Kuzuia Unyanyasaji na Ukatili dhidi ya Wanawake Barani Afrika jukumu la kijamii na wajibu wa kidini

Imeandaliwa na Dkt. Ahmed Khalaf Abulfadl

  • | Sunday, 1 October, 2023
Kuzuia Unyanyasaji na Ukatili dhidi ya Wanawake Barani Afrika jukumu la kijamii na wajibu wa kidini

      Kwa hakika, unyanyasaji wa wanawake ni tatizo kubwa linalosumbua ulimwengu wote hasa barani Afrika. Takwimu zinaonyesha kuwa mwanamke mmoja kati ya wanawake watatu barani Afrika amepatwa na unyanyasaji wa kijinsia katika maisha yake. Sura za unyanyasaji wa kijinsia zinazopatikana barani Afrika ni pamoja na ubakaji, unyanyasaji wa kingono, ndoa za mapema na za kulazimishwa, na ukeketaji wa wasichana.

Kuna sababu nyingi zinazochangia kuenea kwa unyanyasaji wa wanawake barani Afrika, miongoni mwa sababu hizo ni:

  • Mfumo dume: Utamaduni wa mfumo dume unaowapa wanaume nguvu na ukuu zaidi kuliko wanawake huchangia katika unyanyasaji wa wanawake. Katika jamii za mfumo dume, wanawake mara nyingi huonekana kama mali ya wanaume na wananyimwa haki zao za msingi.
  • Umaskini: Umaskini unaweza kuwafanya wanawake kuwa hatarini zaidi kwa unyanyasaji. Wanawake wanaoishi katika hali duni ya kiuchumi wakiteseka umaskini mara nyingi huwa hawana rasilimali za kujilinda kutokana na unyanyasaji.
  • Ukosefu wa elimu: Ukosefu wa elimu unaweza kuwafanya wanawake wasijue haki zao na wasijue namna ya kujilinda kutokana na unyanyasaji au hata kudai haki zao wakipatwa na unyanyasaji wa aina yoyote.
  • Ukosefu wa sheria na sera zinazolinda wanawake: Katika baadhi ya nchi za Afrika, sheria na sera zinazolinda wanawake dhidi ya unyanyasaji hazipatikani au hazitekelezwi.

Baada ya kuashiria sababu na vyanzo vya tabia hii, tunapenda kueleza hatua kadhaa zinazoweza kuchukuliwa ili kuzuia unyanyasaji wa wanawake barani Afrika. Hatua hizi ni pamoja na:

  • Kuelimisha jamii kuhusu unyanyasaji wa kijinsia: ni muhimu kuwaelimisha watu kuhusu unyanyasaji wa kijinsia, jambo linaloweza kusaidia kubadilisha mitazamo iliyosambaa kuhusu unyanyasaji wa kijinsia na kuhamasisha watu kuchukua hatua zaidi za kuuzuia uhalifu huu.
  • Kuimarisha sheria na sera zinazolinda wanawake: Sheria na sera zinazolinda wanawake dhidi ya unyanyasaji ni muhimu kwa kuwapa wanawake haki na usalama, hapo tunaashiria kuwa tatizo si lazima lihusiane na kutunga sheria tu, bali kuitekeleza na kuwajibika nazo.
  • Kukuza na kuimarisha usawa wa kijinsia: Kuendeleza usawa wa kijinsia husaidia kupunguza unyanyasaji wa wanawake kwa kuwapa wanawake nguvu na uhuru zaidi.
  • Kutoa rasilimali kwa waathiriwa wa unyanyasaji: Rasilimali kama vile yawe makazi, ushauri, na matibabu ya kimwili zinaweza kusaidia waathiriwa wa unyanyasaji kupona na kuendelea na maisha yao.

Hata hivyo, yapo mashirika mengi yanayojihusisha na kuzuia unyanyasaji wa wanawake barani Afrika. Mashirika hayo yanafanya kazi katika viwango mbalimbali, kuanzia elimu ya jamii hadi kutoa huduma kwa waathiriwa wa unyanyasaji.

Kwa kweli, kuzuia unyanyasaji wa wanawake ni kazi ngumu, lakini ni muhimu na la dharura. Kwa kuchukua hatua za kuelimisha jamii kuhusu unyanyasaji wa kijinsia, kuimarisha sheria na sera zinazolinda wanawake, na kukuza usawa wa kijinsia, tunaweza kushirikiana kuunda dunia ambapo wanawake wanaishi bila ya hofu ya kupatwa na unyanyasaji wa aina yoyote.

Ama kuhusu mtazamo wa Uislamu kuhusiana na unyanyasaji wa wanawake, basi Uislamu una mtazamo wazi dhidi ya unyanyasaji wa wanawake, ambapo Qur'an imewahimiza wanaume kuwatendea wake zao kwa wema, uadilifu na huruma. Mwenyezi Mungu (S.W.) Amesema:

{Wanaume ni wasimamizi wa wanawake, kwa kufadhiliwa na Mwenyezi Mungu baadhi yao juu ya baadhi, na kwa mali yao wanayo yatoa.} (4:34)

{Na kaeni nao kwa wema}. (4:34)

{Wakikut'iini msiwatafutie njia ya kuwaudhi bure}. (33:30)

Naye, Mtume Muhammad (S.A.W.) pia alitoa mafundisho kadhaa dhidi ya unyanyasaji wa wanawake. Alisema katika Hijja ya kuaga: (Ninawasihi muwatendee wanawake wema, kwani wao ni mama zenu, binti zenu, na dada zenu, kwa hivyo wahurumieni, wahurumieni mayatima wao, wala msiwadhulumu, wala msiwapige, wala msiwatusi.)

Na alisema: (Aliye bora wenu ni yule aliye bora kwa familia yake, na mimi ni bora kuliko wote kwa familia yangu.(

Naye Bibi Aisha (R.A.) alisema: “Mtume Muhammad (S.A.W.)  hakuwahi kumpiga mtu kwa mkono wake, akiwa mwanamke, au mtumwa, isipokuwa katika jihadi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Pia, hakuwahi kulipiza kisasi kutoka aliyemkosea, isipokuwa ikiwa kitu cha haramu kwa Mwenyezi Mungu kilikiukwa, basi angelipiza kisasi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu”

Sisi katika Kituo cha Al-Azhar cha kupambana na fikra potofu tunaona kuwa unyanyasaji wa wanawake kwa sura zake zote ni ugaidi ulio wazi, ambapo husababisha madhara makubwa kwa jamii nzima; maana mwanamke ndiye sababu ya kufanikisha mikakati ya maendeleo na juhudi za kuleta ustawi na utulivu katika jamii yoyote, kwa hiyo tunatoa wito wa kupambana na tabia hiyo mbaya kwa lengo la kuzuia tabia hiyo na kuepukana na athari zake hatari kwa mtu na jamii.

Print
Categories: Makala
Tags:
Rate this article:
No rating

Please login or register to post comments.