Athari za Dawa za Kulevya juu ya Usalama na Amani ya Jamii

Imeandaliwa na Dkt., Alaa Salah Abdulwahed

  • | Thursday, 27 June, 2024
Athari za Dawa za Kulevya juu ya Usalama na Amani ya Jamii

 

 

    Kwa hakika Mwenyezi Mungu Amemtukuza mwanadamu akamfanya kiumbe bora kuliko viumbe wengine wote, kwa mujibu wa kauli ya Mwenyezi Mungu: {Na hakika tumewatukuza wanaadamu, na tumewapa vya kupanda nchi kavu na baharini, na tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tulio waumba} [17/70]. Na kauli yake (S.W.): {Bila ya shaka tumemuumba mtu kwa umbo lilio bora kabisa} [95/4].

Kwa hiyo mwanadamu ni kiumbe ambaye ameumbwa kwa namna iliyo bota akapewa heshima na fadhila kubwa zaidi kuliko viumbe wengine. Na kati ya misingi ya kumtukuza mwanadamu kuliko viumbe wengine akili ambayo ni kiungo cha kumwongoza mwanadamu na kumbainishia heri na shari, wema na uovu, zuri na baya ili awe na mamlaka na uwezo wa kujiamua na kuendesha maisha yake mwenyewe, tena kujiendeleza na kujipatia yaliyo mazuri na kuepukana na mabaya.

Inafahamika kwamba Mwenyezi Mungu Amewaamuru waja wake wamshukuru kuhusu neema nyingi nyingi Alizowapa na kwa kuangalia njia za kutoa shukurani kuhusu neema hizo tunatambua kuwa kuzilinda neema ni njia ya msingi ya kueleza shukrani kwa neema pamoja na kuziendeleza, kwa mfano neema ya akili shukrani zake ni kwa kuilinda kutokana na uharibifu wowote na kuiendeleza kwa elimu na mafunzo mazuri yenye faida.

La kushangaza kuona baadhi ya watu wanaziharibu akili zao kwa makusudi kwa kutumia dawa za kulevya wakipuuza madhara yatokanayo tabia hiyo mbaya. Hawa wanakuwa wanajiua kidogo kidogo na kuharibu maisha yao wenyewe, mwishoni wanajikuta wameshapotea kabisa wakaharibiwa maisha yao.

Kwa jumla, utumiaji wa dawa za kulevya unaharibu na kuangamiza mahusiano ya kijamii na kusababisha jamii isambaratike na kudhoofika. Tabia hiyo mbaya inaathiria vibaya mshikamano wa jamii na kuipelekea kuwa jamii ambayo haina nguvu kabisa.

Kwa upande mwingine, tabia ya kutumia dawa za kulevya huathiria vibaya siyo kwa jamii tu bali hali ya kiuchumi pia inaathirika vibaya kwa tabia hiyo, ambapo watumiaji wa dawa hizo hawasaidii uchumi wa nchi yao ila kuuharibu kwa kununua dawa hizo kwa njia ambazo hazina faida yoyote kwa uchumi. Vile vile, wanatumia hela nyingi katika biashara hiyo haramu ambayo uchumi wa nchi haufaidiki chochote kutokana biashara hiyo bali hupata hasara kubwa katika juhudi za kufuta athari mbaya zinazosababishwa na tabia hiyo.

Zaidi ya hayo, watumiaji wa dawa za kulevya hawana mchango wowote kuusukuma na kuusaidia uchumi wa nchi yao uimarike na kuendelezwa. Watumiaji wa dawa za kulevya wanatumia mapato yao yote katika njia hiyo mbaya wakijinyima na jamaa zao kunufaika na mapato hayo katika mambo yenye faida mpaka mahitaji ya lazima ya maisha yao.

Kwa hakika tabia ya kutumia dawa za kulevya ni tabia mbaya inayoharibu mtu na jamii nzima na ni njia mojawapo njia za kuziharibu jamii na kuzigeuza jamii zisizo na nguvu yoyote ya kupambana na maadui wala kukidhi mahitaji na matarajio ya wananchi na nchi zenyewe. Athari za tabia hiyo hazimwathiria mtumiaji tu bali zinaathiria hali ya kijamii na kiuchumi kwa jumla.

Kwa hakika, ulevi na kutumia dawa za kulevya humpelekea mtu ajitupe katika maovu na mabaya makubwa kama vile; kuzuia njia ya Mwenyezi Mungu na kujiweka mbali na njia yake. Pia, miongoni mwa athari mbaya za kutumia dawa za kulevya kutokubalika kwa dua ambapo mtumiaji wa dawa za kulevya tayari amepinga kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu akakwenda kinyume na maamrisho na makatazo aliyoletewa na Mola wake, jambo ambalo linafanya dua zake zisikubaliki. Vile vile, mtumiaji wa dawa za kulevya ni mfano mbaya ambaye anawaita watu kwa mabaya na maovu.

Vile vile, ulevi humpelekea mtu alaaniwa na kufukuzwa kutoka rehma na amani ya Mwenyezi Mungu na ridha ya Mtume. Pia, kutumia dawa za kulevya husababisha magonjwa mengi ambayo yanaweza kumwangamiza mtumiaji wa dawa hzio, licha ya hayo tabia ya kutumia dawa za kulevya huharibu mahusiano ya kijamii na kueneza maovu na mabaya katika jamii pamoja na kuchochea jinai na uhalifu wa aina mbalimbali.

Print
Categories: Makala
Tags:
Rate this article:
No rating

Please login or register to post comments.