Dalili za kuharamisha Ugaidi kwa sura zake zote

  • | Tuesday, 4 October, 2022
Dalili za kuharamisha Ugaidi kwa sura zake zote

     Uislamu ndiyo dini ya maumbile mazuri, rehema, amani na usalama, kwa hiyo waislamu wanatakiwa kuepukana na kitendo chochote kinacho pelekea kuvuruga hali ya jamii au kusababisha ghasia na fujo katika nchi. Pia, dini hiyo inawakataza wafuasi wake kutumia nguvu na kuwadhulumu wengine kwa sababu yoyote, bali hakika Uislamu uliharamisha uvamizi dhidi ya nafsi, heshima, mali kwa kisingizio chochote.
Vile vile, sheria ya kiislamu haikuzingatia kuharamisha uvamizi unaofanywa dhidi ya wengine tu, bali imeharamisha mtu kujisababisha madhara yoyote kwa hiyo kujiua kuliharamishwa na kukutazwa kikali katika sheria ya kiislamu, Mwenyezi Mungu (S.W.) Amesema: {Na toeni katika njia ya Mwenyezi Mungu, wala msijitie kwa mikono yenu katika maangamizo. Na fanyeniwema. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema} [2/195]. Naye Mtume (S.A.W.) alisisitiza hilo kwa kusema: “Yeyote aliyejiua kwa zana hufufuliwa siku ya Mwisho akiwa anashika zana hiyo na kuadhibiwa nayo motoni kwa milele”.
Kwa hakika, sheria ya kiislamu imekataza kikali uadui wa aina yoyote na kukataa sana kuwatishia watu pasipo na haki, ikawatahadharisha waislamu kutoka athari mbaya za uadui na kuwatishia wengine hata ikiwa kwa lengo la mzaha tu. Imesimuliwa kutoka kwa Amer bin Rabiaa (R.A.): “Kwamba mmoja wa waislamu enzi ya Mtume (S.A.W.) amechukua viatu vya mwenzake kwa njia ya mzaha, Mtume aliposikia hayo akamlaumu sana akasema: Msimtishie mwislamu, kwani kumtishia mwislamu ni dhuluma kubwa”.
Kwa kuwa sheria ya kiislamu inahimiza ushirikiano na kuimarisha mahusiano ya kijamii baina ya watu wote japokuwa kutofuatiana katika mambo kadhaa kama dini, rangi, lugha, kikabila n.k. sheria hiyo imetangaza katika matini kadhaa za Qurani na Sunna kuwa dini hiyo inawataka wafuasi wake, bali walimwengu wote washirikiane katika mazuri na manufaa ya umma na kuepukana na uadui kwa namna zake zote, kama Alivyoeleza Mwenyezi Mungu katika kauli yake: {Na saidianeni katika wema na uchamngu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu} [5/2].
Pia, Uislamu ulisisitiza uharamu wa damu ya mwanadamu yeyote pasipo na haki ukakataza kumuua mwanadamu ambaye hakumuua wala hakufanya dhambi ya kumfanya astahiki adhabu ya kifo, Mwenyezi Mungu (S.W.) Amesema: {Wala msiuwe nafsi ambayo Mwenyezi Mungu amekataza isipo kuwa kwa haki. Na aliye uliwa kwa kudhulumiwa basi tumempa madaraka mrithi wake. Lakini asipite mpaka katika kuuwa. Kwani yeye anasaidiwa} [17/33].
Mtume (S.A.W.) amebainisha sababu za kumhukumia mwislamu adhabu ya kifo katika hadithi yake isemwayo: “Hairuhusiwi kumuua mwislamu anayekiri kuwa hakuna Mungu Anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba mimi ndiye Mtume wa Mwenyezi Mungu ila kwa sababu mojawapo sababu zifuatazo: mzinifu aliyeshaoa, aliyemuua mtu pasipo na haki, aliyeritadi na kuachana na jamma ya waumini”.
Vile vile, sheria ya kiislamu imeshadidisha adhabu ya mauaji na uadui kwa jumla ikafanya anayemuua mtu mmoja ni kama aliyewaua watu wote, maana inayoelezwa katika kauli yake Mwenyezi Mungu (S.W.): {Kwa sababu ya hayo tuliwaandikia Wana wa Israili ya kwamba aliye muuwa mtu bila ya yeye kuuwa, au kufanya uchafuzi katika nchi, basi ni kama amewauwa watu wote. Na mwenye kumuokoa mtu na mauti ni kama amewaokoa watu wote. Na hakika waliwajia Mitume wetu na hoja zilizo wazi. Kisha wengi katika wao baada ya haya wakawa waharibifu katika nchi} [5/32].
Isitoshe, bali Mwenyezi Mungu Amewaandalia wanaosababisha vitisho na hofu kwa watu wasio na hatia adhabu kali mno kwa kuwa Amewaweka katika kundi la wanaopigania vita dhidi ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wanaeneza ufisadi na uharibifu katika nchi, Mwenyezi Mungu (S.W.) Amesema: {Basi malipo ya wale wanao mpiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakawania kufanya uchafuzi katika nchi, ni kuuwawa, au kusalibiwa, au kukatwa mikono yao na miguu yao kwa mabadilisho, au kutolewa nchi. Hii ndiyo hizaya yao katika dunia; na katika Akhera watapata adhabu kubwa} [5/33].
Kwa jumla, dalili za kuharamisha ugaidi na kuwatishia watu na kuvuruga amani na utulivu wa nchi ziko nyingi sana katika Qurani Takatifu na Sunna za Mtume (S.A.W.), lakini hapa si mazingira ya kusimulia dalili na kutaja matini zinazounga mkono sheria ya kiislamu kuhusu suala hilo, bali la kuzingatiwa zaidi kutambua kuwa dini ambayo ina dalili hizo zote za kukataza vurugu na ukatili haiwezekani kuwa ni hiyo hiyo dini ya kueneza magombano na mapigano wala kuwa dini ya kuwalazimisha watu kujiunga nayo bali ukweli ni kwamba dini hii ni dini ya amani na usalama.
Madai ya kuwa magaidi wanatekeleza maamrisho ya dini hiyo au wanafanya jinai hizo kwa ajili ya kupata radhi ya Mwenyezi Mungu na kusimamisha sheria au kuhuisha dola la kiislamu na ukhalifa wake, ni madai matupu hayana usahihi wowote na ni rahisi kwa yeyote anayetaka kuhikisha kuwa dini hii haihusiani na maovu haya yote kuelewa hivyo kwa kutumia akili na dalili.

Kwa hiyo, Kituo cha Al-Azhar cha kupambana na fikra kali kinatoa wito wa kupambana na aina zote za fikra hizo kwa njia mbalimbali za kuwaepusha vijana wetu kuvutwa na makundi ya kigaidi au kushawashika na fikra potovu za makundi haya.


 

Print
Categories: Makala
Tags:
Rate this article:
2.5

Please login or register to post comments.