Katika siku ya kumi na sita mwezi wa Novemba kila mwaka ulimwengu husherehekea kumbukumbu ya Siku ya Kimataifa ya Usamehevu kwa lengo la kuadhimisha na kuimarisha maadili ya usamehevu, msamaha, upendo na ushirikiano, ambayo ni maadili yaliyohimizwa na Uislamu tangu zaidi ya miaka 1400.
Wanavyuoni wamebainisha kuwa Uislamu imeainisha misingi inayotakiwa kuzingatiwa katika matendeano na wengine ambao ni wasio waislamu, na kwamba misingi hiyo inategemea zaidi usamehevu ambao unafungamana na msamaha unaomaanisha kuwafanyia watu wema na kutojali makosa yao bali kufanya heri hata wakiwa tofauti kiitikadi kimila na kadhalika.
Aidha, wataalamu wamesisitiza kuwa tabia ya usamehevu ni mojawapo maadili yenye hali ya juu katika dini hiyo adhimu, na kwamba usamehevu katika Uislamu uko dhahiri katika sura mbalimbali; kama vile: usamehevu wa kidini unaomaanisha kuwa wafuasi wa dini tofauti kuishi pamoja wakiwa na uhuru na amani kuchagua dini na kutekeleza ibada zao bila ya kusumbuliwa wala kulazimishwa kufuata dini maalum. Kwa hiyo, katika Uislamu watu wote wako sawa katika haki za kuishi maisha mazuri yenye raha, amani na uhuru bila ya kumbagua yeyote kutokana na dini yake au kabila au rangi, ambapo mwanadamu amepewa utukufu na heshima kubwa mno katika dini ya Uislamu kwa mujibu wa chanzo cha sheria ya kiislamu; Qurani Takatifu.
Hivyo, haikubaliki kuzingatia hitilafu za watu katika imani, uraia, jinsia, lugha, rangi, kabila ... sababu ya kuchocheza vurugu na chuki baina ya wanadamu, bali kweli ni kuwa Mwenyezi Mungu (S.W.) Ametaka waja wake wawe mataifa na makabila mbalimbali kwa hikima ya kujuana, kukamilishana na kukidhi maslahi za maisha pamoja.
Kwa kuangalia mtazamo wa Uislamu kuhusu wasio waislamu na hasa "Watu wa Kitabu" tunaelewa kuwa dini hiyo imetaka waislamu na wasio waislamu wakamilishane, wasiadiane na washirikiane kuimarisha nchi na kuendeleza jamii. Mtazamo huo unaotokana na kauli yake Mwenyezi Mungu (S.W.): {Mwenyezi Mungu hakukatazini kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawakukupigeni vita, wala hawakukutoeni makwenu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao uadilifu} [Al-Mumtahinah: 8]. Kwa mujibu wa aya hii na nyinginezo sheria ya kiislamu imebainisha misingi ya miamala baina ya waislamu na wasio waislamu.
Na kwa ajili ya kubainisha kuwa dini hii haikuja ili kuwalazimisha watu wafanye wasiyoyataka hata wakiwa wanakataa kujiunga nayo, Mwenyezi Mungu (S.W.) Alisema: {Hapana kulazimisha katika Dini. Kwani Uwongofu umekwisha pambanuka na upotofu} [Al-Baqarah: 256].
Kwa kweli, usamehevu katika Uislamu unajitokeza kupitia aina mbalimbali za usamehevu; usamehevu wa kidini hujitokeza katika hali ya kuhurumiana na kuishi pamoja kwa uhuru na amani baina ya wafuasi wa dini na madhehebu tofauti bila ya kuwa na vurugu wala ubaguzi wowote. Pia, usamehevu wa kifikra unaomaanisha kuwapa watu wote uhuru wa kujielezea na kujadiliana bila ya kumzuia mtu haki hii hata akiwa mpinzani sharti washiriki wote wazingatie vidhibiti vya kuhojiana na waheshimu wengine kwa wengine. Miongoni mwa misingi ya usamehevu wa kfikra katika Uislamu kuwapa wataalamu, watafiti wanao sifa maalum za kuwawezesha kufanya jitihada katika hukumu za kisheria watoe maoni yao bila ya kubanwa, kwa hiyo Qurani Tukufu imewahimiza waumini wajadiliane na wengine kw wema na kuheshimu maoni mbalimbali, kwa lengo la kujenga husiano za kibinadamu zilizo imara kwa msingi wa usamehevu na amani.
Mwenyezi Mungu (S.W.) Alibainisha misingi ya kujadiliana na watu Aliposema: {Wala msijadiliane na Watu wa Kitabu ila kwa njiailiyo nzuri kabisa} [Al-Ankabut: 46]. Naye Mtume (S.A.W.) alizingatia sana kudhihirisha kuwa Uislamu ni dini ya rehma, usamehevu na msamaha na watu wote waislamu na wasio waislamu, akitahadharisha kikali kuwafanyia dhuluma, kwa kusema: "Yeyote kumdhulumu mwenye ahadi au kumpunguzia haki yake au kumkalifisha zaidi ya uwezo wake au kumchukulia kitu pasipo na ridhaa yake basi nitabishana naye Siku ya Mwisho".
Eneo la dola la kiislamu lilipoongezeka katika enzi ya Mtume (S.A.W.) palikuwa makabila mengi ya kiarabu ambao wakresto na hasa huko Najraan, hakufanya ila kuafikiana nao kwa mujibu wa mikataba na azimio zinazohifadhi haki zao kuendelea na imani yao na kufanya ibada zao wakiwa huru na kuhifadhi pahala pa ibada zao, pamoja na kuwapa uhuru wa kifikra, elimu na kazi. Aidha, Mtume (S.A.W.) alikuwa anatumia mtindo mzuri na maneno matamu na watu wote na hasa wasio waislamu, akiwapa maswahaba wake watukufu (R.A.) mfano wa kuigwa wa usamehevu na ukarimu wakati aliposhinda makafiri wa Makkah na kuingia Mji Mtukufu baada ya kulazimishwa kuuhamia, ambapo ingawa alikuwa na fursa ya kuwaangamiza wale makafiri kwa uadui na dhuluma waliyoyafanya naye lakni hakufanya ila msamaha akawaachilia huru.
Hivyo, inafahamika kwamba Uislamu ni dini inayojengeka juu ya kusameheana baina ya waislamu wenyewe kwa wenyewe na baina ya waislamu na wasio waislamu, kwa mujibu wa matini nyingi katika Qurani Tukufu kama vile; kauli yake Mwenyezi Mungu: {Na wanayoyaepuka madhambi makubwa na mambo machafu, na wanapokasirika wao husamehe} [Al-Shuura: 37].
Kwa kuwa msamaha ni mojawapo dalili za utukufu, ubora na imani thabiti, Mtume (S.A.W.) alikuwa anawafundisha maswahaba wake namna ya kuwa na sifa hii. Imesimuliwa kuwa mtu mmoja alikuja kwa Mtume (S.A.W.) akamuuliza: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Nimsamehe mtumishi wangu kiasi gani? Mtume akajibu: kila siku mara sabini". Pia, miongoni mwa sababu kuu za kuenea kwa Uislamu kwa haraka katika kila pembe duniani ni misingi yake ya tabia njema zikiwemu sifa hizi za usamehevu, upole, rehma na sheria yake yenye hikima na uadilifu.
La kuzingatiwa ni kwamba wenyeji wa nchi mbalimbali walipoona tabia njema za waislamu na maadili mema wanayoyafuata wakajiunga na dini hiyo adhimu kwa urahisi na haraka, kwa njia hii Uislamu ilienea sana ulimwenguni. Ukisoma azimio alizozifunga Swahaba Abu Obidah bin Al-Jarrah na watu wa Al-Shaam zilizowapa wasio waislamu haki ya kuendelea na dini zao na kuhifadhi mahekalu na makanisa yao ndani ya miji na nje yake yasiharibishwa wala kumuudhi hata mmoja wao na pia kuahidiana nao kuwatetea kutokana na uadui wowote kwa muibu wa ushuru wa kiasi kidogo mno, kwa hiyo waliitwa Ahlu-Dhimma maana wanaolipa kwa ajili ya kutetewa.
Watu hawa wa Ahlu-Dhimma wamekubali masharti na vidhibiti vya azimio hizo, wakaishi katika amani, uhuru na miamala mizuri, kwa hiyo wakavutwa kwa dini ya Uislamu wakaona bora kujiunga nayo. Basi wale ambao wakawa waislamu halisi hawakuwa na wajibu ya kulipa Jizyah.
Kwa jumla, usamehevu ni mojawapo maadili mema ya kiislamu ambao unahitajika wakati wote kwa ajili ya kupata utulivu, amani na maendeleo kwa jamii yote. Vile vile, historia ya kiislamu imejaa misimamo ya kubainisha umuhimu wa sifa hii na namna ya kuitekeleaza katika hali halisi ya umma. Kwa hakika usamehevu hudhihirika zaidi na ambao ni tofauti kidini, kiitikadi, kikabila, kimadhehebu n. k.
Tunahimisha makala yetu hii kwa kueleza kuwa usamehevu humaanisha kuwa na heshima na rehma pamoja na watu wote na kuwajibika kushirikiana na wote bila ya kujali tofauti zilizopo baina yako na wengineo. Kuwadharau wengine au kuwatusi au kuwalazimisha kuwa na hali au sifa au fikra maalum kwa sababu yoyote hakuafikiani kabisa na mafundisho ya Uislamu.
Pia, maumbile ya kibinadamu yanatubidi kuishi pamoja na wanadamu wote na kushirikiana nao tukiwaheshimu na kuwafanyia wema na uadilifu japokuwa tofauti hizo, Mwenyezi Mungu (S.W.) Amesema: {Enyi mlio amini! Kuweni wasimamizi madhubuti kwa ajili ya Mwenyezi Mungu mkitoa ushahidi kwa haki. Wala kuchukiana na watu kusikupelekeeni kutofanya uadilifu. Fanyeni uadilifu. Hivyo ndio kuwa karibu mno na uchamngu} [Al-Maidah: 8] Kwa hiyo inabainika kwamba Mwenyezi Mungu Ndiye Anavijua vitendo vyote vya waja wake vikubwa na vidogo vidogo, kwa hiyo mwislamu anapaswa awe mcha Mungu katika hali zake zote, wala asimdhulumu yeyote kwa sababu yoyote. Na kwamba hitilafu siyo sababu ya kutosha ya kuruhusu kuwafanyia wengine uadui au mabaya.