Hapana shaka kuwa Uislamu unatilia mkazo ushirikiano na umoja wa Waislamu katika nyanja zote za maisha, kimaadili, kitabia, hata katika Ibada; Hakuna ibada, au tabia ya Kiislamu, au jambo la kidunia isipokuwa unakuta ndani yake wito wa umoja.
Ibada ya Hijja ni mojawapo ya nguzo tano kuu za Uislamu. Nayo ni msimu bora wa kumtii Mwenyezi Mungu Mtukufu, na fursa nzuri kwa Waislamu kuonyesha umoja wao, nguvu yao, na mshikamano wao kwa kauli na matendo.
Hijja ni Arafa
Siku ya Arafa inazingatiwa kuwa ni picha halisi ya umoja wa Waislamu na nguvu zao. Mamilioni ya Waislamu wanasimama katika safu safu wakiwa wameungana katika nia, dua, na mavazi ili kuhuisha mansaki hii tukufu, wakimwitikia wito wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kutangaza utumwa na utiifu wao kwake pekee (S.W), kumkana kila mshirikina, na kukataa dhulma yoyote au kiburi cha kimataifa dhidi ya taifa la Kiislamu na Waislamu wote.
Mojawapo wa waandishi amesema: “Lau wenye mamlaka wa Waislamu wangetaka kuitumia Hijja katika kuleta umoja wa Kiislamu basi wangefaulu”. Kwani mamilioni ya watu wanakuja kutoka miji mbalimbali ya ulimwengu na kukusanyika katika uwanja mmoja na kuzielekeza nyoyo zao na masikio yao mahala hapo penye kukhofisha.
Waislamu wanapotekeleza mansaki za Hijja, wanasimama pamoja mkono kwa mkono na mbegu kwa mbegu; yaani wote ni sawa mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, bila kujali rangi, lugha, makabila, taifa, au hali ya kijamii, jambo linaloakisi usawa na udugu baina ya Waislamu, ambapo wakaribishana, wajuana, wabadilishana tamaduni zao. Basi pindi wataporudi kwenye nchi zao watayatangaza mambo waliyojifunza kwa ndugu zao, na watakuwa kwao ni kama wajumbe wa mkutano mkuu, jambo linalounganisha nchi za kiislamu zenyewe kwa zenyewe. Kwa hivyo basi, tunaweza kusema kuwa Hijja ni njia ya mafahamiano, mshikamano, na kuimarisha mahusiano na ushirikiano na maungamano baina ya mataifa ya Kiislamu.
Hijja haikujitenga na maisha ya watu ya kila siku, bali imeshikana nayo, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema ndani ya kitabu chake kitukufu: "Ili washuhudie manufaa yao na kutaja jina la Mwenyezi Mungu katika siku maalum.." {Al-Hajj :28}, yaani manufaa ya biashara duniani na malipo katika akhera.
Pamoja na hayo, Hijja ni fursa mwafaka kwa ajili ya kuwakhofisha maadui ya Uislamu na Waislamu na kuwatishia na kuzitokomeza njama zao, basi ni adui gani mkali aliye dhidi yetu kuliko mamlaka ya kizayuni ambayo imepora ardhi yetu na kuwafukuza wananchi wetu na ikawaua na inaendelea kuwaua watoto wa Kipalestina na kuhalalisha mauaji yao, heshima zao, na kuvunja utu wao?
Kwa hivyo tunapaswa kutoacha fursa ya Hijja na mkusanyiko wa pekee wa mamilioni ya Waislamu, upotee ovyo bila ya kuutumia kuwaamsha Waislamu kutoka usingizi wao na kuwafanya wajitolee kupinga shari ya maadui wetu, na kujadili matatizo ya Waislamu, na kujaribu kutoa fumbuzi wa pamoja.
Kwa upande wake, Kituo cha Al-Azhar cha Kupambana na Fikra Kali kinausia mambo yafuatayo katika kivuli cha kile tunachokishuhudia katika siku hizo, hasa kwa mnasaba wa msimu wa Hijja. Kati ya mambo hayo:
- Kuongeza ufahamu wa mahujaji kwa roho na kiini cha faradhi ya Hijja ili mahujaji waweze kutekeleza na kufanya maadili ya mansaki za Hijja katika maisha yao ya kijamii, iwe wakati wa utendaji wa Hijja na baada yake.
- Kuchukua msimu wa Hijja ni tukio la kusoma shida za uma wa Kiisilamu na kuzipatia fumbuzi ili mkutano usiwe sherehe tu, lakini badala yake unaathiri vyema maendeleo na umoja wa uma wa Kiisilamu
- kuhimiza serikali na taasisi za Hijja kutumia vizuri msimu wa Hajj kama njia ya kuunganisha uimarishaji na ustawi wa uma katika nyanja zote za maisha
- Kuchukua msimu wa Hijja kama njia ya kujua mafanikio ya nchi zote ili kuimarisha ushirikiano katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kitamaduni.