Mwezi wa Dhul-Hijjah ni miongoni mwa miezi mitukufu katika Uislamu, na ndani yake mna siku kumi za mwanzo ambazo zina daraja kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu S.W, Siku hizi ni kipindi adhimu chenye baraka, fursa, na thawabu nyingi kwa waumini. Ni wakati wa kuonyesha ibada, unyenyekevu, na kujikurubisha kwa Mola kwa njia mbalimbali.
Dalili za kisheria kuhusu siku kumi za Dhul-Hijjah na fadhila zake
Mwenyezi Mungu S.W Anasema: "Naapa kwa alfajiri, Na kwa masiku kumi" (Surat Al-Fajr: 1-2), Wanazuoni wengi wa tafsiri, wakiwemo Ibn Kathir, Al-Tabari, na wengine, wameeleza kuwa "masiku kumi" yanayokusudiwa katika aya hii ni siku kumi za mwanzo za Dhul-Hijjah, Hili linaonyesha daraja na utukufu wake kwenye Mwenyezi Mungu S.W.
Pia Mtume S.A.W amesema: "Hakuna siku ambazo matendo mema yanapendwa zaidi kwa Mwenyezi Mungu S.W kuliko hizi siku kumi." Wakasema: "Hata jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, Ee Mtume wa Mwenyezi Mungu?" Akasema: "Hata jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, isipokuwa mtu aliyetoka na nafsi yake na mali yake, kisha hakurudi na chochote".
Hii hadith inaonyesha kwamba matendo mema katika siku hizi yana uzito mkubwa hata zaidi ya jihadi – isipokuwa jihadi ya kujitolea kikamilifu mpaka kufa shahidi.
Fadhila za Siku Kumi za Dhul-Hijjah
1. Ni siku bora zaidi katika mwaka: Mtume S.A.W amesema: "Hakuna siku ambazo matendo mema yanapendwa zaidi kwa Mwenyezi Mungu kuliko hizi siku kumi".
2. Ndani yake kuna siku ya Arafah: Siku hii ina daraja kubwa, hasa kwa wasiokwenda kuhiji. Mtume S.A.W alisema: "Funga ya siku ya Arafah inafuta madhambi ya mwaka uliopita na ujao".
3. Ni kipindi cha Hajj na ibada kubwa: Mahujaji hufanya ibada zao muhimu zaidi katika siku hizi, kama kusimama Arafah, kutupa mawe, kuchinja, na kutawafu.
4. Ndani yake kuna siku ya Eid Al-Adhha: Ni siku ya kuchinja na kufurahikia neema ya Mwenyezi Mungu, na pia ni siku ya ibada.
Matendo Mema Yanayopendekezwa Katika Siku Hizi
1. Kumuadhukuru Mwenyezi Mungu: kupitia Tahlil (La ilaha illa Allah), Takbir: (Allahu Akbar) Tahmid (Alhamdulillah) Wanazuoni wamesema kuwa ni sunna kusema adhkari hizi kwa sauti hadharani kwa wanaume, na kwa utulivu kwa wanawake.
2. Kufunga: Kufunga katika siku hizi hususan kwa wasiokwenda kuhiji kunaleta thawabu nyingi, na ni njia ya kujitakasa, Mtume S.A.W amesema: "Funga ya siku ya Arafah, ninatarajia kwa Allah kufuta madhambi ya mwaka uliopita na wa mwaka unaofuata", Funga hii ya Arafah ni kwa ajili ya wasiokuwa mahujaji, kwa sababu mahujaji wako katika ibada maalum ya kusimama Arafah.
3. Sala na Qur’an: Kuthibitisha sala tano kwa wakati, kusali sunnah, na kusoma Qur’an kwa wingi.
4. Kutoa sadaka na kuamrisha mema: Kutumia fursa hii kusaidia masikini, yatima, na wenye uhitaji, pia kuchangia katika miradi ya kheri.
5. Kuchinja kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (Udh-hiyah): Ni sunna kwa mwenye uwezo kuchinja mnyama siku ya Eid kama alivyofanya Mtume S.A.W, aliye na nia ya kuchinja, inapendekezwa asikate nywele au kuchuna ngozi kuanzia mwanzo wa Dhul-Hijjah hadi atakapochinja, Mtume S.A.W amesema: "Mwanadamu hajafanya kitendo chochote siku ya Eid al-Adh-ha kinachopendwa zaidi kwa Allah kuliko kumwaga damu ya mnyama (udh-hiyah)... na hakika damu yake itafika kwa Allah kabla ya kugusa ardhi…". Hadith hii inaonyesha utukufu wa ibada ya kuchinja kama njia ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu S.W.
6. Kutubu na kuomba msamaha: Huu ni wakati wa kurekebisha uhusiano na Mwenyezi Mungu S.W, kuomba msamaha, na kuacha madhambi.
Mwishoni, Siku kumi za mwanzo za Dhul-Hijjah ni miongoni mwa nyakati bora zaidi za ibada, ni hazina ya neema na fursa ya kufukia kwa ucha Mungu, ni wakati wa kujitahidi kwa kila namna katika ibada na matendo mema, ni fursa ya kujenga daraja ya juu mbele ya Mwenyezi Mungu S.W, kwa moyo wa ikhlasi, kwa bidii, na kwa matumaini ya maghfira na radhi ya Mola. Mwislamu anapaswa kuzichukua kwa uzito, ajitahidi kufanya matendo mema kwa wingi, kwani ni nyakati chache na zenye thawabu nyingi zisizopatikana wakati mwingine wowote wa mwaka, Mwislamu mwenye hekima hatapuuza siku hizi, bali atazitumia kwa shukrani na juhudi.