Usamehevu ni Msingi wa Kiislamu kwa Shahada ya Wasio Waislamu

Imeandaliwa na Dkt.; Alaa Salah Abdulwahed

  • | Thursday, 16 November, 2023
Usamehevu ni Msingi wa Kiislamu kwa Shahada ya Wasio Waislamu

 

Kwa kweli, Uislamu ndiyo dini ya usamehevu, upendo na tabia njema. Usamehevu ni mojawapo tabia takatifu zilizosisitizwa na Uislamu ambao ni umbile lililopitishwa na Mwenyezi Mungu kuanzia mwanzo wa uumbaji mpaka siku ya mwisho. Mwenyezi Mungu Ameumba mbingu na ardhi, akaumba viumbe vya kila sura na aina, akawatukuza wanadamu na kuwatumia Manabii na Mitume kuwaongoza kwenye njia yake iliyonyooka. Ujumbe wa mbinu kwa Manabii na Mitume wote ulikuwa unajulikana kwa jina la "Hanifiyya Samhaa" jambo linalothibitisha kuwa usamehevu ni msingi muhimu wa jumbe za Mitume wote (A.S.), kwa hiyo, usamehevu, husiano nzuri na upendo huwa sifa kuu za wito wa Manabii na Mitume wote.

Mtume wetu (S.A.W.) ambaye ni Mtume wa mwisho alikuja kukamilisha na kufikisha ujumbe huo huo, bali zaidi ya hayo, kusisitiza kuwa sifa hizo na misingi hiyo hazihusishwi na waislamu tu bali ni misingi ya miamala na watu wote waislamu na wasio waislamu, kwa ajili ya kutimiza maadili ya kibinadamu na kukuza ushirikiano wa kistaarabu. Mwenyezi Mungu (S.W.) Amebainisha kwamba wasilamu wanatakiwa kutendeana na watu wote kwa mujibu wa misingi hiyo ya msamaha na uadilifu Aliposema: {Mwenyezi Mungu hakukatazini kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawakukupigeni vita, wala hawakukutoeni makwenu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao uadilifu} [Al-Mumtahinah: 8].

Kwa kuangalia kwa makini aya hii, tunafahamu kuwa Mwenyezi Mungu Amewaamrisha waislamu kufanya wema na uadilifu na watu wote bila ya kujali dini yao, uraia wao wala kabila lao sharti kutowaudhu waislamu au kuwafanyia khiyana, jambo ambalo linatubainishia msamaha wa dini hii adhimu.

Aidha, Mtume (S.A.W.) amesawiri tabia hii nzuri ya usamehevu kivitendo katika vipindi vyote vya Da'awa na katika hali zote. Pia, Mtume amehimiza sana kueneza tabia hii ya usamehevu baina ya watu wote; waislamu na wasio waislamu, wenyeji wa jamii moja wenyewe kwa wenyewe na wenyewe kwa mataifa wengine, akizingatia usamehevu ni mojawapo maadili mema. Katika maisha yake, Mtume (S.A.W.) alikuwa mwenye msamaha kwa watu wote hata maadui wake waliomuudhi, mpaka akawapa mateka wao msamaha akawaamuru maswahaba wake wawe pole na huruma na mateka hao. Fauka ya hayo, Mtume wakati wa kurudi kutoka At-Taif akiwa na majeraha mabaya na mateso mengi kutokana na aliyoyafanyiwa na watu wa mji huu, akajiwa na Malkia wa Majabali na kusema: "Ewe Mohammed! Hakika Mwenyezi Mungu Amejua waliyoyafanya watu hawa nawe na mimi ni Malkia wa Majabali Amenituma kukuuliza unataka niwafanyie nini, ungekubali niwaangamize kwa kuporomosha milima hiyo miwili wakafa wote ningefanya hivyo. Lakini Mtume (S.A.W.) akakataa kuwaangamiza akisema: Hapana kwani nataraji waongoke au wazae wanaoamini dini hiyo na kumwabudu Mwenyezi Mungu peke yake" imesimuliwa na Muslim.

Kwa hiyo tunaona kwamba Malkia wa Majabali alikuwa anasubiri agizo la Mtume (S.A.W.) kuwaangamiza wale makafiri, lakini rehma yake na msamaha wake ulimfanya akataa kuwafanyia madhara wala adhabu.

Hali hikutofautiana sana aliposhinda washirikina wa Makkah akawa na fursa nzuri ya kulipiza na kuwaadhibu kutokana na uadui wao na mateso waliyosababisha kwa waislamu, ambapo wamewafanyia mabaya na maangamizi makubwa, na kuwalazimisha kutoka na kuacha mali na makazi yao, ingawa haya yote Mtume alipoingia Makkaha akishinda washirikina katika mwaka wa Al-Fat-h, aliwahotubia maqureish waliokusanya wakihofia hatima yao ambayo Mtume ataipitisha akasema Mtume: "Enyi Watu wa Qureish! Je mnadhani kazi gani nitafanya kwenu?! Wakajibu: Labda heri kwani wewe ni mtu mwenye rehma na ukarimu kama ulivyolelewa. Akawaachilia huru na kusema: Mpo huru" Imesimuliwa na Al-Twabariy.

Hivyo, inaonekana wazi namna msamaha na rehma ni sifa za msingi za dini hii na Mtume (S.A.W.), na kwamba dini hiyo adhimu ndiyo dini ya uadilifu, usamehevu na kuhurumiana baina ya wanadamu wote, inayohimiza wafuasi wake wafanye wema na watu wote bila ya kujali dini zao wala uraia wao wala makabila yao. Dini inayohifadhi heshima ya mwanadamu na kuzingatia uhuru wa imani.

Jambo la kuzingatiwa hapa, ni kwamba wengi wa wasio waislamu walikiri sifa hii ya usamehevu wa Uislamu, wengi wao ni wasomi wa nchi za magharibi, kama vile; mwanachuoni mwingereza Thomas Arnold aliyetaja katika kitabu chake: (Kulingania kwa Uislamu):

"Kwa hakika wazo lililoenea kuwa Uislamu ulienea kwa nguvu na ulazimisho halikubaliki hata kidogo, kwani imani ya kiislamu na nadharia yake husifika kwa usamehevu na kuwapa watu uhuru wa kuchagua dini yoyote. Dalili ya haya ni kwamba makafiri walisalia dini zo za kishirki na kuabudu masanamu wakikataa wito wa Mtume , lakini wakati huo huo walikuwa wanapata haki zao zote wakiwa na uhuru kamili usio na mfano hata Ulayani mpaka enzi za hivi karibuni. Inafahamika kwamba kujiunga na Uislamu kutokana na ulazimisho hakukubalika katika sheria ya kiislamu, kwa mujibu wa Qurani Takatifu. Pia, kuwepo kwa makundi mengi ya wakristo katia nchi mbalimbali za kiislamu, wakitawaliwa na waislamu lakini wakati huo wanapewa haki zao zote, ni dalili thabiti ya kuwa usamehevu na miamala mema waliopewa wakristo hao"

Kwa upande wake, mwandishi Mmarekani Louthrob Stodrad alisifu sana yaliyokuwa yanafanywa na Makhalifa wa waislamu na watawala wa miji ya kiislamu kwa wasio waislamu aliposema:

"Khalifa Omar alikuwa anauzingatia sana utukufu wa mahali patakatifu pa kikristo, na kuwa makhalifa waliokuja baadae walikuwa hivyo hivyo, ambapo hawakutusi wakrisro wala hawakuwasumbua mahujaji wakristo waliokuwa wanakuja kila mwaka kuhiji kwa Baitul-Maqdes mjini (Al-Quds / Jerusalem) kutoka kila pembe duniani"

Naye mustashriki mmfaransa Emil Dermenghm huvutwa na kushangaa kwa Uislamu na sifa zke, zilizochangia kwa kiasi kikubwa dini hii ienea na kuvuta na kudadisi duniani. Akitaja kuwa sababu muhimu zaidi ya hayo ni tabia njema za waislamu ambao hawakujibu maovu kwa maovu, bali huwa na msamaha na rehma. Mustashriq huyu amesema katika kitabu chake cha (Maisha ya Mohammed):

 "Hakika Uislamu imeshinda kwani ni dini inayoto wito ambayo nchi na maeneo ya mashariki yalikuwa yanahitaji sana wito kama hii kwa vigezo kama hivyo, ambapo waislamu walivumilia mateso mengi kabla ya Hijra bila ya kujibu uadui huu, na baada ya Hijra wakiwa wameshazoea uvumilivu na kupambana na shida za kila aina wakawa wanalazimika na kusifika kwa usamehevu kwa dhana yake mpana".

Baada ya kusoma maoni haya ya wanachuoni wazungu walio na mitazamo ya ukati na kati wakifuata kweli bila ya kuwa na upendeleo wa upande kuliko mwingine, tunaweza kusema kuwa maoni haya na mengineyo yameafikiana juu ya kwamba Uislamu ni dini inayolingania usamehevu na kuziheshimu dini nyingine na kuwapa wasio waislamu haki zao zote za kuishi katika nchi ya kiislamu kwa amani na uhuru wa kufanya ibada zao. Hilo linamaanisha kwamba Uislamu ni dini ya kuhimiza wema na kukataza shari, dini ya kueneza uadilifu na usawa kwa watu wote kwa kuwa wote ni waja wa Mwenyezi Mungu (S.W.) na hatima zao ni zake tu.    

      

     

 

Print
Categories: Makala
Tags:
Rate this article:
No rating

Please login or register to post comments.