Tabia Njema Msingi Muhimu wa Jamii Imara

Imaendaliwa na Dkt., Alaa Salah Abdulwahed

  • | Monday, 5 May, 2025
Tabia Njema Msingi Muhimu wa Jamii Imara

 

    Inafahamika kwamba ubora wa maisha ya waislamu unategemea kiwango walicho nacho kutoka tabia njema ambazo zina umuhimu mkubwa mno katika dini hiyo, mpaka Mtume (S.A.W.) alijumlisha malengo ya utume wake katika kauli yake: "Hakika nimetumwa kwa ajili ya kutimiza tabia njema". Tabia hizo ni kipimo cha kusanifisha jamii na kufanikiwa kwake, ambapo jamii bora ni ile inayofuata maadili ya kibinadamu na tabia njema baina ya watu wake kwa kusifika kwa sifa nzuri kama vile; ushujaa, ukarimu, ukweli, huruma, rehma, uaminifu, uadilifu n.k.

Qurani Takatifu inahimiza sifa na tabia njema na kusimulia visa kadha wa kadha kueleza ubora na utukufu wa tabia hizo, kuhusu ushujaa wa Nabii Mussa (A.S.) na nguvu wake katika haki Mwenyezi Mungu Amesema: {Na alipo yafikia maji ya Madyana alikuta umati wa watu wananywesha (wanyama wao), na akakuta karibu yao wanawake wawili wanawazuia wanyama wao. Akasema: Mna nini? Wakasema: Hatunyweshi sisi mpaka wamalize hao wachunga. Na baba yetu ni mzee sana * Basi Musa akawanyweshea; kisha akarudi kivulini, na akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika mimi ni mhitajiwa kheri utakayo niteremshia * Basi mmoja katika wale wanawake wawili akamjia, naye anaona haya. Akasema: Baba yangu anakwita akulipe ujira wa kutunyweshea. Basi alipo mjia na akamsimulia visa vyake, alisema: Usiogope; umekwishaokoka kwenye watu madhaalimu * Akasema mmoja katika wale wanawake: Ewe baba yetu! Muajiri huyu. Hakika mbora wa kumuajiri ni mwenye nguvu na muaminifu} [28/23-26].

Pia, tunasoma kisa cha Nabii Yusuf (A.S.) na tabia alizokuwa nazo na namna alivyoweza kujiokoa kutoka mtihani mgumu wa Mke wa Bwana wake aliyetaka kumlaghai lakini kwa kuwa tabia yake na sifa nzuri Mwenyezi Mungu Alimwokoa kama ilivyokuja katika Qurani: {Na yule bibi wa nyumba aliyo kuwamo Yusuf alimtamani kinyume cha nafsi yake, na akafunga milango. Akamwambia: Njoo! Yusuf akasema: Audhubillahi! Najikinga na Mwenyezi Mungu. Huyu bwana wangu kaniweka maskani nzuri, na hakika wenye kudhulumu hawatengenekewi} [12/23] Na kwa sababu ya tabia njema na maadili yake Yusuf alipandishwa cheo akawa msaidizi wa mfalme baada ya kuwa mfungwa: {Basi mfalme akasema: Mleteni kwangu, awe wangu mwenyewe khasa. Basi alipo msemeza alinena: Hakika wewe leo umekwisha tamakani kwetu na umeaminika * Yusuf akasema: Nifanye mshika khazina za nchi. Kwani hakika mimi ni mlinzi mjuzi * Basi namna hivi tukampa Yusuf cheo katika nchi; anakaa humo popote anapo penda. Tunamfikishia rehema zetu tumtakaye, wala hatupuuzi malipo ya wafanyao mema * Na hakika malipo ya Akhera ni bora zaidi, kwa walio amini na wakawa wachamngu} [12/54-57].

Kwa hivyo, tunatambua vipi dini yetu adhimu inategemea na kuzingatia sana tabia njema na maadili mema, mbali na visa vya Manabii na Mitume, tunaona Qurani Takatifu inatoa wito wa kutakasisha tabia na kuchunga maadili kwani ni sababu ya kutukuka kwa umma wowote. Mwenyezi Mungu Amesema: {Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha kufanya uadilifu,na hisani, na kuwapa jamaa; na anakataza uchafu, nauovu, na dhulma. Anakuwaidhini ili mpate kukumbuka} [16/90]. Na tukifuatilia aya za Qurani Tukufu tutaelewa kuwa tabia njema ndiyo msingi muhimu wa umma wetu huu na hakuna dalili lililo wazi zaidi kuliko kumsifu Mtume kwa: {Na hakika wewe una tabia tukufu} [68/4]. Na kauli yake Mtume alipotaka kubainisha lengo kuu la utume wake: "Hakika nimetumwa kwa ajili ya kutimiza tabia njema".

Kwa upande mwingine, Qurani Tukufu ilituhadithia kuhusu hatima ya tabia mbaya na ukosefu wa maadili na sifa nzuri na namna ilivyokuwa hali hii sababu ya kuporomoka na kusambaratika kwa jamii na staaraabu nyingi duniani. Mwenyezi Mungu Amesema: {Na pindi tukitaka kuuteketeza mji huwaamrisha wale wenye starehe na taanusi, lakini wao huendelea kutendamaovu humo. Basi hapo kauli huthibiti juu ya mji huo, nasi tukauangamiza kwa maangamizo makubwa} [17/16] na Qurani na Sunna imejaa visa vya umma zilizoangamizwa kwa sababu ya tabia zake mbaya, mifano ni kama vile; kaumu wa Manabii Hudu, Swaleh, Luut, Shuaieb na wengine ambao walichafuka kitabia wakastahiki kuadhibiwa duniani na adhabu ya akhera ni kali zaidi.

Aya nyingi katika Qurani zimesimulia visa vya umma hizo, kuhusu kaumu Aad Mwenyezi Mungu Amesema: {Ama kina A'di walijivuna katika nchi bila ya haki,na wakasema: Nani aliye kuwa na nguvu kushinda sisi?Kwani wao hawakuona kwamba Mwenyezi Mungu aliye waumba ni Mwenye nguvu kushinda wao? Na wao wakawawanazikataa Ishara zetu! * Basi tuliwapelekea upepo wa kimbunga katika sikuza ukorofi, ili tuwaonjeshe adhabu ya kuwahizi katikauhai wa duniani, na bila ya shaka adhabu ya Akhera inahizaya zaidi, na wala wao hawatanusuriwa} [41/15-16]

Na kuhusu kaumu wa Nabii Swaleh Mwenyezi Mungu Amesema: {Na walikuwamo mjini watu tisa wakifanya ufisadi katika nchi wala hawafanyi la maslaha} [27/48] Ama kaumu Luut Mwenyezi Mungu Amesema: {Na pale Lut'i alipo waambia watu wake: Hakika nyinyi mnafanya uchafu, ambao hapana mmoja katika walimwengu aliye kutangulieni kwa hayo * Je! Nyinyi mnawaingilia wanaume, na mnaikata njia? Na katika mikutano yenu mnafanya maovu? Basi haikuwa jawabu ya watu wake isipo kuwa kusema: Tuletee hiyo adhabu ya Mwenyezi Mungu ikiwa wewe ni katika wasemao kweli * Akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Ninusuru na watu mafisadi hawa!} [29/28-30]

Hali hiyo hiyo ilikuwa na kaumu wa Nabii Shueib kama ilivyosimuliwa katika Qurani Tukufu: {Na kwa watu wa Madyana tulimtuma ndugu yao Shua'ib. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Hamna mungu mwengine isipo kuwa Yeye. Imekwishakufikieni hoja wazi kutoka kwa Mola Mlezi wenu. Basi timizeni sawasawa vipimo na mizani, wala msiwapunje watu vitu vyao, wala msifanye uharibifu katika nchi, baada ya kuwa imekwisha tengenea. Hivi ndivyo bora kwenu ikiwa nyinyi ni Waumini * Wala msikae katika kila njia mkitisha watu, na kuwazuilia na Njia ya Mwenyezi  Mungu wale wenye kumuamini, na mkataka njia ipotoke. Na kumbukeni mlipokuwa wachache, naye akakufanyeni kuwa wengi. Na tazameni jinsi ulivyo kuwa mwisho wa mafisadi} [7/85-86].

Hivyo ndivyo, mtazamo wa Uislamu kuhusu tabia njema na athari ya kuutekeleza katika hali halisi ya maisha ya walimwengu wote kwa jumla na hasa hasa waislamu na jamii za kiislamu.

Print
Categories: Makala
Tags:
Rate this article:
No rating

Please login or register to post comments.