Siku ya Arafah, inayoafikiana na tarehe 9 Dhul-Hijjah katika kalenda ya Kiislamu, ni miongoni mwa siku tukufu kabisa katika Uislamu, yenye fadhila kubwa na maana za kiroho za hali ya juu. Katika siku hii, mamilioni ya mahujaji husimama katika kiwanja kitakatifu cha Arafah, wakimwelekea Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa dua na unyenyekevu na utiifu kwa ajili ya kusamehewa madhambi yao yote hadi wakirudi kama wamezaliwa upya. Mbali na ibada, siku ya Arafah pia hubeba ujumbe mzito wa umoja wa Waislamu.
Arafah ni hali Halisi ya Umma Mmoja
Katika siku ya Arafah, watu kutoka kila kona ya dunia, husimama mahala pamoja, wakiwa wamevaa vazi moja linalofuta tofauti zote za kijamii na kiuchumi, bila ya kuangalia rangi, lugha, hadhi na taifa. Hii ni ishara wazi kuwa Waislamu ni umma mmoja, wanamwabudu Mola Moja, wanamfuata Mtume Mmoja, wanasoma Kitabu Kimoja, wana lengo moja kuu la kutafuta radhi za Allah.
Arafah ni wito wazi wa kuepuka migawanyiko
Ijapokuwa Umma wa Kiislamu katika zama hizi unakabiliwa na migogoro ya kimadhehebu, kisiasa na kijamii, lakini Siku ya Arafah huja kutukumbusha kuwa umoja juu ya misingi ya dini ndiyo njia sahihi ya kupata nguvu na heshima. Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema: "Shikamaneni na kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msigawanyike", [Al 'Imran: 103] na siku ya Arafah ni mfano hai wa aya hii.
Katika siku hii hakuna vyeo wala nasaba; kila mtu husimama mbele ya Mola wake akiwa mnyenyekevu. Taswira hii huimarisha thamani za usawa, kusameheana na utu, ambavyo ni msingi wa umoja wa kweli. Mtume Muhammad (S.A.W) katika hotuba ya kuaga siku ya Arafah alisema: "Nyote mmetokana na Adamu, na Adamu aliumbwa kwa udongo. Hakuna ubora wa Mwarabu juu ya asiye Mwarabu isipokuwa kwa taqwa."
Hatimaye, Arafah si siku tu ya kusimama na kuomba, bali ni siku ya urudishaji wa ahadi ya kuwa Umma mmoja, wenye maono ya pamoja na moyo wa kushirikiana. Je, hatutaitumia siku ya Arafah kama mwanzo mpya wa safari ya umoja wa kweli? Tunarudia kusema kwamba Umoja wa Waislamu si kauli tu ya maneno, bali ni wajibu wa kidini na jukumu la pamoja linalohitaji uelewa, kujitolea, na juhudi za dhati katika kuimarisha roho ya udugu na mshikamano kati ya Waislamu. Katika wakati huu ambapo Uislamu unakabiliwa na changamoto kubwa duniani, ni lazima tutafakari sababu za migawanyiko na kujitahidi kwa moyo wa kweli kujenga umoja wa kweli unaojengwa juu ya maadili na misingi ya Uislamu. Kwa umoja tutajenga ustawi wetu, na kwa migawanyiko tutadhoofika. Basi na iwe kauli yetu mbiu: “Nguvu yetu imo katika umoja wetu, na wokovu wetu uko katika kuwa na kauli moja.”