Ukati na kati/ uwastani ni sifa mojawapo sifa kuu za sheria takatifu ya kiislamu, ambapo sheria hii inasifika kuwa ni sheria ya usamehevu, ulaini na kuhurumiana, kwani sheria hii ndiyo sheria inayoambatana na maumbile sahihi ya mwanadamu. Uislamu ni dini inayopendeleza zaidi ukati na kati katika mambo yake yote, kidini, kidunia, ibada, miamala n.k. Kwa hiyo, Mwenyezi Mungu (S.W.) Amebainisha kuwa umma huu kwa kufuata dini hiyo takatifu ndio umma wa wastani na kwamba mbinu yake ni mbinu ya kiwastani, Mwenyezi Mungu Amesema: {Na vivyo hivyo tumekufanyeni muwe Umma wa wasitani} [Al-Baqarah: 143].
Kwa mujibu wa Aliyoyasema Mwenyezi Mungu umma wa kiislamu ni umma wa wastani ambao unakuwa mashahidi juu ya watu wote kwa uadilifu, na kuwaelekeza kwenye maadili mema ambapo Uislamu ni dini ya wepesi na ulaini pasi na haraja, dhiki wala kuwashadidishia watu mambo wasiyoyaweza. Ni dini ya uwiano baina ya mahitaji ya mwili na mahitaji ya roho, yeyote haruhusiwi kujizuia vitu vilivyo halali kwake, bali anatakiwa kujikurubisha kwa Mola wake kupitia wajibu na mubaha.
Kwa maana hiyo, Ukati na kati (Wastani) ni: kuhakikisha uwiano unaotegemewa kuendesha mambo ya viumbe vyote, kutokana na matakwa ya Mwenyezi Mungu na Sunna yake Aliyoipitisha, na kwa hikima na upangaji wa awali unaowekwa na Mwenyezi Mungu Mwenye kukadiria kila kitu kwa kipimo chake cha pekee. Uwiano huu unaomaanisha wastani na kusawazisha baina ya vitu vyote na kuvifanya vikamilishane, uwiano huo ndio kaida ya msingi na sifa kuu ya ukati na kati, kwani uwiano huu ukikosekana wastani huwa umekosa nguzo wake wa msingi, kwa sababu hali hii itasababisha kujitokeza upendeleo badala ya uwiano, hivyo uadilifu hukosekana pia. Kwa jumla, kupendelea ncha moja kuliko nyingine kunakataliwa katika Uislamu, ambapo dini hii ni dini ya wastani na uadilifu bila ya kupunguza wala kuongeza. Maana kukosa uwiano na usawa ni chanzo cha matatizo mengi.
Ishara za Wastani katika Uislamu na sura zake ziko nyingi, miongoni mwa sura hizo:
Mosi: Wastani wa Uislamu katika sheria zake, unadhihirika katika mambo kadhaa katika sheria kama vile; kufuata mbinu wa kutoa hukumu kidogo kidogo, ni dalili mojawapo dalili za rehma ya Mwenyezi Mungu aliyokuja nayo Mtume (S.A.W.) kwamba sheria ya kiislamu haikutoa agizo au katazo mara moja, bali kidogo kidogo ili waislamu waweze kutekeleza lile agizo na kuzoea kulifanya au kuepukana na katazo hilo na kuzoea kuachana nalo. Sheria ya kiislamu ilifuata mbinu hiyo katika hukumu nyingi na hasa makatazo au mambo yaliyoharamishwa kama vile kuondoa masanamu katika eneo la Ka'aba, hukumu hiyo imetolewa na kutekelezwa taratibu, amapo inajulikana kuwa masanamu yameondolewa siku ya kuingia Mtume (S.A.W.) Makka mshindi siku ya Al-Fath. Mfano mwingine ni kukataza ulevi ulioharamishwa kidogo kidogo.
Mwanzoni wa Uislamu sheria ya kiislamu imejikita zaidi kuharamisha movu kuliko kuamrisha mema, kwa kuwa kuanzisha jamii mpya inahitaji kuondoa athari mbaya za enzi zilizopita, kwa hiyo sheria imeanza kuharamisha mabaya haya kidogo kidogo kuanzia kuziandaa nafsi zikubali hukumu za Mwenyezi Mungu kwa lengo la kuhakikisha mwitikio wa watu lengwa kwa hukumu za dini, hasa wale waliozoea kufanya mabaya haya. Pia, mfumo huo wa kuharamisha na kutoa makatazo kidogo kidogo unalenga kutoa hukumu kwa ulaini na upole na kuwapa walinganiwa fursa ya kupata nafuu kutokana na mabaya haya ambayo ni kama maradhi yanahitaji muda wa kupona. Mfumo wa kutoa hukumu za kisheria kidogo kidogo unahitajika hasa katika mambo yaliyoendelea kwa muda mrefu katika jamii ya kabla ya Uislamu kama ulevi na kuyaaudu masanamu.
Yeyote anayetafakuri kuhusu hukumu zote za sheria ya kiislamu hatapata ugumu kutambua kuwa hukumu hizo zimetegemea sana urahisishaji na wepesi, ambapo hiyo ndiyo mbinu ya Mwenyezi Mungu na Mtume, na sifa ya msingi ya dini hii adhimu. Sifa takatifu za dini hiyo zinadhihirika wazi katika sira ya Mtume (S.A.W.) na shime aliyokuwa nayo kwa wepesi na upole hata alikuwa anawahimiza maswahaba wake kufuata mbinu hiyo hiyo katika Da'awa na kutoa hukumu za kisheria.
Matini za kuthibitisha upole wa dini na wepesi wake ziko nyingi, Mwenyezi Mungu Amesema: {Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito} [Al-Baqarah: 185], Amesema pia: {Hapendi Mwenyezi Mungu kukutieni katika taabu} [Al-Maidah: 6], Amesisitiza pia: {Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika Dini} [Al-Hajj: 78]. Vile vile, katika sunna za Mtume (S.A.W.) jambo hilo hilo limesisitiziwa sana, ambapo Abu Hurairah (R.A.) amesimulia kuwa Mtume (S.A.W.) amesema: "Hakika dini hii ni nyepesi, na yeyote atakayebishana na dini ila atashindwa, kwa hiyo fanyeni ulaini na upole na jitahidieni zaidi katika ibada nyakati za asubuhi na jioni na sehemu ya usiku". Pia, Mtume (S.A.W.) alikuwa mfano bora wa upole na ulaini, ambapo hiyo ndiyo ilikuwa sifa kuu yake kama alivyoeleza Bibi Aisha (R.A.) aliposema: "Mtume (S.A.W.) akiwa anachagua baina ya mambo mawili alikuwa anachagua lililo rahisi zaidi"
Pili: Wastani wa Uislamu katika Da'awa, kwa kweli Da'awa ya Uislamu ina mbinu maalum ambazo kimsingi zinategemea upole na usamehevu siyo kama wanavyodai baadhi ya wasiojua chochote kuhusu Uislamu kuwa dini hiyo imenea kwa kutumia nguvu kwa dalili ya kwamba wengi waliojiunga na Uislamu hawakulazimishwa kufanya hivyo bali waliona na kutambua utukufu wa dini hiyo na usamehevu wake. Kwa hakika historia ya kiislamu haikushuhudia tukio hata moja la kuwalazimisha au kutishia watu waingie katika dini hata katika hali ya vita na maadui.
Zaidi ya hayo, lengo kuu ya dini ni kuwaongoza watu wote kwenye njia ya Mwenyezi Mungu ambayo ni njia ya amani, utulivu na uhuru. Kwa hiyo, Da'awa ya kiislamu haikuhusishwa na Waarabu peke yao, kwani Uislamu ni dini iliyoteremshwa kwa wanadamu wote, na Mtume (S.A.W.) ndiye rehma kwa malimwengu, hivyo mbinu aliyoitumia katika Da'awa ilitokana na kauli ya Mwenyezi Mungu (S.W.): {Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. Hakika Mola wako Mlezi ndiye anaye mjua zaidi aliye ipotea Njia yake, na Yeye ndiye anayewajua zaidi walio ongoka} [An-Nahli: 125].