Je, Umefuzu katika Ramadhani?!

Imeandaliwa na Dkt.; Alaa Salah Abdulwahed

  • | Sunday, 7 April, 2024
Je, Umefuzu katika Ramadhani?!

 

 

     Mwezi mtukufu wa Ramadahni umekaribia kuisha, ambapo waislamu mwishoni mwa mwezi huu mtukufu huwa katika makundi mawili; waliojikurubisha kwa Mwenyezi Mungu wakajitahidi katika ibada na kutumia wakati mwingi kusali na kufanya ibada kwa ajili ya Mwenyezi Mungu wakiwa wametakasika saumu yao kutoka dosari yoyote, na wengine waliopoteza muda mwingi kuangali T.V. na kulala na kushughulikia mambo yasiyotakiwa katika mwezi huu mtukufu.

Katika hali hii kila mmoja wetu anatakiwa kujiuliza: Je, amefuzu katika Ramadhani au la? Kwa kufuzu Ramadhani kwa mwislamu huwa anastahili malipo mema ya Mwenyezi Mungu na furaha ya Eid pamoja na furaha ya baadaye atakapofufuliwa kwa ajili ya kuamuliwa hatima yake aende peponi au motoni. Ama wale waliopoteza mwezi wakajizuia mema na baraka zake huwa wamefeli na kupata hasara kubwa mno, maana hawajui kama watapata fursa ya kushuhudia mwezi huu mwakani au la.

Mwislamu mwenye akili nzuri hana budi kuwekeza katika mwezi mtukufu wa Ramadhan kupitia mema na ibada mbalimbali, ambapo mwezi huu ni fursa ya pekee ya kufanya biashara yenye faida kubwa mno isiyo na mfano, biashara hiyo haileti mapato ya fedha lakini ni ghali zaidi kuliko fedha na dhahabu.

Ni biashara ya kupata radhi na maghufira kutoka kwa Mwenyezi Mungu (S.W.), biashara ambayo faida na malipo yake hayana mfano kabisa, ni upepo mwenye upana unaofanan na upana wa mabingu na ardhi imeandaliwa kwa wachamungu.

Bila shaka, Mwenyezi Mungu (S.W.) Alipoainisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan uwe mwezi bora kuliko miezi yote Alikuwa na hekima ya kufanya hivyo, pengine hekima hiyo ni pamoja na kueleza kuwa mwezi huu ni fursa adhimu ya kupata rehema, radhi na maghufira ya Mwenyezi Mungu (S.W.)

Kwa kuangalia fadhila za mwezi huu mtukufu tunaona kuwa una mambo kadhaa yanayoufanya ni mwezi bora kuliko yote, kwa hiyo waislamu wanatakiwa kutumia nafasi ya kuja kwa mwezi huu ili watafute thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kwa hakika Mwenyezi Mungu (S.W.) Ameuelezea mwezi mtukufu wa Ramadhani ni mwezi bora kuliko miezi yote kwa kuwa Qurani imeteremka ndani ya mwezi huu unao usiku ulio bora zaidi kuliko miezi elfu moja nao ni usiku wa Al-Qadr.

Kwa mujibu wa Qurani Tukufu Mwenyezi Mungu Amebainisha kuwa Qurani imeteremka katika mwezi huu: {Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur'ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo waziza uwongofu na upambanuzi. Basi ataye kuwa mjini katika mwezi huu na afunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushukuru} [Al-Baqara: 185].

Hebu tujaribu kutaja baadhi ya fadhila za mwezi wa Ramadhani Mtukufu, ambapo katika mwezi wa Ramadhwaan kuna fadhila nyingi ambazo ni:

Ni mwezi wa Qurani kama Alivyosema Allaah Mtukufu: {Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur'ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo waziza uwongofu na upambanuzi.} [Al-Baqara: 185]. 

Vilevile kama ilivyopokewa na Ibn 'Abbaas (radhiya Allaahu 'anhu) kuwa makusudiyo yake   kwa hakika kuteremshiwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) Qur-aan mwanzo ni katika mwezi wa Ramadhwaan na vilevile Qur-aan mwanzo wa kuteremka ni usiku wa Laylatul-Qadir na Laylatul-Qadir iko katika mwezi wa Ramadhwaan. Hivyo basi ni juu yetu kufanya juhudi katika mwezi huu kukithirisha sana kusoma Qur-aan.

Mwezi wa kujifunza subira ambayo ni katika jambo gumu na halipati ila kwa mtu mchaji Allaah na mnyenyekevu kwa Allaah. Na katika kufunga kunatakiwa subira pale mtu anapojizuilia kutokana na kutokula, kunywa, matamanio na mengineyo. Imekua Swawm ni nusu ya subira na subira malipo yake ni pepo. 

Na mwezi wa kuomba maghufira kwa mujibu wa ilivyokuja katika Hadiyth iliyopokelewa na Maimamu wawili:

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) amesema, "Pindi inapokuja Ramadhwaan inafunguliwa milango ya pepo, na hufungwa milango ya moto, na mashetani wanafungwa kwa Minyororo." [mesimuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim]

 Kwa hakika utaona katika mwezi huu watu wengi wanajitahidi kujiepusha na maasi, watu wanajaa misikitini kwa kufanya ibada ya mwezi huu hii ni kwa sababu mashetani wamefungwa na shetani juu ya uasi wake lakini anauogopa mwezi wa Ramadhwaan na vitimbi vyake vinakuwa dhaifu ndio mana wengi nyoyo zinabadilika wanaswali  na kujitahidi kufanya kheri.  Lakini ikimalizika Ramadhwaan tu basi Swalah imekwisha kama vile Allaah yupo Ramadhwaan tu. Huu ni msiba ndugu zangu Waislamu Allaah Asitujaalie katika hao.

Kwa hakika mwezi wa Ramadhan ni soko lakini si soko la biashara ya kawaida, bali ni soko muhimu lenye manufaa makubwa makubwa na heri isiyo na mfano duniani na Akhera, kwa hiyo tumetahadharishwa na Mtume (S.A.W.) tusipoteza fursa ya Mwezi huu bila ya kustahiki maghufira na radhi ya Mwenyezi Mungu (S.W.).

Print
Categories: Makala
Tags:
Rate this article:
No rating

Please login or register to post comments.