Kuwatisha Watalii na wenye ahadi ya amani kwa Mtazamo wa Uislamu

Imeandaliwa na Dkt. Alaa Salah Abdulwahed

  • | Wednesday, 11 October, 2023
Kuwatisha Watalii na wenye ahadi ya amani kwa Mtazamo wa Uislamu

     Kwa hakika anayeangalia hali ya siku hizi hatakuwa na ugumu wowote kutambua kuwa njia ya kuingia kwa watalii kwenye nchi za kiislamu inakuja chini ya dhana ya amani inayojulikana katika sheria ya kiislamu, jambo linalofanya zoezi la kuingia kwao ni zoezi lisilo na pingamizi yoyote kisheria. Kwa hiyo, haijuzu washambuliwe wala kutishwa au kuhofishwa kwa namna au sababu yoyote, kwani amani ambayo ni ahadi ipo na mfano wake pia ipo, kwa hiyo kisheria wana haki ya kuwa na amani wakti wa kuwapo kwao nchini.

Kwa kubainisha hayo, tukiangalia kibali cha kuingia nchi kwa asiye mwananchi ambayo ni “Visa” tunaelewa kuwa mtalii haruhusuwi kuingia humo ndani nchi ila akipata ile “Visa” kwa hiyo huwa na amani, kwa maneno mengine huwa na mkataba wa amani baina yake na nchi anapoingia hasa akiwa na mwaliko wa kufanya ziara au kazi maalumu ambapo yule mgeni husikia amani juu ya nafsi yake na mali zake kwa kushika mkataba huu mkononi mwake. Pia, haikubalika kuwa mgeni atakubali kutembelea nchi fulani akiwa hana amani juu ya nafsi na mali yake, hali hii inamaanisha kuwa mtalii au mgeni kwa jumla anayeamua kutembelea nchi yoyote ya kiislamu huwa na haki ya kutetewa na awe na amani na utulivu kwa mujibu wa kauli ya Mwenyezi Mungu (S.W.): {Na ikiwa mmoja wapo katika washirikina akikuomba ulinzi, basi mpe ulinzi apate kusikia maneno ya Mwenyezi Mungu. Kisha mfikishe pahala pake pa amani. Haya ni kwa kuwa hao ni watu wasiojua kitu} [9/6].

Na katika Sunna Mtume (S.A.W.) alisema: “Ahadi ya waislamu ni moja, mmoja wao akitoa ahadi basi wote wanatakiwa kuitimiza” kwa maana hii kuwapa watalii amani na ahadi ni haki ya kila mwislamu bila ya kujali madaraka au cheo chake au jinsia, ambapo husihi kutoka mtawala na kutoka watu wa kawaida. Kwa kueleza haya Ibnu Qudamah Al-Maqdisiy amesema: Hali hii inamaanisha kuwa amani ikipewa kwa watu wenye ahadi na waislamu basi haijuzu kuwaua wala kuwatishia wala kuwaudhi katika nafsi, mali wala makazi na kwamba kutoa ahadi inakubaliwa kutoka kila mwislamu mwenye mamlaka ya kujiamua mwanamume au mwanamke, bwana au mtumwa. Maoni haya yamekubaliwa na Al-Thawriy, Al-Awzaiy, Al-Shafiiy, Isak na wengi wa wataalamu.

Na tukiangalia hukumu na haki zinazofuata kupewa kibali cha kuingia nchi yaani; “Visa” tunaona kwamba ni sababu ya kumpa yule mgeni amani yake na wakati huo huo ni mkataba wa kumlinda yule mgeni kutokana na madhara yoyote. Wanachuoni wa Fiqhi na sheria ya kiislamu walitaja namna na njia mbalimbli za kuomba na kupewa amani kwa mgeni nchini mwa waislamu, miongoni mwa njia na namna hizo kupata kibali cha kuingia nchi kwa hiyo, watalii wa uraia wowote wana haki ya kupewa amani madamu hawakufanya uharibifu wala kusababisha ghasia au ufisadi nchini. Kama kawaida yake katika masuala ya aina hii, sheria ya kiislamu hupanua katika mambo yanayochangia kuzuia umwagaji wa damu wala hata vitisho au vurugu.

Kwa kuwa dini ya Uislamu ni dini ya amani na usalama inayohimiza utulivu, upendo na undugu, haikubaliki kuwa dini hiyo hiyo inawaruhusia wafuasi wake kuwaudhi wagenu wao hata wakiwa si waislamu kwa madai ya kwamba hawana ahadi wala amani kwa mujibu wa fikra za wachache wa waislamu wasio na elimu ya kutosha wala hawana uelewa ulio sawa kwa sheria na vyanzo vyake.

Kinyume na hayo, wae watalii wanatakiwa kusaidiwa na kupokelewa vema kwani wanatembelea nchi za kiislamu kwa ajili ya kuzinufaisha nchi hizo na wananchi wake kiuchumi, na pengeni baadhi yao huamua kujiunga na Uislamu kama inavyotukia mara kwa mara. Kuna kanuni na vidhibiti maalumu vya nchi, dini, jamii katika nchi za kiislamu na wala haikubaliki kuwa mtalii aliyekuja akizingatia na kufuata zile taratibu na kanuni apatwe na maovu au vitisho kwa sababu yoyote. Mtume (S.A.W.) alikuwa anawapokea wajumbe kutoka pande mbalimbali na kutuma maswahaba wake kwa nchi na mamlaka kadhaa duniani kwa lengo la kueneza ujumbe wa Uislamu, haikutokea kuwa waislamu walitishia wageni wao au kusababisha uharibifu katika nchi yoyote, bali walikuwa wajenzi wa staarabu mbalimbali duniani na mfano bora wa mwanadamu mwenye manufaa kwa watu wote.

Kutokana na hayo tunasisitiza kuwa Uislamu umeharamisha kuwatisha watalii na wageni, bali watu kwa jumla kwa sababu yoyote isipokuwa kufanya uharibifu au uadui dhidi ya waislamu, ama kuwatisha wageni hakuafikiani na mafundisho ya Uislamu hata kidogo.

 

Print
Categories: Makala
Tags:
Rate this article:
No rating

Please login or register to post comments.