Hotuba ya Kuaga ya Mtume ni Azimio la Kimataifa la Amani na Utulivu

  • | Monday, 26 June, 2023
Hotuba ya Kuaga ya Mtume ni Azimio la Kimataifa la Amani na Utulivu

  

Mtume (S.A.W.) alisimama akihotubia waumini, bali wanadamu wote kwenye siku ya Arafa katika Hijja ya Kuaga, ambapo alitoa maneno mazito ya kusisitiza namna ya kuishi baina ya wanadamu kwa amani na utulivu, siyo hiyo tu bali aliwaelezea walimwengu wote namna ya kuishi kwa amani pamoja na wanyama pia.

Katika hotuba hiyo Mtume Mohammed (S.A.W.) alitoa mawaidha makubwa kwa watu wake. Sentensi ya kwanza tu aliondosha mbele yake yote waliyokuwa nayo Waislamu kama vile unyang’anyi, uizi, kulipiza kisasi, na umwagaji wa damu, na paragrafu ya mwisho alisisitiza usawa kati ya muumini wa Kihabeshi na Khalifa wa Waislamu. Kwa hakika aliweka msingi mkubwa Ulimwenguni kwa ajili ya kuamiliana kwa uadilifu na ukarimu.

Miongoni mwa yaliyokuja katika hotuba yake Mtume (S.A.W.) kwamba alisema: “Enyi watu! Yasikilizeni maneno yangu kwa umakini! Hakuna ajuaye…huwenda mwaka huu ukawa wa mwisho kwangu kuwa hapa pamoja nanyi! Enyi watu! Kama ambavyo siku hizi, miezi hii na mji huu ni vitukufu, vivyo hivyo, uhai wenu, mali zenu na staha zenu ni vitukufu. Ni haramu kuvikiuka. Enyi Waislamu! Kesho, mtakutana na Mola wenu na kuhesabiwa kwa yale mnayoyatenda leo! Msirejee kinyumenyume kwenye mila zenu za zamani na kuchinjana nyinyi kwa nyinyi baada yangu! Jueni kwamba nitawatangulieni na kuwasubiri kwenye Birika (la Kawthar)! Nitajifakhiri kwa idadi yenu juu ya umma nyingine! Angalieni msinishushe chini (kwa kuangukia katika dhambi)!

Enyi Waislamu! Kila mwenye amana ya mtu airejeshe kwa mwenye nayo! Kila aina ya riba imefutwa; iko chini ya migu yangu. Bali mtu anatakiwa kurejesha mkopo. Usidhulumu wala usidhulumiwe! Sasa kujihusisha na riba kumeharamishwa kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Mambo yote yenye kuchukiza, yaliyokuwa yakifanywa katika zama za Ujahiliya, sasa yako chini ya miguu yangu. Riba ya kwanza ninayoifuta ni ile ya (ami yangu) Abbas ibn Abdulmuttalib.

Enyi Maswahaba! Uhasama wa enzi za Ujahiliya, nao umefutwa moja kwa moja. Taasubi ya kwanza ninayoifuta ni ile ya Rabia, mjukuu wa AbdulMuttalib.

Enyi watu! Leo shetani amepoteza nguvu yake ya kurejesha ushawishi na mamlaka yake katika hii ardhi yenu. Lakini, bado ataendelea kufurahi iwapo mtamfuata katika mambo ya upuuzi, mbali na yale ambayo nimeyafuta. Jiepusheni nayo pia ili kuilinda dini yenu!

Enyi watu! Chungeni haki za wanawake! Amilianeni nao kwa upendo na huruma! Ninawausieni kumcha Mwenyezi Mungu kuwahusu wanawake! Mmewachukuwa wanawake kama amana ya Mwenyezi Mungu; staha na heshima yao kwa jina la Mwenyezi Mungu! Mna haki juu ya wanawake, nao wana haki juu yenu! Haki mliyonayo juu ya wanawake ni kwamba wasiruhusu yeyote kuikanyaga heshima ya familia yenu! Haki ya wanawake juu yenu ni kuwa mnatakiwa kuwapa, kihalali, matumizi na mavazi. Hairuhusiwi kwa mwanamke kutoa kitu katika mali ya mumewe na kumpa mtu bila ruhusa yake.

Ama kuhusu watumishi wenu, walisheni katika vile mnavyokula nyinyi wenyewe na muwavike katika vile mnavyofaa nyinyi wenyewe. Wakifanya kitu ambacho hamuwezi kuwasamehe, basi waacheni waondoke! Lakini msiwaadhibu; kwa maana, nao ni waja wa Mwenyezi Mungu.

Enyi waumini! Sikilizeni maneno yangu na myazingatie vizuri! Muislamu ni ndugu wa Muislamu; hivyo Waislamu wote ni ndugu. Hairuhusiwi kudhulumu haki ya ndugu yako katika dini, labda kama ataitoa kwa ridhaa yake mwenyewe.

Enyi Waumini! Ninakuachieni amana, ambayo mkishikamana nayo hamtapotea kamwe. Amana hiyo ni Qur’an, Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Enyi watu! Muabuduni Mwenyezi Mungu! Tekelezeni swala tano za kila siku! Fungeni swaumu wakati wa mwezi wa Ramadhan na mtii maamrisho yangu! Hivyo mtaingia Peponi.

Enyi watu! Tahadharini na kupindukia hali ya kiasi! Kupindukia katika dini ndiyo sababu iliyowafanya waliokuwa kabla yenu kuangamia! Jifunzeni taratibu za hijja kutoka kwangu! Huwenda nisiweze kukutana nanyi tena hapa, baada ya mwaka huu! Wale waliopo wafikishe maneno yangu kwa wale ambao hawapo! Huwenda yule aliyefikishiwa akayaelewa vizuri zaidi na kuyalinda maneno yangu kuliko mfikishaji.”

Baada ya kusema maneno hayo, aliwauliza maswahaba zaidi ya laki moja na elfu ishirini waliokuwepo hapo: “Enyi watu…kesho mtaulizwa kuhusu mimi; mtasema nini?”
“Tunashuhudia kuwa ulitekeleza wajibu wako kama Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, ukatuonya na kutuusia”, umati wa waumini ulisema kwa pamoja.

Kufuatia ushuhuda huo wa Waumini, Mtukufu Mtume (s.a.w) akauliza mara tatu: “Je nimefikisha?” Maswahaba wote wakatoa kauli za ushuhuda, ndipo alipoinua mikono yake juu na kumuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awe shahidi:

“Shuhudia ewe Mola wangu! Shuhudia ewe Mola Wangu! Shuhudia ewe Mola wangu!”

Hotuba hii ya Kuaga ni sheria zinazoratibu mahusiano ya kijamii, mukhtasari wa mafunzo ya Uislamu na, wakati huo huo, ni mizani ya mwenendo na haki za binaadamu. Kabla ya uundwaji wa Azimio maarufu la Haki za Binaadamu, La Fayette, mwanafalsafa maarufu wa Kifaransa anayetambulika kuwa miongoni mwa waasisi na nguzo muhimu ya Mapinduzi ya Ufaransa ya mwaka 1789, baada ya kufanya utafiti wa kina kuhusu mifumo mbalimbali ya kisheria duniani, hatimaye alikutana na Hotuba ya Mwisho ya Mtukufu Mtume (s.a.w); na alipoiona kuwa inawakilisha misingi ya haki na uadilifu kwa wanadamu wote, akalazimika kukiria: “Ewe Muhammad Mwenye ukuu…! Umefikia kilele cha juu kabisa cha uadilifu kiasi kwamba hakuna mtu aliyekifikia na hakuna atakayekifikia!”

Katika Hotuba hiyo, Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) anaainisha kanuni ambazo wanadamu wanatakiwa kuzijua ili pasiwepo na udhuru kwa kutozijua. Umati mkubwa uliokuwepo uliwezesha yaliyomo katika Hotuba hiyo kuwafikia wanadamu wote.

 

Print
Categories: Makala
Tags:
Rate this article:
No rating

Please login or register to post comments.