Mfarakano ndio Msinig wa Kudhoofisha Umma

Imeandaliwa na Dokta; Alaa Salah Abdulwahed

 • | Tuesday, 31 October, 2023
Mfarakano ndio Msinig wa Kudhoofisha Umma

     Kwa hakika, kutofautiana ni umbile lililopitishwa na Mwenye Mungu (S.W.) katika ulimwengu, na hekima mojawapo hekima za dunia, ambapo kutofautiana kwa viwango vyake vyote ni jambo la lazima maishani ambalo haiwezekani kutolewa mbali au kupuuzwa. Matini nyingi na misemo mingi ilisemwa kubainisha misingi na nguzo za kutofautiana na kueleza namna ya kunufaika kutoka hali hii iwe sababu ya kukamilishana wala siyo sababu ya kuzozana, zaidi ya kubainisha namna ya kugeuza tofauti zilizopo baina ya watu ziwe misingi ya maendeleo na ustawi kivitendo. La kushangaza kwamba baadhi ya makundi ya waislamu wanaojitokeza mara kwa mara wakiikana faida ya kutofautiana na hekima yake, na kuizingatia hali hii kama ni sifa mbaya na maouvu, isitoshe bali wanatangaza vita dhidi ya wanaotofautiana nao kwa madai ya kwamba kutofautiana ndiko sababu ya kutosha ya kupigana na kuuana, wakiathiriwa na mambo mengi kama vile; kutofahamu matini zinazotoa maelezo kuhusu kutofautiana na misingi yake, au kuzitumia matini hizo kinyume na makusudi yake na kadhalika. Mikondo hiyo ilikuwa na ingali chanzo kikubwa cha hatari kwa ummah wa kiislamu, kwani inafuata na kueneza fikra na itikadi zinazochangia kuwasha fitina na mapigano baina ya watu kwa jumla na waislamu hasa hasa, licha ya kuwazuia wengine kupata haki zao kujielezea na kuwa na uhuru wa kimaumbile.

Kwa kutazama hali yetu ya kisasa, wapo watu ambao hawafanyi chochote ila kusababisha mizozo na mapishano tu, hawakubali kabisa kubadilisha maoni yao hata wakielewa kwamba wamekosa, bali wanawataka wengine wawafuate katika maoni yao haya, maana wanadhani kwamba wapo sawa wakati wote, ilhali wengine wanaotofautiana nao wana maoni makosa wakati wote, basi baadhi yao hujadili kuhusu maneno aliyoyaweka katika mazingira isiyo yake akahitilafiana na wengine, akawa anataka awalazimishe wengine wafuate maoni yake, na baadhi yao wanashutumu kuwa na upendeleo kwa madhehebu maalumu, ilhali yeye mwenyewe anaanzisha madhehebu mpya isiyoafikiana na makubaliano ya umma, na wapo wengine wanaokataza kufuata maoni ya wengine wakati huo huo huwaomba watu wamfuate na kumwiga, mbali na wanaotangaza vita kwa ajili ya masuala yasiyo ya msingi yaliyokuwa sababu ya hitilafu baina ya Salaf na masuala mengine yanayofanana na hayo lakini hali hii haikusababisha Salaf hao kuzozana au kupigana. Kwa kweli sababu kuu ya kuzozana baina ya baadhi ya watu ni kutokuwa na ufahamu kwa ujumla na kukosa uelewa wa Fiqhi ya kutofautiana hasa hasa, kwa hiyo umma unahitaji sana uelewa wa aina hii zaidi kuliko wakati wowote mwingine.

Misingi inayojenga ufahamu wa kiislamu kuhusu hitilafu katika kiwangu cha kibinadamu:

 1. Kwamba kutofautiana ni kanuni thabiti na umbile la viumbe, kwa hivyo ni hali hiyo hiyo kwa waislamu katika aghalabu ya mambo ya maisha yao.
 2. Kwamba kutofautiana kunagawanyika katika aina mbili:
 • Aina mbaya: ambayo inatokana na matamanio matupu na maoni yasiyo na elimu wala dalili.
 • Aina nzuri: ambayo inatokana na jitihada sahihi kwa viwangu vyake vyote.
 1.  Kwamba kuna baadhi ya masuala yasiyokubali kutofautiana na masuala mengine yanakubali, na yale masuala yasiyokubali kutofautiana ndiyo masuala yanayohusiana na hukumu thabiti zisizo na machaguo, na kila lililothibitishwa katika dini na kutambulika kwa dalili thabiti lisilo na maoni mbali mbali, bali rai moja tu, ama masuala yasiyokuwa hivyo, basi huwa maudhui ya jitihada, uchunguzi na kutofautiana kuhusu masuala kama hayo ni jambo zuri.
 2. Kwamba waislamu wote wanapaswa kufanya jitihada kwa ajili ya haki kila mmoja kadri anavyoweza, na jitihada kwa wataalamu wa fiqhi wanao mamlaka ya kutoa hukumu za kifiqhi ama iwe jitihada kamili au jitihada ya kusistiza hukumu maalumu au jitihada isiyo kamili; lakini kwa wale wasio na elimu na mamlaka ya kutoa hukumu za kifiqhi basi jitihada yao huhusishwa na kuchagua mtaalamu wa fiqhi anaetakiwa kufuatwa, kwa hiyo inabidi kutofautisha baina ya masuala ya hitilafu na masuala ya jitihada, ambapo masuala ya hitilafu siyo yale yale masuala ya jitihada, bali mengi ya masuala ya hitilafu yamezuka pasipo na msingi wa elimu wala dali, bali matamanio au kuigiza tu.
 3. Kwamba kufanya juhudi kwa ajili ya kuomba haki si sharti kupelekea kutambua haki au hukumu sahihi wakati wote, huenda mtu afanye juhudi kubwa za kutaka kutambua haki na ukweli lakini mwishoni hafanaikiwi kwa hekima isiyojulikana ila kwa Mwenyezi Mungu pekee.
 4. Kwamba hitilafu baina ya waislamu katika masuala yanayokubali kutofautiana kuhusu hukumu yake ni mtihani kwa waislamu hao kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine ni rehema kwao, maana ni mtihani wa kuwaelekeza kwenye maarifa na mafunzo ya maisha, na rehema kwa kutowaadhibu kwa kukosa kuhusu jitihada yao katika masuala kama haya, na kuwapa nafasi ya kujifarajisha siyo kujibanabana.

Mambo yanayopaswa juu ya Mwislamu kwa ndugu yake Mwislamu kuhusu masuala ya hitilafu:

 1. Kufahamu kuwa jitihada ya kutambua na kufafanua haki ni jambo la lazima (lililofaradhishwa) juu ya kila mwislamu kulingana na uwezo wake, na kwa mujibu wa mamlaka yake ya kutoa hukumu kwa kutegemea jitihada kwa ujumla.
 2. Kutambua kuwa mwenye kufanya jitihada (Mujtahid) anapaswa kufuata hukumu aliyoipata kutokana na jitihada yake hata akitofautiana na wengine katika hukumu hiyo.
 3. Kufahamu kuwa haijuzu kukataza wala kukana hukumu ya mwislamu mmoja aliyefuata vidhibiti vya jitihada akatoa hukumu katika suala mojawapo masuala yanayokubalika kufanyiwa jitihada, madamu suala hilo inakubali kutofautiana hukumu yake, japokuwa likiwa kosa lake ni dhahiri, kwani kukosa katika jitihada siyo sababu ya kumtuhumu mtu na kumshutumu ufasiki au ukafiri, kwa dalili ya aya nyingi kama vile kauli ya Mwenyezi Mungu (S.W.): "Wala si lawama juu yenu kwa mlivyokosea. Lakini ipo lawama katika yale ziliyofanya nyoyo zenu kwa makusudi".
 4. Kutambua kwamba kuwahukumia waislamu kunatokana na hali yao ya nje tu, ama nia zao na nyoyo zao, basi ni kwa Mwenyezi Mungu peke yake, kwani yeye ndiye pekee Anaejua yaliyomo ndani yake.

Mwishoni:

Kwa hakika miongoni mwa misingi na vidhibiti vya fiqhi ya kutofautiana kulazimika kwa adabu za kiislamu zinazopaswa kuhusu mijadala na mazungumzo, wala sio mubalagha tukisema kuwa hali ya kuzozana na kusambaratika kwa waislamu mara nyingi huwa kwa sababu ya kutolazimika kwa masharti, misingi na vidhibiti hivyo vya majadiliano, na kwamba maendeleo ya waislamu katika siku zijazo yanategemea sana uwezo wao kuendesha na kudhibiti hitilafu zao kwa mujibu wa adabu na misingi iliyopitishwa na Uislamu.

Enyi Ndugu Waislamu! tunaweza kujiuliza swali muhimu nalo ni: kwa nini umma na mataifa mengine wanafanya juhudi kubwa za kutuvuta kwenye vita na mizozo? Kwa sababu gani wanaungana dhidi yetu, ilhali sisi hatuwezi kuwa na msimamo mmoja kuhusu masuala muhimu na maamuzi ya msingi? Kwa nini hatuwajibikie maagizo na mafunzo ya Mwenyezi Mungu kuungana na kusaidiana?!

Bila shaka, hali mbaya tuliyo nayo ni kwa sababu ya kudhoofika kwa umma na kusambaratika kwa vijana na mataifa wake, tunatakiwa kuwa jasiri na wenye ushujaa mkubwa zaidi kupambana na mateso ya maisha na kuinusuru dini yetu na kuwaokoa ndugu zetu katika kila pembe duniani.

   

Print
Categories: Makala
Tags:
Rate this article:
No rating

Please login or register to post comments.