Pande za Kibinadamu katika Sheria ya Kiislamu

Imeandaliwa na Dkt.; Alaa Salah Abdulwahed

  • | Thursday, 2 January, 2025
Pande za Kibinadamu katika Sheria ya Kiislamu

    Bila shaka dini ya Uislamu ndiyo dini ya kumtukuza mwanadamu na kumpa heshima kubwa bila ya kujali taifa lake, kabila lake, jinsia yake wala cheo au nafasi yake, bali inawazingatia watu wote ni viumbe wa Mwenyezi Mungu waliopewa heshima na Mola wao Mlezi Aliyesema: {Na hakika tumewatukuza wanaadamu, na tumewapa vya kupanda nchi kavu na baharini, na tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tulio waumba} Israa: 70.

Kwa hiyo, utukufu na heshima ni kwa wanadamu wote kama ilivyobainika katika Sunna za Mtume (S.A.W.) aliyekuwa anaeleza heshima kwa wanadamu wote kwa kuzingatia fadhila yao na nafasi waliyo nayo. Imesimuliwa kuwa “Mtume (S.A.W.) alipitia siku na jeneza ya myahudi mmoja akasimama kwa kuonyesha heshima kwa jeneza, maswahaba wakamwuliza: Ewe Mtume wetu mbona umesimama kwa jeneza hii ingawa ni ya myahudi?! Akamjibu: Je, siyo nafsi?!!” kwa namna hii Mtume (S.A.W.) ameeleza na kusisitiza kwamba sheria ya kiislamu ilipoharamisha kumdharau yeyote ilikusudia watu wote na iliwaamrisha waislamu wasaidane na wengine wawe na mahusiano mazuri na wengine ilikuwa inakusudia wanadamu wote; maana rehma ya dini hii iliyotokana na rehma yake Mtume (S.A.W.) ni kwa wanadamu wote si kwa kundi maalumu.

Mwenyezi Mungu (S.W.) Aliwaita waja wake katika Qurani Takatifu kwa tamko la “Watu” ambalo linajumuisha wanadamu wote, tamko hilo limetajwa mara 63 katika Qurani Takatifu, jambo linalobainisha kuwa sheria ya kiislamu ambayo msingi wake wa kwanza ni Qurani inawahotubia wanadamu kwa jumla wala haijawahusisha kundi maalum kwa mafundisho na maadili iliyokuja nayo. Mwenyezi Mungu Amewaita wanadamu wote katika aya nyingi kama vile: {Ewe mwanaadamu! Nini kilicho kughuri ukamwacha Mola wako Mlezi Mtukufu? * Aliye kuumba, akakuweka sawa, akakunyoosha * Katika sura yoyote aliyo ipenda akakujenga} Infitaar: 6-8. Zaidi ya hayo Mwenyezi Mungu Alibainisha kuwa asli ya wanadamu wote ni moja na kwamba hakuna sababu ya kumpendeleza mmoja zaidi kuliko mwingine isipokuwa uchamungu: {Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari} Al-Hujuraat: 13.

Pia, miongoni mwa mambo ya msingi katika sheria ya kiislamu ni kusisitiza kwamba ujumbe wa Mtume Mohammed (S.A.W.) unasifika kuwa ni ujumbe wa wanadamu wote sio ujumbe wa kundi au taifa maalumu, kwa hiyo Mwenyezi Mungu (S.W.) Amemsifu Mtume wake Akisema: {Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwawalimwengu wote} Al-Anbiyaa: 107.

Uislamu imepanga mahusiano ya kibinadamu baina ya watu wote na Qurani imebainisha kuwa msingi wa mahusiano haya ni kushirikiana na kusaidiana kwa wema na hisani kwa upande mmoja na kwa upande mwingine kubadilishana manufaa kwa mujibu wa kauli yake Mwenyezi Mungu: {Na saidianeni katika wema na uchamngu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi  Munguni Mkali wa kuadhibu} [5/2] kwa kuangalia kimalizio cha aya hii tunaona kuwa Mwenyezi Mungu Ametoa onyo kali kwa wale wasiolazimika kwa maamrisho yaliyotajwa katika aya yenyewe. Jambo linalothibitisha umuhimu wa kuwajibika kwa mwislamu kwa dini yake, umma wake, jamii yake na nchi yake. Mwislamu ni mwakilishi wa mafunzo ya dini yake na balozi wa umma wake, kupitia vitendo vyake na mwenendo wake maadili mema ya dini hutambulikana na kiini cha Uislamu hujulikana.

Miongoni mwa maadili na misingi imara ya dini hiyo kuhifadhi mahusiano ya kibinadamu na kuchunga vizuri uhusiano uliopo baina ya mwislamu na watu wote bila ya kujali dini wala rangi wala kabila wala chochote kingine, kwani watu wote wametokana na asli moja kama ilivyoelezwa mwanzoni mwa sura ya An-Nisaa: {Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi. Na tahadharini na Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaombana, na jamaa zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaangalieni} [4/1].

Na katika sura hiyo hiyo tunaona kuwa Qurani Takatifu inatwelezea umuhimu wa kuungana kwa watu na kuukuza huhsiano wao wenyewe kwa wenyewe kwa ajili ya maslahi ya jamii na ulimwengu kote. Na katika agizo la jumla Mwenyezi Mungu Amewaagiza wanadamu wote kumwabudu peke yake tena kuamiliana kwa wema na hisani: {Muabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe na chochote. Na wafanyieni wema wazazi wawili na jamaa na mayatima na masikini na jirani wa karibu na jirani wa mbali, na rafiki wa ubavuni na mpita njia, na waliomilikiwa na mikono yenu ya kulia. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wenye kiburi wanao jifakhiri} [4/36]

Kwa kuangalia aya hii tunaona kuwa imewakusanya watu wa aina mbalimbali maana imetoa wasia kwa watu watunzane wote kwa wote, tunaowajua na ambao hatuwajui, jamaa na ukoo, jirani, na hata wageni wapitao njia tumeamrishwa kuwafanyia wema na hisani. Pia, Mtume (S.A.W.) alikuwa anawausia maswahaba zake na waumini wote kufanya hisani na kulazimika kwa wema na watu wote hata wasio waislamu kwani undugu wa kibinadamu ni asli ya miamala yoyote baina ya mtu na mwingine. Kwa hiyo, mwislamu anatakiwa kuwa mwema na mpole na watu wote angalau hakufanyiwa uadui wala hakuudhiwa, na hata ikitukia kwamba mwislamu ameudhiwa na kuvamiliwa basi anatakiwa kujibu uadui huu pasipo na dhuluma wala ukatili.

Vile vile tunaelewa kuwa mwislamu hatakiwi kuwa mwema na hamaa na ukoo wake tu, bali na watu wote na hasa mayatima, maskini, wanyonge na wanao shida yoyote maishani mwao, kwa kuwa kusaidiana ni mojawapo maadili ya msingi katika Uislamu ambapo mwislamu anatakiwa kuwa mpole na mwenye huruma na rehma kwa wote na kuwalea watoto wake kwa mujibu wa tabia hizo njema.

 

Print
Categories: Makala
Tags:
Rate this article:
No rating

Please login or register to post comments.