Uislamu ni dini ambayo imejulikana kwa wepesi wake na msamaha wake siyo kwa wafuasi wake tu, bali kwa wanadamu kwa jumla. Dini hiyo imempa mwanadamu haki ya kujiamua na kuchagua dini anayoifuata na itikadi anayoishikilia.
Uhuru wa itikadi ni msingi muhimu miongoni mwa misingi ya dini hiyo adhimu kwa mujibu wa kauli yake Mwenyezi Mungu (S.W.): {Hapana kulazimisha katika Dini. Kwani Uwongofu umekwisha pambanuka na upotofu. Basi anaye mkataa Shet'ani na akamuamini Mwenyezi Mungu bila ya shaka amekamata kishikio madhubuti, kisicho vunjika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua} [2/256].
Kulingana na misingi ya Uislamu na mafunzo yake kutofautiana kikabila, kitikadi, kilugha, kitabia n.k. ni maumbile yanayokubalika katika Uislamu kwa hikima ya Mwenyezi Mungu (S.W.) Aliyesema katika kitabu chake kitakatifu: {Na Mola wako Mlezi angeli penda ange wafanya watu wote wakawa umma mmoja. Lakini hawaachi kukhitalifiana * Isipo kuwa wale ambao Mola wako Mlezi amewarehemu; na kwa hiyo ndio Mwenyezi Mungu amewaumba. Na litatimia neno la Mola wako Mlezi: Kweli kweli nitaijaza Jahannam kwa majini na watu pamoja} [11/118-119].
Pia, Uislamu uliwapa watu uhuru wa kuchagua dini na kufuata sheria ambayo wataridhika nayo kwa kuwa masuala ya itikadi yanafungamana na uelewa wa mtu mwenyewe na imani yake. Mwenyezi Mungu Amesema: {Na sema: Hii ni kweli itokayo kwa Mola wako Mlezi. Basi atakaye, aamini. Na atakaye, akatae} [18/29], tena Mwenyezi Mungu Amemwambia Mtume wake (S.A.W.) kwamba hana mamlaka ya kuwalazimisha watu kuamini ujumbe wake kwani jukumu lake linaishia kuwaambia na kuwaita kwenye njia ya Mwenyezi Mungu na kama watakubali basi ni vema ama wakikataa basi hakuna mamlaka kuwalazimisha na kuwafaradhishia dini. Maana hizo zinaelezwa katika kauli ya Mwenyezi Mungu (S.W.): {Angeli taka Mola wako Mlezi wangeli amini wote waliomo katika ardhi. Je, wewe utawalazimisha watu kwa nguvu mpaka wawe Waumini?} [10/99] na kauli yake (S.W.): {Basi kumbusha! Hakika wewe ni Mkumbushaji * Wewe si mwenye kuwatawalia} [88/21-22].
Zaidi ya hayo, Mtume aliamrishwa katika Qurani aachane na wale waliotangaza kukufuru kwa aliyokuja nayo mpaka amri hiyo imerudiwarudiwa katika suratul Kafiruun: {Sema: Enyi makafiri!* Siabudu mnacho kiabudu * Wala nyinyi hamuabudu ninaye muabudu * Wala sitaabudu mnacho abudu * Wala nyinyi hamuabudu ninaye muabudu * Nyinyi mna dini yenu, nami nina Dini yangu} [109/1-6].
Kwa kweli kutofautiana kidini na kiitikadi siyo sababu ya kumzuia mwislamu kuishi na kuamiliana na wengine wasio waislamu kwa wema na amani, kwani Mwenyezi Mungu Aliwahimiza waislamu kuamiliana na watu wote kwa wema na hisani madamu hawakuwafanyia waislamu uadui wala bughudha, Mwenyezi Mungu Amesema: {Wala kuwachukia watu kwa kuwa wali- kuzuilieni kufika Msikiti mtakatifu kusikupelekeeni kuwafanyia uadui. Na saidianeni katika wema na uchamngu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu} [5/2].
Qurani Takatifu kupitia aya kadha wa kadha imesisitiza kuwa waislamu wanatakiwa kuwa na mahusiano mazuri na watu wa dini na itikadi mbalimbali kwani kuna mambo ya pamoja yanayostahiki kuchungwa na wote waislamu na wasio waislamu kwa msingi wa kushirikiana na kukamilishana kwa ajili ya manufaa ya ulimwengu kote. Kwa kweli Uislamu ulikuja ili kuimarisha mahusiano baina ya watu siyo kwa kuyakata yale mahusiano na kupigana nayo.
Jambo la kusisitiza hilo ni alilolifanya Mtume (S.A.W.) katika Suluhu ya Al-Hudaybiya ambapo alifunga mkataba wa amani wa kwanza kabisa baina ya waislamu na washirikina kwa msingi wa kuheshimiana na kuamiliana kwa wema kwa lengo la kuisha pamoja kwa amani na utulivu na kuendeleza jamii na kuilinda nchi. Ingawa masharti ya mkataba huo yalionekana yanawadhulumu waislamu na kupendeleza washirikina lakini Mwenyezi Mungu Aliuita ushindi kama ilivyokuja katika kauli yake (S.W.): { Hakika tumekufungulia Ushindi wa dhaahiri * Ili Mwenyezi Mungu akusamehe makosa yako yaliyotangulia na yajayo, na akutimizie neema zake, naakuongoe katika Njia Iliyo Nyooka * Na Mwenyezi Mungu akunusuru nusura yenye nguvu} [48/1-3].
Hali hii inathibitisha kuwa Uislamu ndio dini ya amani na utulivu siyo dini ya ugaidi na vurugu, tena baada ya suluhu hilo ilitokea vita vya Khaybar baina ya waislamu na mayahudi na Mtume ameweka mkataba mwingine na mayahudi kwa ajili ya kuzilinda nafsi na damu za pande mbili, pia kuanzia mwaka wa saba baada ya hijra ya Mtume misafara ya mabalozi wa waislamu waliokuwa wanatumwa na Mtume huku na huku ili kueneza ujumbe wa amani na kuanzisha mahusiano na mataifa mbalimbali kwa lengo la kuthibitisha kuwa dini hiyo ni dini ya amani na upendo.
Mtume (S.A.W.) alikubali zawadi alizozipata kutoka wafalme wa umma nyingine kama vile; Al-Najashiy mfalme wa Uhabashi akawafanyia wajumbe wa mfalme yule ukarimu mkubwa akisema: "Hakika watu hawa waliwafanyia maswahaba zetu ukarimu mkubwa". Inatajwa pia kwamba Uislamu unawahimiza waumini wahifadhi mahusiano yao wenyewe kwa wenyewe na kuwafananisha kwa mwili mmoja kama ilivyokuja katika hadithi ya Mtume: "Kwa kweli mfano wa waumini katika upendo na huruma wao wenyewe kwa wenyewe ni kama mwili mmoja kama kiungo kimoja kinauma basi mwili mzima huumwa na kutaabika kwa maumivu ya kiungo hicho".