Misingi ya Kuishi Pamoja kwa Amani kwa Mujibu wa Sheria ya Kiislamu

Imeandaliwa na Dkt.; Alaa Salah Abdulwahed

  • | Thursday, 16 May, 2024
Misingi ya Kuishi Pamoja kwa Amani kwa Mujibu wa Sheria ya Kiislamu

     Kwa kweli kutofautiana kidini na kiitikadi siyo sababu ya kumzuia mwislamu kuishi na kuamiliana na wengine wasio waislamu kwa wema na amani, kwani Mwenyezi Mungu Aliwahimiza waislamu kuamiliana na watu wote kwa wema na hisani madamu hawakuwafanyia waislamu uadui wala bughudha, Mwenyezi Mungu Amesema: {Wala kuwachukia watu kwa kuwa wali- kuzuilieni kufika Msikiti mtakatifu kusikupelekeeni kuwafanyia uadui. Na saidianeni katika wema na uchamngu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Mwenyezi  Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu} [5/2].

Qurani Takatifu kupitia aya kadha wa kadha imesisitiza kuwa waislamu wanatakiwa kuwa na mahusiano mazuri na watu wa dini na itikadi mbalimbali kwani kuna mambo ya pamoja yanayostahiki kuchungwa na wote waislamu na wasio waislamu kwa msingi wa kushirikiana na kukamilishana kwa ajili ya manufaa ya ulimwengu kote. Kwa kweli Uislamu ulikuja ili kuimarisha mahusiano baina ya watu siyo kwa kuyakata yale mahusiano na kupigana nayo.

Jambo la kusisitiza hilo ni alilolifanya Mtume (S.A.W.) katika Suluhu ya Al-Hudaybiya ambapo alifunga mkataba wa amani wa kwanza kabisa baina ya waislamu na washirikina kwa msingi wa kuheshimiana na kuamiliana kwa wema kwa lengo la kuisha pamoja kwa amani na utulivu na kuendeleza jamii na kuilinda nchi. Ingawa masharti ya mkataba huo yalionekana yanawadhulumu waislamu na kupendeleza washirikina lakini Mwenyezi Mungu Aliuita ushindi kama ilivyokuja katika kauli yake (S.W.): { Hakika tumekufungulia Ushindi wa dhaahiri * Ili Mwenyezi Mungu akusamehe makosa yako yaliyotangulia na yajayo, na akutimizie neema zake, naakuongoe katika Njia Iliyo Nyooka * Na Mwenyezi Mungu akunusuru nusura yenye nguvu} [48/1-3].

Hali hii inathibitisha kuwa Uislamu ndio dini ya amani na utulivu siyo dini ya ugaidi na vurugu, tena baada ya suluhu hilo ilitokea vita vya Khaybar baina ya waislamu na mayahudi na Mtume ameweka mkataba mwingine na mayahudi kwa ajili ya kuzilinda nafsi na damu za pande mbili, pia kuanzia mwaka wa saba baada ya hijra ya Mtume misafara ya mabalozi wa waislamu waliokuwa wanatumwa na Mtume huku na huku ili kueneza ujumbe wa amani na kuanzisha mahusiano na mataifa mbalimbali kwa lengo la kuthibitisha kuwa dini hiyo ni dini ya amani na upendo.

Mtume (S.A.W.) alikubali zawadi alizozipata kutoka wafalme wa umma nyingine kama vile; Al-Najashiy mfalme wa Uhabashi akawafanyia wajumbe wa mfalme yule ukarimu mkubwa akisema: "Hakika watu hawa waliwafanyia maswahaba zetu ukarimu mkubwa". Inatajwa pia kwamba Uislamu unawahimiza waumini wahifadhi mahusiano yao wenyewe kwa wenyewe na kuwafananisha kwa mwili mmoja kama ilivyokuja katika hadithi ya Mtume: "Kwa kweli mfano wa waumini katika upendo na huruma wao wenyewe kwa wenyewe ni kama mwili mmoja kama kiungo kimoja kinauma basi mwili mzima huumwa na kutaabika kwa maumivu ya kiungo hicho".

Kwa kuangalia ibada ambazo waislamu wanatakiwa kuzifanya kwa ajili ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, tunaona kuwa ibada hizo zote zinawataka waislamu wawe na umoja na mshikamano, angalieni Swala namna inawalazimisha waislamu wote wasimame pamoja katika mstari mmoja bila ya kumbagua yeyote wote wanasimama kwa namna moja, wanaelekea Qibla moja, wanamwomba Mola Mmoja, wanafanya tendo moja, wakati mmoja. Na katika Hajj wote wanava mavazi haya haya wakielekea mahali pale pale, hamna tofauti baina ya mmoja na mwingine kwa sababu ya utajiri wala kabila wala uraia wala lugha wala rangi. Zaidi ya hapo, Mwenyezi Mungu Amebainisha kuwa umma huu ni umma mmoja tu kama Alivyoeleza katika kauli yake: {Na fanyeni juhudi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kama inavyo stahiki jihadi yake. Yeye amekuteueni. Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika Dini. Nayo ni mila ya baba yenu Ibrahim. Yeye (Mwenyezi Mungu) alikuiteni Waislamu tangu zamani, na katika hii (Qur'ani) pia, ili awe Mtume shahidi juu yenu, na nyinyi muwe mashahidi kwa watu. Basi shikeni Sala na toeni Zaka na shikamaneni na Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye Mlinzi wenu, Mlinzi bora kabisa, na Msaidizi bora kabisa} [22/78].

Na kwa ajili ya kusisitia uzito wa uhusiano huo, Mwenyezi Mungu Aliwaita waislamu ni ndugu hata wakikhitilafiana au hata kugongana: {Hakika Waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemewe} [49/10]. Maana waislamu ni ndugu wenyewe kwa wenyewe haikubaliki kutukia migongano baina yao wa chuki wala bughudha wala mfarakano hata kidogo. Sio waislamu tu, bali Qurani ilibainisha kuwa watu wote wanatakiwa kuwa na umoja na watambue kuwa asli yao wote ni moja naye ni Adam (A.S.) maana nasaba ya wanadamu wote inatokana naye, kwa hiyo mapigano na vita vinavyotukia hapa na kule hayana maana wala hayahusiani na dini yoyote wala akili, bali ushawishi na ulaghai wa kueneza maovu na maangamizi.

Vile vile, Uislamu uliwatahadharisha waislamu kutodharauliana katika kauli yake Mwenyezi Mungu (S.W.): {Enyi mlio amini! Wanaume wasiwadharau wanaume wenzao, wala wanawake wasiwadharau wanawake wenzao. Huenda hao wakawa bora kuliko wao. Wala msivunjiane hishima, wala msiitane kwa majina ya kejeli. Ni uovu kutumia jina baya baada ya kwishaamini. Na wasio tubu, hao ndio wenye kudhulumu} [49/11] Na katika sura ile ile Mwenyezi Mungu Alitaja wazi wazi kipengele cha kusanifisha watu na kuwapa vyeo tofauti Akielezea kuwa ucha Mungu ndio kipengele cha kupendelezana baina ya watu kwa kusema: {Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana namwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliyemchamngu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari} [49/13].

Kwa hakika aya hiyo ya mwisho inatwelezea mengi kuhusu lengo la kuumbwa kwa wanadamu na hikima ya kuwa tofauti na pia matakwa ya Mwenyezi Mungu kutoka kwa waja wake, hayo ndiyo yaliyosisitizwa na ustaarabu wa kiislamu kupitia enzi zake zote.

 

Print
Categories: Makala
Tags:
Rate this article:
4.5

Please login or register to post comments.