Hapana shaka kuwa tabia njema na mwenendo mzuri ni sifa moja wapo sifa za msingi na sababu muhimu miongoni mwa sababu za kuziendeleza jamii na kuzifanikisha, ambapo ustaarabu, ustawi na maendeleo zinafungamana na tabia na mwenendo za watu husika. Mwenyezi Mungu (S.W.) Alipomtuma Mtume wake Muhammad (S.A.W.) Akamkalifisha afikishe ujumbe wake unaojengeka tabia njema, mpaka zikawa msingi mmoja wa misingi na nguzo za ujumbe wa Uislamu. Ingawa tabia njema zilikuwepo na zilikuwa na dosari maalumu na zilikuwa na vipungufu kadhaa. Kwa hiyo, Uislamu ulikuja kwa lengo la kukamilisha tabia hizo na kuziba vipungufu hivyo, ukaziweka imara na kuzikuza na kuziendeleza kwa mujibu wa mafundisho ya sheria ya kiislamu.
Kwa kuangalia Tabia na Mwenendo kwa maana yao ya kijumla tunaelewa kuwa ni hali ya kibinadamu ambayo watu wengi wanaitafuta wakiwa na hamu kubwa ya kuifikia kwa kuwa tabia njema inamtukuza mwanadamu duniani na akhera. Kwa kawaida yao, watu wanampenda mwenye tabia njema na kujikurubisha naye na kutamani kuambatana naye na kuwa na urafiki naye, siyo hii tu, bali pia, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanampenda na kumtukuza mwenye tabia njema kama alivyosema Mtume (S.A.W.): "Kwa hakika ninaowapenda zaidi na watako kuwa karibu zaidi kwangu siku ya mwisho ni wale wanao tabia njema na maadili mema, ilhali watakao kuwa mbali kwangu na ambao ninawachukia zaidi ni wale wanaodai kuwa wanaelewa na wanaozungumza tu na wale wanaotoa hukumu za sheria bila ya kuwa na kiwango chochote cha elimu ya Fiqhi na Sheria".
Kwa hiyo, Uislamu umehimiza sana kuwajibikia mienendo mizuri na tabia njema na kuwatakia wafuasi wake kuhifadhi tabia njema mpaka sheria ya kiislamu imekanusha ukamilifu wa itikadi na uzuri wa imani kwa yule mwislamu anao upungufu au kasoro fulani kuhusu tabia na maadili, kwani tabia katika Uislamu ni ile misingi na nguzo zilizoainishwa na sheria kupitia matini takatifu ya Qurani na Sunna za Mtume (S.A.W.) ambapo zile nguzo na misingi huwaelekeza watu kwenye njia sahihi ya kudhibiti maisha yao na kufikia lengo la kuumbwa kwao. Jambo linalochangia kudhibiti mienendo yao na kuweka maisha yao katika njia inayotakikana kwa kulazimika kwa vidhibiti vya sheria.
Hakika Qur’ani Tukufu ndiyo msingi wa suala lolote linalofungamana na Dini ya Kiislamu, nayo ni mfumo unaofaa kila wakati na mahali, na bila shaka kuwa Qur’ani kupitia dhana hiyo thabiti iliyo sahihi inajumuisha kila linalohitajika na taifa la Kiislamu katika mahusiano yanayowaunganisha waisalmu wenyewe kwa wenyewe, bali pia uhusiano wa taifa la Kiislamu kwa mataifa mengine katika hali mbalimbali. Vile vile Qur'an Tukufu inaanzisha nyumba ya kiislamu ambayo ndiyo jamii ndogo ya mume na mke, na kuweka vidhibiti vya uhusiano huo katika awamu zake zote na inazijaalia zitegemee huruma, upendo na rehma, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao fikiri" [Ar-Rum: 21]. Pia, uhusiano huo unabidi kuzingatia kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Wala msisahau fadhila baina yenu. Hakika Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda" [Al-Baqarah: 237].
Hii ina maana ya kwamba Qur'an Tukufu haishughulikii suala maalumu, bila ya kujali masuala mengine, bali inazungumzia masuala yote katika wakati wake maalumu, kwa hiyo, tunakuta aya zinazozungumzia nyumba ya kiislamu zinaambatana na zile aya zinazoshughulikia masuala ya kijamii, kisha baadaye zile zinazozungumzia mahusiano kati ya mataifa, aya hizo zote na mahusiano haya yanafungamana na hali halisi ambayo mwislamu anaishi kila siku na kutendeana na watu mbalimbali.
Na tukiangalia uhusiano uliopo baina ya umma wa Kiislamu na mataifa mengine, tunakuta kwamba Qur'ani imeuainisha kama yafuatayo: Umma wa Kiislamu ni wenye kuongoza na kulingania kwa Mwenyezi Mungu, hamu yake ya kwanza ni kuvutia mioyo kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na aliyekuwa na kazi kama hiyo, basi hawi kamwe mlinganiaji kwa mgongano na wengine, bali hufanya kazi ili kuvutia mioyo kwa njia sawa kwa kutumia hikima na mawaidha mema, na dalili za hayo ni zingi, kutoka Qur'an Tukufu; kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Nyinyi mmekuwa bora ya umma waliotolewa watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyezi Mungu. Na lau kuwa Watu wa Kitabu nao wameamini ingeli kuwa bora kwao. Wapo miongoni mwao waumini, lakini wengi wao wapotovu" [Aal Imran: 110]
Hivyo, umma wa Kiislamu halikujitolea binafsi, bali lilijitolea kwa ajili ya kuwalingania watu kwa namna iliyo bora kwa Mwenyezi Mungu, na kauli ya Mwenyezi Mungu: "Sema: Hii ndiyo Njia yangu - ninalingania kwa Mwenyezi Mungu kwa kujua - mimi na wanao nifuata. Na ametakasika Mwenyezi Mungu! Wala mimi si katika washirikina" [Yusuf: 108]. Kwa hivyo, umma huo unawajibika kulingania kwa Mwenyezi Mungu kwa mujibu wa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na mlinganiaji kwa Mwenyezi Mungu hawi na hatakuwa kamwe miongoni mwa walinganiaji wa kupiga vita.
Zaidi ya hayo, Mtume (S.A.W.) ameashiria hali hii kwa kauli yake: "Hakika mlitumwa wenye kusahilisha sio wenye kushadidisha". Na hiyo kwa matini ni kutupa sisi waislamu jukumu la kuwalingania wengine na kuwaita kwenye njia ya Mwenyezi Mungu (S.W.) kama lilivyokuwa jukumu la Manabii na Mitume, kwa kuwa Uislamu utabaki na kuendelea kwa hikima na matakwa ya Mwenyezi Mungu, basi shughuli za kuilingania dini hiyo zitaendelea.
Na miongoni mwa sunna ya kivitendo ya Mtume (S.A.W) kwamba Mtume alikuwa na huruma pamoja na Mayahudi, Wakristo na makabila ya Kiarabu waliokuwa wanajadiliana na kubishana naye kwa lengo la kuwavutia kwa njia iliyongoka ya Mwenyezi Mungu, na hiyo tunaikuta katika kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lilio sawa baina yetu na nyinyi: Ya kwamba tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote; wala tusifanyane sisi kwa sisi kuwa Waola Walezi badala ya Mwenyezi Mungu. Na wakigeuka basi semeni: Shuhudi- eni ya kwamba sisi ni Waislamu" [Aal Imran: 64].
kwa njia hii inayojaa huruma, ulaini na rehma ambayo inaonyesha kuwa msingi wa mahusiano baina ya Waislamu na wengineo ni amani sio vita, na ulaini sio vurugu na malumbano sio mgongano, na maana hii inathibitishwa na aya nyingi katika Qur'an Tukufu. Na miongoni mwa aya hizo ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na wakielekea amani nawe pia elekea, na mtegemee Mwenyezi Mungu" [Al-Anfaal: 61]. Aidha, Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: "Anaye kushambulieni nanyi mshambulieni, kwa kadiri alivyo kushambulieni" [Al-Baqarah: 194]. Ama anayedai kuwa uhusiano baina yetu sisi waislamu na makafiri ni uhusiano wa kupigana na kugongana, basi huyu ni miongoni mwa wanaobadilisha dini na wapitao mipaka ambao ni lazima waelewe dini yao au wajiepukane na kutoa fatwa ili wasikosea Uislamu kama inavyotokea siku hizi.
Ama yule anayehojiana kwa kauli ya Mwenyezi Mungu: "Na piganeni na washirikina wote" [Al-Tawabah: 36], basi amesahau kwa makusudi lengo na sababu za aya iliyopita, nazo ni kauli yake Mtukufu katika aya hiyo hiyo: "kama wao wnavyo pigana nanyi nyote", basi sababu ya kutukia mapigano ni mapigano, kwa maneno mengine; sababu ya kupigana ni kujitetea siyo kuwashmbulia wengine au kuanza uadui, na ikiondoka sababu na lengo, basi tukio litaondoka vile vile, pia kuna dalili ya hayo kutoka Sunna ya Mtume (S.A.W.) na sera zake, ambapo Mtume (S.A.W.) aliwaacha Wakristo wa Hajr, aidha aliwaacha Majus wa Oman na Hajar wakiendelea na mila yao ya Umajusi.
Vile vile, aya iliyomo katika sura ya An-Nisaa imewajaalia watu wote ni wa tumbo moja na nafsi moja ambayo ndio msingi wa mahusiano yaliyopo baina ya watu kwa misingi wa ushirikiano katika wema na uchamungu na kubadilishana manufaa ambayo inasimamisha maisha ya watu, kama Alivyosema Mwenyezi Mungu (S.W.): "Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi. Na tahadharini na Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaombana, na jamaa zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaangalieni" [An-Nisaa: 1].
Kwa hivyo, tunaweza kusema kwamba Qur'ani Tukufu ni msingi wa kila mahusiano yote baina ya watu sawa katika nyumba moja ambayo ni mwanzo wa jamii kubwa na nguzo yake ya kwanza, au kwa umma wa Kiislamu na uhusiano wa waislamu na mataifa wengineo, na hapana shaka kuwa kufuata mafundisho ya Qur'an kuhusu yale mahusiano ya kibinadamu kunalazimika kutendeana na viumbe wote kwa mujibu wa maadili ya huruma, usameheve, na upole.