada, bali huwa katika woga na vitisho, kwa hiyo, Mwenyezi Mungu Alipotoa agizo hilo Alikusudia wale wanaoogopa kutoweza kutimiza haki za Mola wao kwa kukosa amani. Pamoja na hayo, baadhi ya wafasiri wa Qurani wamefafanua kuwa sababu ya kuteremka kwa aya ya: {Na mwenye kuhama katika Njia ya Mwenyezi Mungu atapata pengi duniani pa kukimbilia, na atapata wasaa. Na anayetoka nyumbani kwake kuhama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kisha yakamfika mauti njiani basi umethibiti ujira wake kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye maghfira na Mwenye kurehemu} [Al-Nisaa: 100] ni kwamba baada ya Hijra ya Mtume (S.A.W.) baadhi ya waislamu wakabaki humo humo Makkah wakawa wachache mno kulingana na idadi ya washirikina, hivyo Mwenyezi Mungu Akawaagiza waislamu hao kuhama na kujiunga na Mtume (S.A.W.) na maswahaba zake kule Al-Madinah.

Kutokana na mjadala huu inabainika kuwa dhana ya Hijra ina maana na matumizi tofauti na uelewa wa makundi ya kigaidi na kwamba makusudi ya Hijra katika sheria ya kiislamu ni kuhama kwa ajili ya kuinusuru dini na kujilinda kutokana na maafa na fitina kutoka ardhi isiyofaa kwenda ardhi au nchi inayo amani na utulivu wa kumwezesha mtu kukimu maisha yake katika mazingira mazuri.

Pia, madai ya kuhusisha nchi ya Hijra au nchi inayokusudiwa katika Hijra ni ile inayowakaribisha waislamu na kuwasaidia kutekeleza maagizo ya Mwenyezi Mungu na kuepukana na makatazo yake bila ya kuainisha ardhi maalumu wala nchi fulani kama walivyodai magaidi kuwa nchi inayodhibitiwa nao ndiyo nchi ya kuhamiwa au mwelekeo wa Hijra, jambo lisilo sawa wala halikubaliki hata kidogo.

 

 

 

 

 

Print
Categories: Makala
Tags:
Rate this article:
4.0

Please login or register to post comments.