Afrikaans (Suid-Afrika)

منبرٌ كبيرٌ لنشر وسطية الأزهر الشريف بكل لغات العالم

 

HOTUBA YA IMAM MKUU:  Prof. Ahmad Al-Tayyib  Sheikh wa Al-Azhar  Katika:  Sherehe za kumbukumbu za kuzaliwa kwa Mtume Mtukufu  1439H – 2017
Anonym
/ Categories: Main_Category

HOTUBA YA IMAM MKUU: Prof. Ahmad Al-Tayyib Sheikh wa Al-Azhar Katika: Sherehe za kumbukumbu za kuzaliwa kwa Mtume Mtukufu 1439H – 2017

 

 

 

 

HOTUBA YA IMAM MKUU:

Prof. Ahmad Al-Tayyib

Sheikh wa Al-Azhar

Katika:

Sherehe za kumbukumbu za kuzaliwa
kwa Mtume Mtukufu

1439H – 2017

 

Katika Ukumbi wa Mikutano wa Al-Azhar

                                                                                                                                          

 

Imetolewa: 11/mfungo sita / 1439H

Sawa na tarehe 29/ November / 2017

 

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

Namshukuru Mwenyezi Mungu, Sala na Salamu za Mwenyezi Mungu ziwe kwa mwenye kumbukumbu hii nzuri Mtume wetu Muhammad pamoja na watu wake na Masahaba zake watakatifu.

Mheshimiwa Rais Abdulfattah Sisi, Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri - Mwenyezi Mungu Amhifadhi kumchunga na kumwongoza hatua zake.

Wageni Waalikwa

Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yenu na Rehema zake na Baraka zake

Ama baada ya hayo:

Kwa hakika sherehe zetu hizi leo za kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Mtakatifu - ukweli - ni sherehe za kuja kwa Utume wa mwisho, na Ujumbe wa mwisho wa Mwenyezi Mungu, Ujumbe ambao umewaweka wanadamu wote katika njia iliyonyooka, na kuwatoa katika kiza cha ujinga na upotevu baada ya kukombolewa akili ya mwanadamu kutokana na chuki za kikabila, vikwazo vya utawala wa kifamilia na mfumo wa kabila, na baada ya kukombolewa dhamira ya mwanadamu kutokana na minyororo ya dhuluma, pamoja na ukandamizaji na utumwa… baada ya kufariki Mtume mwenye Ujumbe wa kudumu kwa miaka kumi tu([1]) ndipo ilipoanza kuporomoka ngome za waovu majabari na wenye kudai Uungu moja baada ya nyengine, na kuanza utu na ubinadamu - kwa mara ya kwanza katika historia yake - kunusa harufu ya uhuru, kuonja ladha ya uadilifu na kuelewa maana ya usawa kati ya watu na ulazima wa kumkomboa mwanadamu kutokana na dhuluma ya ndugu yake mwanadamu.

Imamu At-Tabary katika kitabu chake cha historia, anataja kuwa Rabi’y bin A’mir mmoja wa viongozi wa ukombozi wa Kiislamu pindi alipoingia kwa “Rostam” kiongozi wa jeshi la Fursi ili kufanya naye mazungumzo kabla ya kuanza kwa vita vya Al-Qadisiyya, Rostam alimwuliza: kipi kimekuleteni? Rabi’y akasema: “Mwenyezi Mungu Ametutuma ili  kuwatoa wenye kuwaabudu waja na kuwaleta katika ibada ya Mwenyezi Mungu, na kuwatoa katika dhiki na mateso ya dunia na kuwaleta katika mapana yake”([2]). Hayo ni maneno machache ambayo  yanaakisi kukosa kwa Sahaba huyu thamani ya uhuru na uadilifu, na kiu yake ya kutaka watu waishi katika uhuru na uadilifu, kabla ya kujiliwa vitu hivyo viwili na Dini hii mpya.

Ni juu yetu tuzingatie ibara yake huyu Sahaba R.A. pale aliposema “kuwatoa katika dhiki na mateso ya dunia na kuwaleta katika mapana yake” ili tufahamu namna ya maisha ya watu kabla ya hii Dini yalikuwa ni yenye maumivu chini ya mminyo ambao uliwekwa juu yao na mifumo yao ya kisiasa, na staili zao kijamii na kiuchumi, na kuwa Ujumbe huu wa mwisho umekuja ili kuikomboa akili, fikra na dhamira… na njia yake katika kumkomboa mwanadamu ni: msingi wa uhuru uliodhibitiwa pamoja na msingi wa uadilifu, ambao unadhamini kupewa kila mwenye haki haki yake, ambapo pasi na uadilifu moja kwa moja unaharibika uhuru, na kubadilika kuwa ni fujo zinazoondoa misingi mingine ya ubinadamu.

Wageni Waalikwa!

Ikiwa Ujumbe wa mwenye kumbukumbu hii nzuri ni muhimu ili kuongozea watu, basi kujikwaa njia yake ni katika mambo hatari yenye kuharibu staarabu na jamii.

Historia inathibitisha kuwa kudondoka kwa staarabu kulikuwa kwa sababu zilizotajwa na Qurani Takatifu pamoja na kutahadharisha, nazo zinazoitwa utaratibu wa Mwenyezi Mungu katika ulimwengu na wanadamu, na katika sababu muhimu ni kwenda kinyume na mfumo wa Utume katika siasa za kuongoza watu na jamii, kinyume na kuchukua kwao maadili mema ambayo ndiyo lengo lenyewe la kutumwa kwa Mitume, na kwa rehema ya Muumba kwa viumbe vyote, Mtume S.A.W. amesema kuwa: “Hakika yangu nimetumwa ili kukamilisha maadili mema” na akasema tena: “Enyi watu! Hakika mimi ni rehema yenye kuongoza” baada ya kusema Mola Mtukufu: (Na wala hatukukutuma Wewe isipokuwa uwe ni rehema kwa walimwengu wote){Al-Anbiyaa, 107}.

Na kama inavyokuwa kukiuka mwenendo wa Mitume ni kupinga Dini na kuipiga vita, pamoja na kulingania kupinga uwepo wa Mungu, kukufuru Mungu, Malaika wake, Vitabu vyake, Mitume yake na Siku ya Mwisho, vile vile ukiukaji unakuwa na sura ya hatari zaidi na uharibifu unapotokea kwa makundi yaendayo kinyume, na kupelekea akili zao zenye ugonjwa kujiona wao ndio wenye mamlaka juu ya watu, na wao ni mawakala wa Mwenyezi Mungu kwenye mgongo huu wa ardhi, wao peke yao ndio wenye ufahamu wa Dini na tafsiri ya hukumu zake.

Kundi hili au makundi haya ya kigaidi - kwa tofauti ya majina yake - msingi wa imani yao siyo sahihi, naye Mwenyezi Mungu Mtume wake na Waumini wapo mbali kabisa na imani hiyo. Imani yao ni kuwa: yule asiyeamini imani yao miongoni mwa Waislamu, basi huyo ni kafiri, na kwamba kafiri ni halali damu yake mali na heshima .. na mfano wa kundi hili lenye kupotea si lenye kuzuka katika historia ya Waislamu tu, bali yapo pia katika dini zengine imani na madhehebu mengine. Kiukweli yanayotangazwa hivi sasa kuwa ugaidi unatokana na tasnia halisi ya Uislamu, na kuwa unaendesha vitendo vya kuua wasiokuwa Waislamu tu ni maneno ya uzushi yanapingana na uhalisia ambao unakadhibisha uzushi huu pamoja na kufedhehesha nia za wasambazaji wake, kwani vitabu vya historia na vya siasa vimejaa maandiko kuhusu vitendo vya ugaidi vilivyoonasibishwa na dini, na madhehebu ya kisiasa na kijamii.

Na wala hatutaki kuzungumza mbali na msiba ambao umetikisa nyoyo za Wamisri siku ya Ijumaa iliyopita, lakini pia umetikisa wanadamu wote Magharibi na Mashariki, kwa hakika tukio lililotokea Msikiti wa Raudha lilikuwa ni baya mno, na utekelezaji wake uovu ulikuwa si wenye kufikiriwa, wala kutarajiwa kufanywa na mwanadamu wala mnyama wa porini… na hizi risasi ambazo zililenga roho za wenye kusali ndani ya Msikiti kwa sehemu ya kwanza ni vita dhidi ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na kumpinga Mola Mtukufu ndani ya nyumba miongoni mwa nyumba zake.

Wahalifu hawa hawakuwa ni wa kwanza kutekeleza mfano wa uhalifu huu ndani ya nyumba za Mwenyezi Mungu, hakika aliuwawa Khalifa wa pili wa Mtume S.A.W. naye ni: Umar bin Al-Khattab R.A. hali ya kuwa anasali katika mihirabu ya Msikiti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. naye Khalifa wa tatu Uthman bin Affan R.A. aliuwawa hali ya kuwa anasoma Qurani, na damu yake ilitapakaa kwenye msahafu ambao alikuwa anasomea. Hali kadhalika watu wa Khawaarij waliua waliowatangulia na babu zao, naye Ally R.A. aliuwawa akiwa kwenye Sala ya alfajiri huku akiwaita watu kuja kusali.

Na katika kuuwawa kwa Makhalifa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. na kufa kwao mashahidi kwa silaha na kwa usaliti, kuna maombolezo - na ni maombolezo gani!- kwetu na kwa watu wetu miongoni mwa wale waliofiwa na watoto wao pamoja na wategemezi wao … na mkiwa nyinyi - watu wetu wa eneo la Bir Al-A’bd - mmetishwa na kufadhahishwa, basi kumbukeni kuwa historia ya hawa Khawaarij inafahamika katika kuwatia hofu Masahaba za Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. kuwashambulia na kumkufurisha Ally na kumuuwa baada ya kutengana naye na kumvamia.

Na sisi - Mheshimiwa Rais! - tunakupa pole na kuwapa pole wananchi wetu imara kwa ajili ya mashahidi wetu wasio na hatia, tunamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu Awapokee kwa huruma yake pana na radhi zake na kuwaweka katika Pepo yake, na kuunganisha nyoyo za ndugu zao na watu wao, na Awaponye haraka wale walioumia na kujeruhiwa na waliopatwa na msiba.

Na mwisho wa hotuba yangu: ni kuomba radhi kwa kuona haya kutokana na sehemu yako - ewe Bwana wa Mitume! - kama wakikukosea kwa nafasi yako ya juu uliyonayo katika kumbukumbu yako nzuri, baadhi ya wajinga wenye mioyo migumu, ambao wako mbali na njia yako iliyonyooka, wale ambao uhalifu wao haujawazidishia kitu isipokuwa ni kuwa mbali na wewe, Dini yako pamoja na Sheria yako, basi tunaomba radhi - Mtume wa Mwenyezi Mungu - kutokana na uharibifu huu, ubaya huu na ukosefu wa adabu pamoja na kuchafua Ujumbe wako wa usamehevu… na baadaye watafahamu hawa waharibifu kwenye hii ardhi wenye kuritadi pale watakapokosa uombezi wako Siku ya Kiyama, ni mgeuko wa namna gani watakaogeukia.   

Ahsanteni sana kwa usikivu wenu nzuri.

Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yenu na Rehema zake na Baraka zake

 

Imetolewa: 11/mfungo sita / 1439H

Sawa na tarehe 29/ November / 2017

 

              Prof. Ahmad Al-Tayyib

                   Sheikh wa Al-Azhar    

 


([1]) Waislamu wanaviita vita vya “Nahawand” vilivyotokea mwaka wa 19H/640 kuwa ni “Ukumbozi  mkubwa”, kwani waliweza kulimaliza jeshi la mwisho la Wafursi wa Sassanids na kumalizika kwa dola hii… (Hussein Muunis: Atlas ya historia ya Uislamu, ukurasa wa 129). Ama kudondoka kwa dola ya Byzantine, kulikuwa ni kati ya miaka miwili wa 12 na 16H, nao ni mwaka wa kukabidhiwa Qudus kwa Umar (chanzo kilichopita, ukurasa wa 126).

([2]) At-Tabary, Kitabu cha Historia, juzuu ya tatu, ukursa wa 520.

Print
6524 Rate this article:
No rating

Please login or register to post comments.

أقسم بالله العظيم أن أكون مخلصًا لديني ولمصر وللأزهر الشريف, وأن أراقب الله في أداء مهمتى بالمركز, مسخرًا علمي وخبرتى لنشر الدعوة الإسلامية, وأن أكون ملازمًا لوسطية الأزهر الشريف, ومحافظًا على قيمه وتقاليده, وأن أؤدي عملي بالأمانة والإخلاص, وأن ألتزم بما ورد في ميثاق العمل بالمركز, والله على ما أقول شهيد.