Uislamu imepanga mahusiano ya kibinadamu baina ya watu wote na Qurani imebainisha kuwa msingi wa mahusiano haya ni kushirikiana na kusaidiana kwa wema na hisani kwa upande mmoja na kwa upande mwingine kubadilishana manufaa kwa mujibu wa kauli yake Mwenyezi Mungu: {Na saidianeni katika wema na uchamngu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Munguni Mkali wa kuadhibu} [5/2] kwa kuangalia kimalizio cha aya hii tunaona kuwa Mwenyezi Mungu Ametoa onyo kali kwa wale wasiolazimika kwa maamrisho yaliyotajwa katika aya yenyewe. Jambo linalothibitisha umuhimu wa kuwajibika kwa mwislamu kwa dini yake, umma wake, jamii yake na nchi yake. Mwislamu ni mwakilishi wa mafunzo ya dini yake na balozi wa umma wake, kupitia vitendo vyake na mwenendo wake maadili mema ya dini hutambulikana na kiini cha Uislamu hujulikana.
Miongoni mwa maadili na misingi imara ya dini hiyo kuhifadhi mahusiano ya kibinadamu na kuchunga vizuri uhusiano uliopo baina ya mwislamu na watu wote bila ya kujali dini wala rangi wala kabila wala chochote kingine, kwani watu wote wametokana na asli moja kama ilivyoelezwa mwanzoni mwa sura ya An-Nisaa: {Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi. Na tahadharini na Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaombana, na jamaa zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaangalieni} [4/1].
Na katika sura hiyo hiyo tunaona kuwa Qurani Takatifu inatwelezea umuhimu wa kuungana kwa watu na kuukuza huhsiano wao wenyewe kwa wenyewe kwa ajili ya maslahi ya jamii na ulimwengu kote. Na katika agizo la jumla Mwenyezi Mungu Amewaagiza wanadamu wote kumwabudu peke yake tena kuamiliana kwa wema na hisani: {Muabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe na chochote. Na wafanyieni wema wazazi wawili na jamaa na mayatima na masikini na jirani wa karibu na jirani wa mbali, na rafiki wa ubavuni na mpita njia, na waliomilikiwa na mikono yenu ya kulia. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wenye kiburi wanao jifakhiri} [4/36]
Kwa kuangalia aya hii tunaona kuwa imewakusanya watu wa aina mbalimbali maana imetoa wasia kwa watu watunzane wote kwa wote, tunaowajua na ambao hatuwajui, jamaa na ukoo, jirani, na hata wageni wapitao njia tumeamrishwa kuwafanyia wema na hisani. Pia, Mtume (S.A.W.) alikuwa anawausia maswahaba zake na waumini wote kufanya hisani na kulazimika kwa wema na watu wote hata wasio waislamu kwani undugu wa kibinadamu ni asli ya miamala yoyote baina ya mtu na mwingine. Kwa hiyo, mwislamu anatakiwa kuwa mwema na mpole na watu wote angalau hakufanyiwa uadui wala hakuudhiwa, na hata ikitukia kwamba mwislamu ameudhiwa na kuvamiliwa basi anatakiwa kujibu uadui huu pasipo na dhuluma wala ukatili.
Vile vile tunaelewa kuwa mwislamu hatakiwi kuwa mwema na hamaa na ukoo wake tu, bali na watu wote na hasa mayatima, maskini, wanyonge na wanao shida yoyote maishani mwao, kwa kuwa kusaidiana ni mojawapo maadili ya msingi katika Uislamu ambapo mwislamu anatakiwa kuwa mpole na mwenye huruma na rehma kwa wote na kuwalea watoto wake kwa mujibu wa tabia hizo njema.
Pia, Qurani Tukufu inatubainishia kuwa watu wote ingawa ni mataifa na makabila mbalimbali lakini wana mambo ya pamoja ambayo hutakiwa kuzingatiwa na kutoa mbali zile khitilafu kwa ajili ya kueneza fikra ya kuishi pamoja kwa amani na kuamiliana vema baina ya watu wote. Mwenyezi Mungu Amesema: {Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari} [49/13] Kwa hivyo tunaelewa kuwa Mwenyezi Mungu Ameainisha kipimo cha kupendeleana baina ya watu kuwa ni ucha Mungu, maana utajiri, uraia, kabila, rangi, taifa n.k. havitambuliki kama ni vipimo vya kupendeleza huyu au yule.
Vile vile, aya inatwelezea kuwa hikima ya kuumba watu katika mataifa na makabila mbalimbali ni kujuana na kukamilishana na kushirikiana katika mambo ya kuimarisha na kutengeneza maisha na kudumisha uhai. Hali hiyo hiyo, alivyokuwa Mtume (S.A.W.) ambapo alianzisha dola ya kiislamu kwenye jamii mpya ya baada ya Hijra kwa msingi wa undugu baina ya waislamu wenyewe kwa wenyewe na kuhishimiana na kusaidiana baina ya waislamu na wasio waislamu ambao wanaishi pamoja nao katika Al-Madinah, kwa hiyo alifunga mikataba na kutuma misafara na mabalozi kwa kila pembe kwa kutangaza kwamba dini hii ni dini ya kuishi pamoja na watu wote siyo dini ya ubaguzi wala chuki.
Tangazo hilo la amani na upendo lilikuwa ni sehemu ya ujumbe wa Uislamu ambao unategemea upendo na kusaidiana na kuamiliana kwa wema na watu wote kwa ajili ya kutimiza muradi wa Mwenyezi Mungu kuumba watu na kuwafanya mataifa na makabila mbalimbali.