Kwa hakika Mwenyezi Mungu (S.W.) Amemteremshia Mtume wake (S.A.W.) sheria ya kudumu mpaka siku ya mwisho, ambapo hukumu za sheria hiyo zikawa mbinu inayotokana na Mungu na inayohusiana na nyanja mbali mbali za maisha ya wanadamu, kama kwamba mbinu hiyo hufaa kutekelezwa katika zama zote na pahala pote bila ya kujali mazingira au hali, kwani sheria ya kiislamu inasifika kwa inakubali kuboreshwa na kuendelezwa kwa mujibu wa kubadilika kwa hali ya mambo, kwa hiyo sheria hiyo haikuwa na hali thabiti bila ya kufanyiwa uboreshaji kwa kuwa kuboresha ni maumbile ya maisha, na kubadilikabadilika ndiyo kanuni ya dunia ambapo hapana kiumbe wala kitu hubaki na hali moja milele, na kinyume cha uboreshaji ni kuwa kuwa na hali moja na kutokwenda sambamaba na mabadiliko na maendeleo, jambo ambalo huwa sawa na kufa na kukosa uhai, lakini hiyo haiwezekani kwa sababu ya kwamba maisha na mabadiliko hayatengani kamwe.
Uislamu kwa mujibu wa maumbile yake ni dini inayoafikiana na sunna za maisha isiyopingana na maumbile ya Kibinadamu hata kidogo, kwa hiyo, Uislamu ndiyo dini inayohimiza sana kuleta maendeleo ya mara kwa mara kwa hali ya mambo na jamii kwa ajili ya kufika kiwango cha juu kabisa na kuwa na hali bora zaidi katika pande mbali mbali za maisha. Mtume (S.A.W.) ameelezea dhana ya uboreshaji katika sheria ya Kiislamu, aliposema katika hadithi takatifu: "Kwa hakika Mwenyezi Mungu Anawatumia ummah huu mwanzoni mwa kila karne, mmoja wao anaye elimu ya Kuendeleza na kufufua mafundisho ya dini yao". Na kwa kuwa Uislamu ni dini ambayo mafundisho yake yanafaa maisha yote, basi uboreshaji unaokusudiwa katika hadithi hii ya Mtume (S.A.W.) ni ule ule uboreshaji wa maisha katika nyanja zake tafauti. Na uboreshaji tunaolenga sio jambo la kiholela, wala haliwi bila ya misingi na vidhibiti maalumu, bali ni uboreshaji unaotegemea uelewa na kutambua hali halisi ya mambo kwa ajili ya kugundua na kubainisha mabaya yake, hivyo kurekebisha hali ilivyo na kuandaa mabadiliko mapya yenye kuleta uboreshaji na kuendeleza maisha kwa kutegemea masuluhisho yaliyobuniwa kwa lengo la kugeuza maisha ya wanadamu iwe bora katika nyanja zake mbalimbali, jambo ambalo huchangia sana kuboresha hali yao kidini na kidunia.
Kwa kuwa dini ni nguzo ya maisha kikamilifu, basi kazi ya Fiqhi inahusiana na kukidhi mahitaji yote ya maisha hayo, na kwenda bega kwa bega na mabadiliko ya maisha, na madamu masuala ya kifiqhi hayana hukumu thabiti; maana yanakubali kubadilika kutokana na mabadiliko ya hali, yale mabadiliko ambayo ni jambo la kawaida kwa mujibu wa jitihada inayotakika katika mambo yanayoruhusiwa kufanyiwa jitihada katika Uislamu kwa lengo la kuwarahisishia watu mambo ya dini yao na kuondoa mashaka, pamoja na yale masuala mapya ambayo maulamaa wa sheria (Fiqhi) ya kiislamu hawakuyajua wala hawakutoa ufafanuzi wake, hivyo jitihada ikawa jambo linalotakiwa ili kupata hukumu ya kisheria inayofaa, kama vile; suala la kunukuu viungo vya mwanadamu kutoka mtu kwa mwingine, upachizaji, mtoto wa maabara na masuala mengine mengi ya matendeano ya kifedha ya kisasa, na kadhalika, hasa baada ya uzinduzi wa teknolojia ya kisasa ya maelezo ya kilektroniki na mawasiliano, na kuenea utumiaji wa intaneti kwa upana zaidi na zaidi, na kuhitilafiana kuhusu usahihi wa kutumia mbinu hizo kupitisha ndoa au talaka au wasia na matendeano mengineyo.
Kwa kweli zama ya kisasa ina mabadiliko makubwa yenye umuhimu kwa maisha ya binadamu, kwa hiyo sheria ya kiislamu (Fiqhi) inabidi kuwenda sambamba na mabadiliko na maendeleo haya kwa kutoa hukumu za kisheria zinazomsaidia mwislamu aafikiane na zama anapoishi, wala hawi mbali na mabadiliko haya. Kwa hivyo, wito wa kuangalia upya baadhi ya masuala na hukumu za kifiqhi siyo kazi mbaya wala hakumaanishi kutoka nje ya misingi na mafundisho ya dini au kukana hukumu zake, bali hali hiyo inamaanisha kuangalia upya hukumu na maelezo ya kifiqhi yaliyotufikia kizazi baada ya kizazi kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine inamaanisha kutafuta masuluhisho ya kiislamu kwa masula mapya yanayojitokeza katika jamii. Kwani kuna masuala mengi yanayohusiana na maisha ya waislamu ambayo yanahitaji kuangaliwa kwa mtazamo wa kisasa na kupangwa upya, jambo linalobidi kuzingatiwa sana na hasa kwa kuzindua na kuongeza tanzu mpya za Fiqhi kama vile, Fiqhi ya kisasa (hali halisi ya kisasa), Fiqhi ya masuala yaliyo muhimu zaidi na Fiqhi ya waislamu walio wachache. Hayo yote yanatubidi kufanya jitihada zaidi na zaidi zinazoambatana na zama na pahalaa, tukiwa na uelewa, wepesi na ufahamu kwa hali halisi ya mambo.
Ama kuhusu kuboresha fikra, basi ni kubuni dhana na maelezo mapya kuhusu mambo na vitu maalumu. Kwa upande huu, fikra ya kiislamu inagawanyika katika makundi mawili: Fikra zinazokubali kuboreshwa na kuendelezwa au hata kubuniwa. Ilhali zipo fikra zuisizokubali kufanyiwa uboreshaji na kuendelezwa kabisa, kwa kuwa zinapingana na misingi thabiti na nguzo imara za dini ambazo haiwezakani kubadikishwa kama vile, misingi ya itikadi na imani, ambapo vipo baadhi ya vigezo na masharti ya uboreshaji kuhusu fikra ya kiislamu, vigezo na vidhibiti hivyo ni pamoja na: - Kutobadilisha misingi ya sheria wala nguzo zake, bali huwa kuhusu Fiqhi ya sheria na namna ya kuifahamu kutokana na mabadiliko mapya ya wakati, vifaa na mbinu zake tafauti. - Kutobadilisha au kufanya jitihada kuhusu matini zilizo wazi katika maana na hukumu kama vile, aya za Qurani Takatifu na hadithi za Mtume (S.A.W.). Kuwepo kwa jitihada kuhusu masuala yanayobeba mitazamo mbali mbali ambayo maulamaa, wasomi na wanavyuoni wa Fiqhi wamehitilafiana hukumu yake, kwa kuwa masuala hayo yanakubali kujadiliwa kwa mujibu wa mitazamo na maoni tafauti, sharti kutopingana na hukumu kuu za sheria ya kiislamu.
Hapana shaka kuwa miongoni mwa sifa hasa za sheria ya kiislamu wepesi na urahisi wake na kuwa ni sheria ya ukati na kati, jambo lililoifanya sheria hiyo iafikiane na maslahi za watu katika zama zote na pahala pote, na itadumu chanzo cha uboreshaji na maendeleo yoyote yanayokuwa sababu ya kuwanufaisha waislamu na kuunga mkono ustawi na maendeleo ya kistaarabu wangekuwepo wenye jitihada na uboreshaji wanaotambua vyema umuhimu wa jitihada wakielewa vizuri hadithi ya Mtume (S.A.W.) kuhusu kuboresha na kuendeleza dini ipasavyo.