Kukataa vurugu na uadui ni Msingi wa Kiislamu na Maumbile ya Kibinadamu

Imeandaliwa na Dkt.; Alaa Salah Abdulwahed

  • | Monday, 13 November, 2023
Kukataa vurugu na uadui ni Msingi wa Kiislamu na Maumbile ya Kibinadamu

     Kwa hakika dini ya Uislamu ni dini ya usamehevu, wepesi na msamaha ambayo mafunzo yake yote yanachangia kwa kiasi kikubwa katika kueneza utamaduni wa kusameheana na kuvumiliana baina ya wanadamu wote.

Mwenyezi Mungu (S.W.) Ametwamrisha kwa kulazimika kwa usamehevu katika mambo na miamala yetu yote, ambapo Mwenyezi Mungu Alisema Akimwelekeza Mtume wake (S.A.W.): {Shikamana na kusamehe, na amrisha mema, na jitenge na majaahili} Al-Araaf: 199.

Naye Mtume (S.A.W.) alipoteremshiwa aya hiyo alimwuliza Jebrili (A.S.): “Ewe Jebrili ni nini maana ya maneno haya?” Akamjibu: “Ni kwamba Mwenyezi Mungu Anakuamrisha kumsamehe aliyekudhulumu na kumpa aliyekunyima na kuwasiliana na aliyekupuuza”.

Pia, Mtume (S.A.W.) alisema: “Kwa hakika asiye na huruma na usamehevu ni ndiye aliyenyimwa upole na heri”

Miongoni mambo ya msingi ambayo tunatakiwa kuwajibika nayo ni kusameheana na kuvumiliana kwa kuwa sifa hiyo inasaidia kuenea amani na utulivu na kuepukana na ugomvi na migogoro, kwa kuangalia matatizo mbalimbali ya enzi ya kisasa tunatambua kwamba mengi ya majanga ya dunia yetu yametokana na kutokuwa na sifa hiyo ambayo ni sifa mojawapo sifa kuu za dini ya kiislamu. Mwislamu anatakiwa kuwa msamehefu katika hali zake zote na pamoja na watu wote, siyo hivyo tu, bali pamoja na wanyama pia kwani ni balozi wa amani na utulivu kwa jamii yake.

Kwa kweli, Uislamu ndiyo dini ya usamehevu, upendo na tabia njema. Usamehevu ni mojawapo tabia takatifu zilizosisitizwa na Uislamu ambao ni umbile lililopitishwa na Mwenyezi Mungu kuanzia mwanzo wa uumbaji mpaka siku ya mwisho. Mwenyezi Mungu Ameumba mbingu na ardhi, akaumba viumbe vya kila sura na aina, akawatukuza wanadamu na kuwatumia Manabii na Mitume kuwaongoza kwenye njia yake iliyonyooka. Ujumbe wa mbinu kwa Manabii na Mitume wote ulikuwa unajulikana kwa jina la "Hanifiyya Samhaa" jambo linalothibitisha kuwa usamehevu ni msingi muhimu wa jumbe za Mitume wote (A.S.), kwa hiyo, usamehevu, husiano nzuri na upendo huwa sifa kuu za wito wa Manabii na Mitume wote.

Mtume wetu (S.A.W.) ambaye ni Mtume wa mwisho alikuja kukamilisha na kufikisha ujumbe huo huo, bali zaidi ya hayo, kusisitiza kuwa sifa hizo na misingi hiyo hazihusishwi na waislamu tu bali ni misingi ya miamala na watu wote waislamu na wasio waislamu, kwa ajili ya kutimiza maadili ya kibinadamu na kukuza ushirikiano wa kistaarabu. Mwenyezi Mungu (S.W.) Amebainisha kwamba wasilamu wanatakiwa kutendeana na watu wote kwa mujibu wa misingi hiyo ya msamaha na uadilifu Aliposema: {Mwenyezi Mungu hakukatazini kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawakukupigeni vita, wala hawakukutoeni makwenu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao uadilifu} [Al-Mumtahinah: 8].

Kwa kuangalia kwa makini aya hii, tunafahamu kuwa Mwenyezi Mungu Amewaamrisha waislamu kufanya wema na uadilifu na watu wote bila ya kujali dini yao, uraia wao wala kabila lao sharti kutowaudhu waislamu au kuwafanyia khiyana, jambo ambalo linatubainishia msamaha wa dini hii adhimu.

Uislamu ikiwa inawahimiza wafuasi wake kusameheana na kuwa na upole na wepesi, basi dini hiyo wakati huo huo imewakataza kuwa na ugumu na ushadidi, kwa hiyo Mwenyezi Mungu Amekanusha sifa ya ugumu kutoka kwa Mtume wake kwa kusema: {Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu ndio umekuwa laini kwao. Na lau ungeli kuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangeli kukimbia. Basi wasamehe, na waombee maghfira, na shauriana nao katika mambo. Na ukisha kata shauri basi mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanao mtegemea} [3/159].

Imamu Al-Saadiy alipotoa tafsiri ya aya hii alisema: maana ya aya hii ni kwa sababu ya rehma ya Mwenyezi Mungu kwako na maswhaba wako Amekufanya mwenye upole na ulaini nao wakakuamini na kukunusuru na kukupenda, ilhali endapo ulikuwa mkali mwenye moyo mgumu yaani ukiwa na tabia mbaya wanagalikukimbilia kwani mbinu ya kuwaita watu kujiunga na dini na kumfuata Mtume haihusiani na ukali na ugumu kabisa bali, upole, wepesi na ulaini, hivyo ndivyo ilikuwa hali yake Mtume (S.A.W.). Pia, Al-Saadiy aliongeza kuwa kutumia upole katika mambo hupelekea matokeo mazuri na kupata matamanio na matarajio ya mtu, pengine kutumia ukali na ushadidi husababisha kuharibika kwa mambo na kuyafanya magumu zaidi, kwa kueleza ukweli huu Mtume alisema: “Anayenyimwa upole basi amenyimwa heri”. Pia, Mtume alisisitiza kuwa: “Hakika Mwenyezi Mungu ni Mpole na kupenda upole na kutoa thawabu na malipo juu ya upole zaidi kuliko sifa yoyote nyingine”.

Vile vile, upole na ulaini una athari kubwa kuwafanya watu wanaozozana waambatane na kusameheana na kuwaongoza wapotovu na kuwavuta kwenye njia ya heri na mema ya Uislamu, katika hadihi iliyosimuliwa na Bi Asha Mtume (S.A.W.) alisema: “Kwa kweli anayepewa sifa ya upole basi alipewa hadhi yake ya heri ya dunia na akhera”. Kwa kuwa upole na ulaini ni sifa zinazofungamana na miamala baina ya watu na misingi ya kuhurumiana baina ya watu, hatuna budi hapa kueleza namna mbalimbali za usamehevu katika nyanja mbalimbli za maisha kama yafuatayo:

  • Kusameheana katika kuuza na kununua, ambapo kila mmoja muuzaji na mnunuzi wanatakiwa kusameheana na kuhurumiana na kuelewana kwa mujibu wa kauli ya Mtume: “Ni bora kwa mwislamu awe na msamaha na upole akiwa anauza au ananunua au anahojiana na mwenzake”.
  • Kusameheana wakati wa kukabiliwa na mateso na maovu ya wengine, maana mwislamu anatakiwa kuwa na msamaha na watu wote hata wanaomsumbua na kumsababisha maumivu. Inajuliana kuwa Mtume wetu alikuwa mfano bora katika kuwavumilia wengine na adha yao na dalili za hii ni nyingi mno, ambapo watu wake walimlazimisha atoke na ahamie nchi yake anapopenda na kuacha makazi yake na mali yake kwa kupinga wito wake, japokuwa hii aliporejea hakutaka kuwaudhi bali aliwafanyia msamaha mkubwa kuliko katika historia ingawa alikuwa ana uwezo wa kuwaangamiza, bali alitosheleka kumwombea Mwenyezi Mungu awaongoe kwenye njia sahihi ya dini.
  • Kusameheana na watu wote hata wasio waislamu wakati wa amani na vita, ambapo wakati wa vita aghalabu ya watu huwa na hamu ya kuuana na kupigana, jambo linalopelekea maangamizi makubwa na vifo vya wengi na kuiharibu miji na nchi, lakini Uislamu iliweka vidhibiti maalumu kwa hali hii ya kupigana na maadui kutokana na misingi ya usamehevu na kuhurumiana, kwa hiyo dini hiyo adhimu inawaelekeza wapiganaji wake kuwa na huruma hata pamoja na maadui wao maana ni watu. Mtume (S.A.W.) alikuwa akimchagua kiongozi wa kikosi cha wapiganaji anampa wasia awe mcha Mungu katika vita yake na wapiganaji wake kisha alikuwa anasema: anzeni vita kwa jina la Mwenyezi Mungu na kwa ajili yake mpiganeni na wanao kufuru kwa Mwenyezi Mungu bila ya kuvuka mipaka wala kufanya khiyana wala ukatili wala msimwue mchanga ...”. Kwa mujibu wa mafunzo ya Uislamu wapiganaji hawaruhusuwi kuwaua wasio wapiganaji hata wakiwa miongoni mwa maadui, yaani watu wasio wapiganaji kama vile watoto, wanawake, wazee, walemavu, wasio shiriki katika vita kama vile mapadri n.k.

Ikiwa hii ni hali ya msamaha na sura yake wakati wa vita, je wakati wa amani inakuwaje?! Kwa kweli Mwenyezi Mungu Amebainisha hayo kwa kusema: {Mwenyezi Mungu hakukatazini kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawakukupigeni vita, wala hawakukutoeni makwenu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao uadilifu} [60/8] na kutoka kwa Abdullah bin Omar bin Al-As (R.A.) kwamba Mtume (S.A.W.) alisema: “Ye yote atakaemwua mwenye ahadi hatanusa harufu ya pepo, hakika harufu ya pepo hunuswa kwa masafa ya miaka arubaini”.

Kwa hiyo, tunasisitiza ukweli thabiti ambao ni kwamba Uislamu ndiyo dini ya usamehevu na upole na wanadamu wote waislamu na wasio waislamu, na kwamba dini hiyo inawaelekeza wafuasi wake wawe na sifa hizo kwa lengo la kukuza jamii yao na kuendeleza nchi zao wakiepukana na migongano na mizozo na wakiachana na mivutano inayowasukuma kupigana wenyewe kwa wenyewe na wenyewe kwa wengine.

Print
Categories: Makala
Tags:
Rate this article:
No rating

Please login or register to post comments.