Kwa kuangalia hali ya mambo ya siku za hivi karibuni tunaona kuwa fikra mbovu mbalimbali zimeenea kuushutumu Uislamu kuwa ni dini ya vurugu na ukatili na kwamba dini hiyo ilienea na kufika huko na kule kwa kutumia nguvu ya upanga kwa maana ya kuwatisha watu ama wasilimu au wauawe, ilhali ukweli ni kinyume na madai hayo kwa dalili ya kwamba wengi wa waliojiunga na Uislamu walijiunga na dini hiyo kwa hiari yao. Pia, wengi wa waliosilimu walijiunga na dini hii bila ya kupiganiwa wala kulazimishwa wawe waislamu, bali waliitwa wakakubali hasa baada ya kuwaona waislamu na tabia yao na maisha yao, Mwenyezi Mungu Anaeleza kuwa dini hii ni dini ya ulaini na upole wala hakuna ulazimisho katika dini hii: {Hapana kulazimisha katika Dini. Kwani Uwongofu umekwisha pambanuka na upotofu. Basi anaye mkataa Shet'ani na akamuamini Mwenyezi Mungu bila ya shaka amekamata kishikio madhubuti, kisicho vunjika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua} [2/256].
Kwa mujibu wa aya hii imani ya aliyelazimishwa haisihi wala waikubaliki katika sheria ya kiislamu wala haijuzu kuuawa kwa kutoamini kwani Mwenyezi Mungu (S.W.) Alithibitisha kuwa imani ni kwa hiari siyo kwa ulazimisho na kwamba Akitaka Angewafanya watu wote waamini: {Angeli taka Mola wako Mlezi wangeli amini wote waliomo katika ardhi. Je, wewe utawalazimisha watu kwa nguvu mpaka wawe Waumini?} [10/99]. Kwa hiyo, damu ina haki ya kutomwagika bure wala kwa sababu ya kutofautiana katika dini, kwa kuwa Mwenyezi Mungu Ameonya kikali na kuwatahadharisha waja wake wasiuana Aliposema: {Na mwenye kumuuwa Muumini kwa kukusudia, basi malipo yake ni Jahannamu humo atadumu, na Mwenyezi Mungu amemkasirikia, na amemlaani, na amemuandalia adhabu kubwa} [4/93].
Katika tafsiri yake kwa aya hii, Imamu Ibn Kathir alisema kwamba Mwenyezi Mungu Ametoa onyo kali mno kwa kila anayefanya kosa hilo ambalo limeambatana na ushirikina katika aya nyingi katika Qurani Takatifu. Pia Mwenyezi Mungu kauli yake Mwenyezi Mungu: {Kwa sababu ya hayo tuliwaandikia Wana wa Israili ya kwamba aliye muuwa mtu bila ya yeye kuuwa, au kufanya uchafuzi katika nchi, basi ni kama amewauwa watu wote. Na mwenye kumuokoa mtu na mauti ni kama amewaokoa watu wote. Na hakika waliwajia Mitume wetu na hoja zilizo wazi. Kisha wengi katika wao baada ya haya wakawa waharibifu katika nchi} [5/32] Kwa kuelewa maana na tafsiri ya aya hii tunaona namna Mwenyezi Mungu Alivyofanya dhambi hiyo ya kumuua mtu pasipo na haki ni kama aliyewaua watu wote kwa kuwakataza kutofanya uhalifu huu.
Ibnu Abbas (R.A.) alisema kuwa yeyote anayemuua nabii au imamu mwadilifu basi huwa katika dhambi sawa na aliyewaua watu wote na anayemwokoa mtu huwa sawa na anayewaokoa wanadamu wote. Kwa upande wake Imamu Ibnu Hajar alisema aya hii ina mubalagha wazi ambapo Mwenyezi Mungu Alisawazisha baina ya kumuua mtu mmoja na kuwaua watu wote kwa kusisitiza ubaya wa kosa hilo. Inaonekana kuwa hukumu hii haiusiani na waislamu tu, lakini inawahusu wanadamu wote bila ya kujali dini, rangi, kabila, uraia n.k. kwa kuwa kumuua mtu yoyote ni kosa kubwa kabisa ingawa yule mtu ni nani.
Ama kuhusu adhabu ya kulipiza kisasi basi ni adhabu iliyopitishwa na sheria ya kiislamu kwa kumkataza mwislamu asifanya kosa hilo kwa kuwa damu ya mtu yoyote ni haramu, wakati huo huo ni haki ya jamaa wa aliyeuawa wanaweza kukubali fidia au kisasi. Hekima ya adhabu ya kilipiza ni kuwazuia mauaji siyo kuyaeneza kwani anayetaka kufanya uhalifu huu anapofikiria hali yake na adhabu inayomsubiri huweza kujizuia, kwa hiyo Mwenyezi Mungu Amesema kuwa kulipiza ni uhai: {Mtakuwa nao uhai mzuri katika kulipiza kisasi enyi wenye akili, ili msalimike} [2/179], maana aliyoisema Abu Al-Aaliya ni kwamba Mwenyezi Mungu Amefananisha kulipiza kisasi na uhai kwa sababu ya anaye nia ya kumuua mwenzake atakapoelewa kuwa atauawa kwa kosa lake hilo huenda atajizuia. Pia miongoni mwa sifa za waja wa Mwenyezi Mungu kuepukana na damu kama Alivyosema Mwenyezi Mungu: {Na wale wasio mwomba mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu, wala hawaui nafsi aliyo iharimisha Mwenyezi Mungu isipo kuwa kwa haki, wala hawazini – na atakaye fanya hayo atapata madhara* Atazidishiwa adhabu Siku ya Kiyama, na atadumu humo kwa kufedheheka* Isipo kuwa atakaye tubu, na akaamini, na akatenda vitendo vyema. Basi hao Mwenyezi Mungu atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu} [25/68-70].
Vile vile Mtume (S.A.W.) ametahadharisha vikali umwagaji damu pasipo na haki, kutokana na Abu Hurairah (R.A.) amesimulia kuwa Mtume (S.A.W.) amesema: “Jiepukaneni na maovu makubwa saba! Maswahaba wakasema: Ewe Mtume maovu haya ni nini? Akasema: ushirikina, uchawi, kumuua nafsi pasipo na haki, kula riba, kumwibia yatima mali yake, kutoroka wakati wa vita na kuwatuhumu wanawake waumini wanaotaharika kwa zinaa”. Na kutoka kwa Abdulla bin Masoud kwamba Mtume (S.A.W.) alisema: “Kwa hakika haijuzu kumwagika damu ya mwislamu anayekiri kuwa hapana Mungu isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba mimi ni Mtume wake ila akifanya mojawapo maovu matatu yafuatayo: kumuua mtu, kufanya zinaa ilhali ameoa na aliyeritadi na kuacha dini na jamaa wake”.