Ramadhani ni Fursa ya Tawbah na kuomba Maghfirah

Imeandaliwa na Bw., Farid Mohammed

  • | Friday, 14 March, 2025
Ramadhani ni Fursa ya Tawbah na kuomba Maghfirah

 

Mwezi mtukufu wa Ramadhani ni fursa kubwa kwa Waislamu kuwa karibu na Mwenyezi Mungu, na ni msimu wa kuihuisha imani na kuitakasa nafsi na roho kutoka madhambi na maovu. Mwezi huu mtukufu haukomei kwenye swaumu ya vyakula na vinywaji tu, bali pia ni fursa ya kutubia na kusamehewa, kwani Ramadhani inachukuliwa kuwa ni kituo cha kiroho ambamo Mwislamu husimama ili kujihisabu na kurejea kwa Mwenyezi Mungu mwenye kutubia, akiomba msamaha na rehema zake. Amesema Mwenyezi Mungu:Enyi mlio amini! Mmefaradhiwa Saumu, kama waliyo faradhiwa walio kuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mwenyezi Mungu”. Sura ya ALbaqarah : aya 183.

Mwenyezi Mungu Anasema pia: ”Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur'ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi. Basi atakaye kuwa mjini katika mwezi huu naafunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuon-goeni ili mpate kushukuru." Sura ya ALbaqarah : aya 185

Tawbah katika mwezi wa Ramadhani

Tawbah ni kurejea kwa Mwenyezi Mungu baada ya kutenda maasi na madhambi, na ni miongoni mwa matendo makuu mema Anayoyapenda Mwenyezi Mungu mtukufu. Katika mwezi wa Ramadhani, fursa za msamaha huongezeka, na mlango wa Tawbah unafunguka kwa upana, imekuja katika hadithi mtukufu na kusimuliwa kutoka kwa mtume (S.A.W): "anayefunga Ramadhani akiwa na imani ya ufaradhi wake na akiomba thawabu kutoka mwenyezi mungu tu basi alighufiriwa madhambi yaliyotangulia". (wameafikiana juu yake)

Mwezi wa Ramadhani ni fursa ya kidhahabu ya kujiepusha na maasi na madhambi, kwani nyoyo huchangamshwa na kufunguliwa milango ya rehema na msamaha. Katika mwezi huu mtukufu, ufahamu wa kiroho wa Waislamu unaongezeka, jambo ambalo huwarahisishia kutubu na kurudi kwa Mwenyezi Mungu. Mja anayechukua fursa ya mwezi huu katika ibada na dua hujifungulia mlango wa nuru ambayo humtenga na dhambi na kumleta karibu na rehema za Mungu.

Msamaha wa Mungu katika Ramadhani

Miongoni mwa rehema ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa waja wake kwamba aliufanya mwezi wa Ramadhani kuwa ni msimu wa msamaha, na Akauhusisha kwa fadhila kubwa. Mojawapo ya fadhila hizo ni kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu Anazitoa shingo za waja wake wengi kutoka Motoni mwezi huu, na kuwasamehe madhambi yao yaliyotangulia. imekuja katika hadithi mtukufu na kusimuliwa kutoka kwa mtume (S.A.W): "Ikifika Ramadhani hufunguliwa milango ya Pepo, na hufungwa milango ya Moto, na mashetani hufungwa minyororo". (Imesimuliwa na Albukhary)

Sio lengo la ibada hii ya Swaumu kujizuilia na Kula na kunywa tu peke yake, lakini ni Madrasa ambayo huifundisha Nafsi juu ya kuwacha mabaya na maovu. Haya ndio malengo ya ibada yetu hii ambayo inafikia kikomo. Ndio Bwana Mtume (S.A.W) akatwambia katika Hadithi yake: "Yeyote ambaye hatowacha kusema uongo na kutenda kwa uongo basi Allaah (S.w.T) hana haja yake kwa kuwacha chakula chake na kinywaji chake kwa ajili yangu". (imesimuliwa na Albukhary)

Mazingira haya ya kiroho ambayo yametawaliwa na dua, ukumbusho na tasbihi, yanawakilisha fursa kwa Muislamu kuomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu. Wakati wa Ramadhani, Waislamu wanahimizwa kuomba msamaha mara kwa mara, kuswali, na kusoma Qur’ani Tukufu, zote hizo ni njia za kuongeza upataji wa msamaha.

Tawbah na msamaha baina ya mja na Mola wake Mlezi

Moja ya maana nzuri sana ya Tawbah na msamaha katika Ramadhani ni kuwa ni uhusiano wa kibinafsi kati ya mja na Mola wake. Katika mwezi huu mtukufu, Mwislamu anajihisi yuko karibu na Mola wake, na anaomba msamaha kwa dhati na anajutia alichokosa. Swahaba mkubwa Abdullah bin Abbas (R.A) anasimulia kutoka kwa Mtume (S. A.W) kwamba alisema: "Ewe Mola, Wewe ni Mwenye kusamehe na Unapenda kusamehe, basi nisamehe". (Imesimuliwa na Al-Tirmidhiy). dua hii inaangazia ukuu wa msamaha wa Mwenyezi Mungu, na inaonyesha kwamba Mwenyezi Mungu anapenda kuwasamehe waja Wake.

Ramadhani ni mwezi ambao matumaini ya Waislamu yanafanywa upya, wanapoelekea kwenye Mwenyezi Mungu kwa moyo wa kweli, wakimwomba rehema na msamaha. Ni fursa nzuri ya kutakasa roho na kuondoa madhambi na makosa nyoyoni mwao, na ndani yake msamaha wa Mungu na rehema kubwa hudhihirishwa. Siku hizi zenye baraka ziwe fursa kwa kila Muislamu kutubia kwa dhati na kurejea kwa Mwenyezi Mungu kwa mioyo yenye unyenyekevu.

Print
Categories: Makala
Tags:
Rate this article:
No rating

Please login or register to post comments.