Ramadhani ni fursa ya kuitakasa nafsi na kukuza tabia njema

Imeandaliwa na Dkt., Alaa Salah Abdulwahed

  • | Thursday, 27 February, 2025
Ramadhani ni fursa ya kuitakasa nafsi na kukuza tabia njema

 

Bila shaka, Mwenyezi Mungu (S.W.) Alipoainisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan uwe mwezi bora kuliko miezi yote Alikuwa na hekima ya kufanya hivyo, pengine hekima hiyo ni pamoja na kueleza kuwa mwezi huu ni fursa adhimu ya kupata rehema, radhi na maghufira ya Mwenyezi Mungu (S.W.)

Kwa kuangalia fadhila za mwezi huu mtukufu tunaona kuwa una mambo kadhaa yanayoufanya ni mwezi bora kuliko yote, kwa hiyo waislamu wanatakiwa kutumia nafasi ya kuja kwa mwezi huu ili watafute thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kwa hakika Mwenyezi Mungu (S.W.) Ameuelezea mwezi mtukufu wa Ramadhani ni mwezi bora kuliko miezi yote kwa kuwa Qurani imeteremka ndani ya mwezi huu unao usiku ulio bora zaidi kuliko miezi elfu moja nao ni usiku wa Al-Qadr.

Kwa mujibu wa Qurani Tukufu Mwenyezi Mungu Amebainisha kuwa Qurani imeteremka katika mwezi huu: {Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur'ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo waziza uwongofu na upambanuzi. Basi ataye kuwa mjini katika mwezi huu na afunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushukuru} [Al-Baqara: 185].

Hebu tujaribu kutaja baadhi ya fadhila za mwezi wa Ramadhani Mtukufu, ambapo katika mwezi wa Ramadhwaan kuna fadhila nyingi ambazo ni:

1)     NI MWEZI WA QUR-AAN

Kama Alivyosema Allaah Mtukufu: {Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur'ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo waziza uwongofu na upambanuzi.} [Al-Baqara: 185]. 

Vilevile kama ilivyopokewa na Ibn 'Abbaas (radhiya Allaahu 'anhu) kuwa makusudiyo yake   kwa hakika kuteremshiwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) Qur-aan mwanzo ni katika mwezi wa Ramadhwaan na vilevile Qur-aan mwanzo wa kuteremka ni usiku wa Laylatul-Qadir na Laylatul-Qadir iko katika mwezi wa Ramadhwaan. Hivyo basi ni juu yetu kufanya juhudi katika mwezi huu kukithirisha sana kusoma Qur-aan.

2)     NI MWEZI WA SUBIRA

Subira ni katika jambo gumu na halipati ila kwa mtu mchaji Allaah na mnyenyekevu kwa Allaah. Na katika kufunga kunatakiwa subira pale mtu anapojizuilia kutokana na kutokula, kunywa, matamanio na mengineyo. Imekua Swawm ni nusu ya subira na subira malipo yake ni pepo. 

3) MILANGO YA MOTO INAFUNGWA, MILANGO YA PEPO INAFUNGULIWA NA MASHETANI WANAFUNGWA

Kama ilivyokuja katika Hadiyth iliyopokelewa na Maimamu wawili:

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) amesema, "Pindi inapokuja Ramadhwaan inafunguliwa milango ya pepo, na hufungwa milango ya moto, na mashetani wanafungwa kwa Minyororo." [mesimuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim]

 Kwa hakika utaona katika mwezi huu watu wengi wanajitahidi kujiepusha na maasi, watu wanajaa misikitini kwa kufanya ibada ya mwezi huu hii ni kwa sababu mashetani wamefungwa na shetani juu ya uasi wake lakini anauogopa mwezi wa Ramadhwaan na vitimbi vyake vinakuwa dhaifu ndio mana wengi nyoyo zinabadilika wanaswali  na kujitahidi kufanya kheri.  Lakini ikimalizika Ramadhwaan tu basi Swalah imekwisha kama vile Allaah yupo Ramadhwaan tu. Huu ni msiba ndugu zangu Waislamu Allaah Asitujaalie katika hao.

 4)     LAYLATUL QADR

Katika mwezi huu kuna siku ya Laylatul-Qadr siku ambayo ni bora kuliko miezi elfu kama Alivyosema Allaah: {Hakika Sisi tumeiteremsha Qur'ani katika LaylatulQadri, Usiku wa Cheo Kitukufu * Na nini kitacho kujuulisha nini Laylatul Qadri? * Laylatul Qadri ni bora kuliko miezi elfu} [Al-Qadr: 1-3].

 Hakuna siku tukufu na kubwa kama siku hii ni wajibu kwetu kuutafuta usiku huu katika kumi la mwisho kufanya ibada ili tupate fadhila hizo. Ninamuomba Allaah atuwezeshe kwa hilo, Aamiyn.

 5)     DU'AA NI ZENYE KUKUBALIWA

Katika hadiyth iliyopokewa na Imaam Ahmad: Kutoka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwa isnadi iliyo nzuri Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) Amesema: "Kila Muislam du'aa zake ni zenye kukubaliwa atapomuomba katika mwezi wa Ramadhwaan"

6) MWEZI HUU NI MWEZI WA KUTOA

Na alikua Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akizidisha kheri nyingi katika mwezi wa Ramadhwaan. Imepokewa na At-Tirmidhiy kutoka kwa Anas (Radhiya Allaahu 'anhu) Kasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) "Bora ya (wakati wa) kutoa sadaqa ni kutoa katika mwezi wa Ramadhwaa.n"

 Na imepokewa na Zayd bin Aslam kutoka kwa babake, amesema nimemsikia 'Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu 'anhu) anasema, "Ametuamrisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) tutoe sadaqa nikatoa mali yangu nikasema leo nimemtangulia Abu Bakr nimekwenda na nusu ya mali, akasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) kuniambia, "Umewabakishia nini watu wako?" Nikasema, nusu kama hii, na akaja Abu Bakr na kila mali yake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akamuuliza, "Umewabakishia nini watu wako? Akasema, nimewabakishia Allaah na Mtume wake. Nikasema huyu Abu Bakr hapitiki na kitu chochote abadan"

Kuonyesha wema waliotangulia walikua wakishindana katika kheri lakini tofauti kubwa katika zama zetu hizi watu wanashindana katika mambo ya kidunia na kujifakharisha nayo.

Print
Categories: Makala
Tags:
Rate this article:
5.0

Please login or register to post comments.