Utukufu wa Damu, Mali na Heshima katika Uislamu

Imeandaliwa na; Dkt. Alaa Salah Abdulwahed

  • | Monday, 23 October, 2023
Utukufu wa Damu, Mali na Heshima katika Uislamu

     Kila tunapoangalia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii tunaona picha na habari za mauaji na ukatili katika maeneo tofauti tofauti duniani, watoto hukatwa miili, kukosa wazazi na ndugu, kutishwa vibaya kwa namna isiyohusiana na dini wala ubinadamu hata kidogo.

Miongoni mwa mambo aliyoyasisitiza Mtume (S.A.W.) katika Hijja yake ya Mwisho kuhifadhi damu, mali na heshima na kuhakikisha kuwa kuhifadhi haya mambo kunatakiwa kuzingatiwa sana katika maisha ya kila mwislamu. Mtume ametambua umuhimu wa haya mambo na utukufu wake kwa kila mwanadamu ambapo mtu yeyote hawezi kuishi wala kuendelea katika maisha yake akikosa amani na matumaini kuhusu damu yake au mali au heshima.

Mtume (S.A.W.) alisimama akihotubia waumini, bali wanadamu wote kwenye siku ya Arafa katika Hijja ya Kuaga, ambapo alitoa maneno mazito ya kusisitiza namna ya kuishi baina ya wanadamu kwa amani na utulivu, siyo hiyo tu bali aliwaelezea walimwengu wote namna ya kuishi kwa amani pamoja na wanyama pia.

Katika hotuba hiyo Mtume Mohammed (S.A.W.) alitoa mawaidha makubwa kwa watu wake. Sentensi ya kwanza tu aliondosha mbele yake yote waliyokuwa nayo Waislamu kama vile unyang’anyi, uizi, kulipiza kisasi, na umwagaji wa damu, na paragrafu ya mwisho alisisitiza usawa kati ya muumini wa Kihebeshi na Khalifa wa Waislamu. Kwa hakika aliweka msingi mkubwa Ulimwenguni kwa ajili ya kuamiliana kwa uadilifu na ukarimu.

sheria ya kiislamu imebainisha kuwa miongoni mwa madhambi makubwa zaidi kumwua mtu pasipo na haki, kwani nafsi hii ni miliki ya Mwenyezi Mungu na Yeye ndiye Anaye haki ya kuamua hatima yake, Mwenyezi Mungu (S.W.) Alibainisha kuwa kumuuwa mtu haiwi ila kwa kukosea ambapo Amesema: {Na haiwi Muumini kumuuwa Muumini ila kwa kukosea.Na mwenye kumuuwa Muumini kwa kukosea basi amkomboe mtumwa aliye Muumini, na atoe diya kuwapa jamaa za maiti, isipo kuwa waache wenyewe kuwa ni sadaka. Na akiwa ni jamaa wa maadui zenu, hali yeye ni Muumini,basi ni kumkomboa mtumwa aliye Muumini. Na akiwa ni miongoni wa watu ambao pana ahadi baina yenu na wao basi wapewe diya watu wake na akombolewe mtumwa Muumini. Na asiye pata, basi afunge miezi miwili mfululizo, kuwa ni toba kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mwenye hikima} [4/92].

Na baada ya kubainisha hukumu ya kumuuwa mtu kwa kukosea, Mwenyezi Mungu Ameelezea kuwa kumuuwa mtu kwa makusudi ni dhambi kubwa na hatia isiyokubalika inayostahiki adhabu kali na husababisha ghadhabu ya Mwenyezi Mungu: {Na mwenye kumuuwa Muumini kwa kukusudia, basimalipo yake ni Jahannamu humo atadumu, na MwenyeziMungu amemkasirikia, na amemlaani, na amemuandaliaadhabu kubwa} [4/93]. Naye Mtume (S.A.W.) siku moja alikuwa anashika pazia za Ka’aba akisema: “Naapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa utukufu na uharamu wa damu, mali na heshima za mwislamu ni kubwa na muhimu mbele ya Mwenyezi Mungu zaidi kuliko Ka’aba hii”.

La kushangaza kuwa sheria ya kiislamu haikuhusisha hukumu hii kwa mwislamu tu, bali kwa wanadamu wote bila ya kujali dini, imani zao, kwa hiyo tunaona kuwa aya ya kwanza ya kubainisha hukumu ya mtu na adhabu yake akimuuwa mwingine kwa kukosea ilieleza aina mbalimbali za adhabu au fidya kulingana na hali ya mtu aliyeuawa. Pia, sheria ya kiislamu kupitia matini za Qurani na Sunna za Mtume (S.A.W.) kuwa hukumu ya kuharamisha uadui dhidi na dhuluma baina ya watu ni kwa watu kwa jumla si kwa waislamu peke yao, maana mwislamu haruhusiwi kumfanyia mtu yeyote uadui wala madhara na kwamba matini hizo zote zilikuwa zinazungumzia watu kwa jumla.

Isitoshe, bali zimekuja baadhi ya matini kusisitizia haki ya wasio waislamu kuishi kwa amani bila ya kuwa na woga wala wasi wasi kuhusu nafsi zao wala mali zao, kama vile hadithi ya Mtume (S.A.W.): “Yeyote atakaemwua mwenye ahadi basi hatanusa harufu ya pepo, hakika harufu ya pepo hunuswa kwa umbali wa miaka arobaini”.

Na tukiangalia hukumu ya kuibora mali ya mtu asie mwislamu tunatambua kuwa Mwenyezi Mungu Amemwumba mwanadamu akiwa na maumbile ya kupenda mali na anasa za dunia kama Alivyosema (S.W.): {Mali na wana ni pambo la maisha ya dunia. Na mema yanayo bakia ni bora mbele ya Mola wako Mlezi kwa malipo, na bora kwa matumaini} [18/46].(S.A.W.) alisema: “Hakika kitu kilicho bora zaidi kwa mtu mwema ni mali bora”, kwa hiyo, sheria ya kiislamu iliharamisha uporaji na ufisadi kwa mali za watu na kuweka adhabu kali mno kwa mwenye kuwafanyia watu dhuluma katika mali zao kwa mujibu wa Aliyoyasema Mwenyezi Mungu: {Na mwizi mwanamume na mwizi mwanamke, ikateni mikono yao, hayo ni malipo ya waliyo yachuma, ndiyo adhabu ya mfano itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima} [5/38].

Ama kuhusu heshima ya mtu, sheria ya kiislamu imesisitiza pia kuwa heshima ya mtu inatakiwa kuzingatiwa kwa kuwa ni kiumbe wa Mwenyezi Mungu aliyetukuzwa zaidi kuliko viumbe vingine kwa mujibu wa kauli yake Mwenyezi Mungu (S.W.): {Na hakika tumewatukuza wanaadamu, na tumewapa vyakupanda nchi kavu na baharini, na tumewaruzuku vituvizuri vizuri, na tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tulio waumba} [17/70].

Kijumla, sheria ya kiislamu imeweka misingi ya amani kupitia kusisitiza mambo muhimu yanayotakiwa kuzingatiwa ambayo yanajulikana kwa makuu matano nayo ni: kuhifadhi nafsi, dini, mali, heshima na akili. Tukiangalia mamabo haya matano tunaweza kutambua kuwa kuhifadhi haya matano ndiyo kuhifadhi maisha na jamii kwa jumla kutokana na maovu, madhara na maangamizi. Pia, haya makuu matano hayakuhusishwa kwa waislamu tu, bali kwa mujibu wa usamehevu wa dini hiyo yanatakiwa kuwepo kwa wanadamu wote bila ya kujali hitilafu yoyote.

Kwa hakika, jinai za mauaji wa kimbari zinazotekelezwa dhidi ya wasio na hatia katika maeneo mbalimbali duniani, ni dalili wazi ya kwamba ubinadamu uko hatarini, na kwamba roho za watu zikawa jambo la kupuuzwa kwa bahati mbaya zikilinganishwa na maslahi za kisiasa na mipango ya kupitisha utawala na udhibiti wa pande maalumu. Hatari hiyo haiwapati wahanga peke yao, bali ni mfululizo wa matukio na maangamizi, ambapo vita haitambui mshindi wa kudumu wala mshindwa wa kudumu, jambo la kuhuzunisha zaidi ni kuwa hisia za huruma, rehema na upole zinaathirika vibaya kwa hali ya mambo zikaja hisia za ukatili, chuki na unyanyasaji badala yake. Hali ambayo inatoa tahadhari kutoka mustakbali mbaya zaidi kuliko hali tuliyo nayo siku hizi zilizojaa vurugu, ukandamazaji na maangamizi.    

 

Print
Categories: Makala
Tags:
Rate this article:
No rating

Please login or register to post comments.