Kumfuata Mtume wa Rehma (S.A.W.) na Athari zake kwa mtu na jamii

  • | Saturday, 23 September, 2023
Kumfuata Mtume wa Rehma (S.A.W.) na Athari zake kwa mtu na jamii

 

     Inaeleweka kwamba kila umma una kiongozi wake anayefuatwa na kutiiwa katika mambo yote ya maisha. Pia, kila mwanadamu huwa na ruwaza wake ambaye ni kiongozi wake anayemfuata na kutaka kuwa mfano wake katika maisha yake barabara.

Kwa kutambua ukweli huu, sisi waislamu tuna kiongozi wetu ambaye ni kiongozi bora zaidi kuliko wanadamu wote, ni Mtume wetu Mohammed (S.A.W.) aliyesifiwa na Mola wake Mwenyezi Mungu (S.W.) kwa kusema: {Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume waMwenyezi Mungu kwa anaye mtaraji Mwenyezi Mungu naSiku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana} Al-Ahzaab: 21.

Kwa hakika, hikima ya Mwenyezi Mungu (S.W.) imelazimika kuwa Mtume awe mmoja wa wanadamu, siyo mmoja wa Malaika walioridhishwa na Mwenyezi Mungu wala mashetani waliolaaniwa, Mwenyezi Mungu Amesema: "Na wao husema: Mbona hakuteremshiwa Malaika? Na kama tungaliteremsha Malaika, basi bila ya shaka ingeshahukumiwa amri, tena hapo wasingelipewa muhula" [Al-Anaam: 8], kwa hiyo, Mtume (S.A.W.) amejitambua akisema: "Sema: Mimi ni mwanaadamu kama nyinyi" [Al-Kahf: 110], kwa kweli Mwenyezi Mungu (S.W.) hakumfanya Mtume wetu ni mwanadamu kama sisi ila kwa ajili ya kumfuata na kumfanya mfano wa kuigwa kwa urahisi, kwani Mwenyezi Mungu (S.W.) Angemchagua Mtume miongoni mwa Malaika basi watu wangetatizwa kumfuata na kufanya kama anavyofanya yule Malaika tena wange na hoja juu ya Mwenyezi Mungu (S.W.) kwa ugumu wa kumfuata Mtume wa Malaika na kutekeleza sunna yake, lakini ukweli ni kwamba Mtume ni mmoja wa wanadamu aliyepewa jukumu la kufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu (S.W.) kwa waja wake, kwa hiyo watu wanapaswa kumfuata na kwa hakika umma wakitekeleza yaliyomo aya hii wangefurahia milele na kupata mafanikio na kujiokoa kutoka adhabu na mateso duniani na akhera.

Kwa hakia kumfuata Mtume ni kazi yenye manufaa mengi na athari njema sawa kuhusu ulinginiaji au mlinginiaji, ambapo mlinginiaji anaemfuata Mtume ni yule anaewaita na kulingania watu kwa njia ya Mwenyezi Mungu kwa kutegemea busara na hikima akiwa na ukweli na umakini wa kazi yake ya ulinginiaji, akiwa na imani na ibada sahihi, tabia njema na matendeano mema, basi yeyote anayo sifa hizo na hali hiyo, basi hufanikiwa katika kazi yake ya ulinginiaji, tena huwaathiria vema wafuasi wake kwa kuwaongoza kwenye njia iliyo sahihi kwa mawaidha na maelekezo yake, ilhali ambaye huwa kinyume na hayo akawa na imani na ibada batili, tabia mbaya na vitendo vibaya, kazi yake hufeli kabisa na mawaidha yake hukataliwa na watu.

Kwa kweli Mtume ndiye mfano bora na ruwaza wa umma, lakini wakati huo huo Mtume huwa na baadhi ya sifa maalumu ambazo ni sifa zake hasa haifai kuigiwa katika sifa hizo, sifa na hali hizo ni kama vile; kuwaoa wake kuliko wanne, na kufunga saumu kwa muda wa siku kadhaa mfululizo, hata hivyo Al-Bukhari ametaja kutoka kwa Abu Huraira (R.A.) kutoka Mtume (S.A.W.) kwamba amesema: {Msifungeni Saumu kwa muda wa siku kadhaa mfululizo, akakariri hayo mara mbili, maswahaba wakasema: Ewe, Mtume wewe unafanya hivyo, akasema: hakika mimi napata chakula na maji kutoka kwa Mola wangu Mlezi, lakini nyinyi fanyeni kulingana na uwezo wenu tu}.

Pia, Mtume (S.A.W.) amewaamrisha waislamu wamfuate katika mambo ya sheria tu, ama mambo mengine ya dunia basi watu huwa na maarifa na ujuzi zaidi kuhusu hali zao za dunia, Muslim amesimulia kutoka kwa Anas (R.A.) kwamba Mtume (S.A.W.) siku moja aliwapitia watu waliokuwa wanakata mitende kwa ajili ya kulima mingine, akawaambia: msingalifanya ingalikuwa bora na mngalipata tende nyingi na nzuri, akasema (msimulizi): mitende yao ikaoza na haikutoa tende kabisa kwa sababu ya waliyoyafanya kwa kumfuata maelekezo ya Mtume, kisha Mtume akawapitia tena akawauliza: mbona mitende yenu haikutoa tende?! wakamjibu: tulikufuata tu, akawaambia: nyinyi mnajua zaidi mambo yenu ya dunia}, maana watu hawa walipofuata maelekezo ya Mtume wakijua kuwa bora kutofanya hivyo wakapata hasara, lakini funzo ni kwamba mtu anatakiwa kumfuata Mtume katika mambo ya dini na sheria, lakini mambo ya dunia huenda mtu ana ujuzi zaidi kuliko Mtume kuhusu jambo fulani basi hufuata ujuzi na maarifa yake.

Kwa hakika Mtume wetu Mohammed (S.A.W.) ametufundisha namna ya kuwa na huruma na rehma kwa watu, bali kwa wanyama na viumbe wote wa Mwenyezi Mungu, kwa hiyo Qurani Takatifu imesisitiza kwamba rehma ya Mtume siyo hasa kwa waumini wala waislamu tu, bali ni rehma ya kujumla, rehma inayoenea na kupaa malimwengu yote kwa mujibu wa kauli yake Mwenyezi Mungu (S.W.): {Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwawalimwengu wote} Al-Anbiyaa: 107.

Kwa hiyo, sote tunatakiwa kuwa na rehma na huruma kwa viumbe wote wala tusiwe na chuki, upumbavu, ugumu kwa wengine hata wakiwa wasio waislamu, kwa kuwa rehma ni msingi mmojawapo misingi maalumu ya dini yetu adhimu ambayo inaitambua dini ya Uislamu, dini ya rehma na Mtume wa Rehma kwa dunia nzima.

 

Print
Categories: Makala
Tags:
Rate this article:
No rating

Please login or register to post comments.