Kwa hakika Mwenyezi Mungu ameumba mbingu na Ardhi na akajichagulia mbingu ya saba na Makka pakawa ni patakatifu akaumba pepo na Malaika, akaifanya firdausi ndio pepo ya juu zaidi, na Jibril ndiye kiongozi wa Malaika na katika mwaka akaweka miezi, siku, nyakati za siku na saa. Akachagua mwezi mtukufu wa Ramadhani, siku bora ni Ijumaa, usiku mtakatifu ni Lailatul Qadri, na saa ya kukubaliwa dua ipo Ijumaa na masiku matukufu yapo kwenye siku kumi za mwanzo wa mfungo tatu. Allah akawaumba wanadamu, akawachagua aliowathamini ni muuminina, na akawachagua katika muuminina mitume, akawapandisha cheo mitume fulani, akaita rusul, na katika rusul akawapandisha wengine wanajulikana ulul–‘azm, na katika hao akatubainishia vipenzi vyake, na bila shaka katika vipenzi vya Allah kiongozi wao ni Mtume wetu Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam).
Muislamu alibarikiwa na Mwenyezi Mungu, aliwekewa madaftari mawili, moja kuandikiwa mazuri yake na jengine kuandikiwa mabaya yake. Ama kafiri aliwekewa daftari moja tu analoandikiwa mabaya tu. Ni juu ya Muislamu awe na lengo la kwenda peponi ajizatiti kiibada kila zama na awe na malengo kwa kila msimu, kwani Mola na Mtume walitueleza siri hiyo.
Kwa kweli kufika kuishi mpaka kushuhudia siku kumi za mwanzo wa mwezi mtukufu wa Dhul-Hijja ni neema kubwa kutoka Mwenyezi Mungu ambayo inatupasa tumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa neema Aliyotujaalia ya kutuwekea miezi mitukufu, au siku tukufu au nyakati tukufu ambazo ‘amali njema huwa na thawabu nyingi mno. Na hivi tunakaribia kabisa kuingia katika mwezi mwingine mtukufu wa Dhul-Hijjah.
Katika mwezi huu, siku kumi za mwanzo ni siku bora kabisa mbele ya Allaah ambazo 'amali yoyote inayotendwa humo ni yenye kupendwa mno na Allaah, Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) ameahadithia kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakuna siku ambazo ‘amali njema zinazotendwa humo, zinapendwa mno na Allaah kama (‘amali zinazotendwa katika) siku kumi hizi.” Yaani: Siku kumi za mwanzo wa mwezi wa Dhul-Hijjah. Wakauliza: Ee Rasuli wa Allaah! Je, hata kuliko jihaad katika njia ya Allaah? Akajibu: “Hata Jihaad katika njia ya Allaah isipokuwa mtu aliyekwenda na nafsi yake na mali yake ikawa hakurudi na kimojawapo.” [Al-Bukhaariy].
Ee ndugu Muislamu! Usiache fursa hii kukupita kujichumia thawabu tele kutokana na uzito wa malipo katika masiku haya. Hivyo basi tunawanasihi kusoma yafuatayo kuhusu fadhila za masiku haya kumi ya Dhul-Hijjah pamoja na amali za kutenda katika masiku haya matukufu kabisa mbele ya Allaah ('Azza wa Jalla).
Kwa jinsi zilivyokuwa na umuhimu mkubwa siku hizo kumi, hadi kwamba Allaah (Subhaanah wa Ta'aalaa) Ameziapia katika Qur-aan Anaposema: {Naapa kwa Alfajiri * Na kwa masiku kumi} [Al-Fajr: 1-2], Wanachuoni wafasiri wa Qur-aan wamekubaliana kwamba zilokusudiwa hapo ni siku kumi za Dhul-Hijjah.
Pia, Inapasa kumdhukuru mno Allaah (Subhaanah wa Ta’alaa) kwa kukumbuka neema Zake zisizohesabika kama Anavyosema: {Ili washuhudie manufaa yao na kulitaja Jina la Allaah katika siku zinazojulikana} [Al-Hajj: 28]
Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) kasema: “Hizo ni siku kumi za Dhul-Hijjah.” Na Amesema: “Manufaa ya dunia hii na ya Aakhirah.” Manufaa ya Aakhirah yanajumuisha kupata radhi za Allaah. Manufaa ya vitu vya dunia inajumuisha wanyama wa kuchinjwa na biashara. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]
Kutokana na ilivyotajwa katika usimulizi wa Hadiyth ifuatayo, kwamba amali yoyote utendayo katika masiku kumi hayo, ni bora kuliko kwenda kupigana jihaad vitani. Ukizingatia kwenda kupigana jihaad ni jambo zito mtu kuliitikia, kwani huko kuna mashaka mbali mbali, ikiwemo kupoteza mali, khofu ya kujeruhiwa na kupoteza viungo vya mwili, kufariki, n.k. Ila hilo si zito kwa mwenye iymaan ya hali ya juu kabisa kutaka kuyakabili mashaka hayo na kutamani kufa shahidi. Kwa hiyo usidharau ‘amali yoyote hata iwe ndogo vipi itekeleze kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni Al-Jawwaad (Mwingi wa Ukarimu), Al-Kariym (Mkarimu), Al-Wahhaab (Mwingi wa kutunuku, Mpaji wa yote), Al-Majiyd (Mwingi mno wa vipawa na ukarimu).
Vile vile, miongoni mwa fadhila na ubora wa siku hizo takatifu kwamba ibada zote zimejumuika katika siku kumi hizi nazo ni Swalaah, kufunga Swiyaam, Swadaqah, Hajj, wala hazijumuiki pamoja wakati mwingine.
Aidha, Msimu wa ibada wa siku hizi kumi, haupatikani ila kwa mwaka mara moja. Dakika zake, saa, siku na wiki, ndizo zinazompendeza Mwenyezi Mungu, lau mwanadamu atajitahidi kiibada siku hizi, atakuwa amefaulu sana.
Katika siku hizi kumi, siku ya tisa inajulikana ni siku ya ‘Arafa, inajulikana kwa thawabu na msamaha mwingi kutoka kwa Allah, ndio siku waumini wanapeleka dua zao kwa wingi. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [Dua bora nzito ni ya siku ya ‘Arafa]. Na kwa sababu waumini wengi wameacha machafu yao kwa ajili ya ‘Arafa, mahujaji na wasiokuwa mahujaji na ndio siku ya hijja kubwa. Na mwenye kufunga siku hii husamehewa madhambi ya mwaka uliopita na mwaka ujao.
Ipo siku ya mwisho, siku ya kumi ya mfungo tatu, inayojulikana kuwa ni siku ya kuchinja, zipo ibada tofauti tofauti, kutupa vijiwe, kunyoa, kutufu, kukimbia baina ya Swafaa na Marwaa, kuchinja na kuswali Iddi.
Fadhila za siku hii ni nyingi. Muislamu anatakikana asizipoteze, bali azipatilize na ashindane katika mambo ya kheri na ajishughulishe kwa amali njema.
Ndugu Muislamu, Usighafilike, Mwenyezi Mungu ndiye aliyekuumba hivyo ulivyo na akakuchagulia alichokuchagulia na akakupa nawe nafasi ya kujichagulia vile utakavyo, kuwa na moyo, uchume juani kwa muda mfupi na ukale kivulini kwa muda mrefu kwenye maisha ya milele, Allah ametudokezea misimu tofauti tofauti yenye malipo mbali mbali, kwa mfano, lailatul-Qadri na masiku kumi ya mfungo tatu. Tuzidishe ibada katika siku hizi kumi kwa kuswali, kufunga, kutoa sadaka, kuleta tasbihi, tahlili na mwisho kuswali idd na kuchinja.